Home Makala KIM YO JONG ‘GRISI’ INAYOLAINISHA DIPLOMASIA KOREA KASKAZINI

KIM YO JONG ‘GRISI’ INAYOLAINISHA DIPLOMASIA KOREA KASKAZINI

1359
0
SHARE

Na MARKUS MPANGALA


OKTOBA 8, mwaka jana, Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alimpandisha cheo dada yake, Kim Yo Jong, na kumpa madaraka zaidi kwenye chama tawala—Chama cha Wafanyakazi. Watu wengi walijiuliza swali moja kuu: Ni nani huyu Kim Yo Jong ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama au Baraza Kuu la Uamuzi ndani ya Korea Kaskazini linalojulikana kama Politburo.

Wakati akipandishwa cheo, hakuna aliyekuwa akifikiria kuwa siku moja Kim Yo-jong, atavaa viatu vya ‘upatanishi’ na ‘kulainisha’ diplomasia ya Korea Kaskazini dhidi ya mahasimu wao Korea Kusini, pamoja na Marekani kama ilivyotokea Februari 8, mwaka huu kwenye uzinduzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi. Haikufikiriwa wala kutabiriwa, lakini inatokea sasa.

Kim Yo Jong ametembelea Korea Kusini kumwakilisha kaka yake  na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Korea zote mbili, ziliandamana pamoja chini ya bendera moja katika sherehe za uzinduzi huo.

Ushiriki wa Korea Kaskazini umeonekana kama kulegeza uhusiano baina ya nchi hizo mbili. Hata hivyo, Marekani na Japan wameishtumu Korea Kaskazini kwa kutumia michezo hio kama chombo cha propaganda.

Nilikuwa natazama televisheni ya Africanews matukio yote ya uzinduzi wa michezo hiyo ya Olimpiki. Awali kabla ya uzinduzi, sikuamini macho yangu pale nilipoona walinzi takribani 10 wakiwa wamemzunguka Kim Yo Jong akiwa ameambatana na Mkuu wa Serikali wa nchi yake, Kim Yong Nam, wakishuka kwenye ndege na kukanyaga ardhi ya Korea Kusini na hata pale alipokuwa akizuru maeneo mbali mbali nchini humo. Ilikuwa kama rais wa nchi fulani anaitambelea Korea Kusini.

Kim Yo Jong alivaa koti refu la kukinga baridi lenye rangi nyeusi, mkoba mweusi na mwonekano wenye kila dalili za urembo na mvuto. Aliongozana na maofisa wengine watatu kutoka Korea Kaskazini katika vikao vya kuwakilisha nchi yao. Kim Yo Jong alionekana mtulivu, mcheshi na ‘turufu ya kuaminika’ ya Korea Kaskazini mbele ya rais wa Korea Kusini,  Moon Jae-in, aliyetwaa madaraka hayo mwaka jana na kuahidi kuzungumza na Kim Jong Un.

Makutano ya viongozi nchi zote mbili  yanatoa ishara ya nyota  njema ya kidiplomasia katika siku zijazo, baada ya kushindikana katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Mkutano huo pia unapunguza  ‘msuguano’  uliochochea kuingia vitani katika miaka 1950.

Niwakumbushe wasomaji kuwa Korea lilikuwa taifa moja kabla ya kugawanyika. Korea Kusini tangu awali ilikuwa na vimelea vya uongozi unaojinasibu kwa kufuata mkondo wa itikadi ya kibepari. Wenzao Korea Kaskazini walikuwa na vimelea ya ujamaa na baadaye ukomunisti.

Korea Kaskazini walisaidiwa na nchi zenye kufuata falsafa ya ujamaa za China na Urusi kwa wakati huo. Wakati Korea Kusini ilikuwa na inaendelea kuwa ‘rafiki mzuri’ wa Marekani na washirika wake—ikiwa ni pamoja na Japan ambayo ni hasimu wa Korea Kaskazini.

Awali Kim Jong Un, alipomteua dada yake Kim Yo Jong  kwanza alipewa wadhifa wa kuwa Afisa wa cheo cha juu katika chama, miaka mitatu iliyopita. Ikumbukwe familia ya Kim, imeongoza Korea Kaskazini, tangu nchi hiyo ilipoundwa, mwaka wa 1948.

KIM YO JONG NI NANI?

Tatizo jingine hakuna tarehe sahihi ya kuzaliwa mwanadada huyu.  Utata uliopo kwenye vyombo vya habari vinabashiri kuwa ana miaka 28, huku vingine vikimtaja kuwa na miaka 30. Vyombo vingi katika ulimwengu huu, havina taarifa za kutosha kuhusu maisha ya familia hiyo ikiwemo elimu, marafiki, ndugu na jamaa—ukiacha zile zinazotolewa na serikali ya Korea Kaskazini.

