Home Makala Kitakachofanyika kupata mbadala iwapo Clinton atajitoa

Kitakachofanyika kupata mbadala iwapo Clinton atajitoa

734
0
SHARE

HILAL K SUED

Jumapili iliyopita mgombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa Novemba 8 mwaka huu, Hillary Clinton alizimia katika hafla moja jijini New York ya kuadhimisha miaka 15 ya ulipuaji majengo jijini humo.

Picha za video zilizosambaa zilimuonyesha akisaidiwa na wapambe wake kuingizwa kwenye gari na madaktari wake