Inaelezwa kuwa Kim Yo Jong alizaliwa mwaka 1987, ni mtoto wa kike wa mwisho wa hayati Kim Jong-il na ni dada yake wa tumbo moja kiongozi wa sasa wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Tunaambiwa kuwa anazidiwa umri na kaka yake (Kim Jong Un) kwa miaka minne na inasemekana kwamba wana uhusiano wa karibu sana.

Aidha, inadaiwa ameolewa na mtoto wa katibu wa chama tawala, Choe Ryong Hae.  Inaelezwa kuwa Choe Ryong Hae ni mshauri muhimu wa Kim Jong Un. Vilevile Kim Yo Jong amekuwa akionekana sana miaka ya hivi karibuni, ikiwa kazi yake kuu ni kulinda taswira ya kaka yake kupitia cheo chake cha Mkurugenzi wa Propaganda ya chama na taifa. Gazeti la Business Insider, limesema kuwa ziara ya Kim Yo Jong, ni ya kwanza kwa mwanafamilia yao kwenda Korea Kusini.

Kuhusu elimu , Kim Yo Jong  na Kim Jong Un walisoma nchini Uswisi kuanzia mwaka 1996 hadi 2000 katikati ya usiri mkubwa sana, huku ikidaiwa kuwa walitumia majina ya bandia kuficha utambulisho wao kama watoto wa utawala wa Korea Kaskazini. Wakiwa masomoni ndipo undugu wao ulibainishwa zaidi kwani waliishi ugenini wakiwa wapweke bila wazazi wao. Kim Yo Jong amewahi kusoma Chuo Kikuu cha Kijeshi cha  Kim Il-sung (Kim Il-sung Military University) mara baada ya kurejea nchini akitokea masomoni Uswisi. Alisoma Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Kim Il-sung. Inasemakana amesoma pamoja na Kim Eun-gyong ambaye ni binti wa  Megumi Yokota

KOREA KUSINI NA MAREKANI?

Katika ziara yake nchini Korea Kusini, Kim Yo Jong alikuwa na ujumbe mahsusi kwa mwenyeji wake Moon Jae-in. Ujumbe huo ulitoka kwa Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un unaomtaka Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in atembelee Pyongyang, ili wafanye mazungumzo baina yao.

Kim Yo Jong anafanya kazi ambayo kwenye masuala ya magari tungesema amekuwa ‘grisi’ (inayolainisha vyuma)—kulainisha msuguano na uhasama uliotamalaki kati ya Korea Kusini na Marekani kwa upande mmoja, na Korea Kaskazini ambayo imewekewa vikwazo sababu ya utengenezaji wa silaha za nyukilia.

Hata hivyo Rais Moon amesema kuwa Korea Kusini inataka kuhakikisha kuwa mkutano huo unafanyika huku akiitaka Korea Kaskazini kurudi katika meza ya mazungumzo na Marekani. Mwaliko huo uliandikwa kwa mkono wa Kim Jong Un.

Kim Yo Jong amekuwa na wakati mzuri kwani huambatana na ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu zaidi wa Korea Kaskazini kuwahi kuzuru Korea Kusini tangu kumalizika kwa vita vya Korea miaka 60 iliyopita.

Hata hivyo hatua hiyo imewakera serikali ya Marekani ambayo ilimtuma Makamu wa Rais, Mike Pence, kuhudhuria sherehe za uzinduzi wa mashindano ya Olimpiki. Pence alisusia mwaliko wa chakula cha jioni ambacho alitakiwa kukaa meza moja na Kiongozi wa Serikali ya Korea Kaskazini, Kim Yong-nam.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Yo Hap, limesema kuwa chanzo cha msuguano kati ya Marekani na Korea Kaskazini, ni mvutano juu ya mpango wa nyukilia wa Korea Kaskazini ambao unapingwa vikali na majirani zake Japan, Korea Kusini pamoja na hasimu wao Marekani.

Kwa upande wake Rais wa Korea Kusini, ametoa masharti kabla ya kukubali mwaliko wa Kim Jong Un. Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-yeon, amebainisha kwamba kuna masharti ambayo lazima yabainishwe kabla ya kukubali mwaliko wa uongozi wa nchi hiyo kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.

Korea Kusini imesema kuwa itakutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, iwapo atakuwa tayari kukaa mezani kuzungumza na Marekani katika mzozo wa nyukilia. Hapo ndipo ilipo changamoto ya Kim Yo Jong kuhakikisha anazilainisha Korea Kusini na Marekani. Je ataweza hilo?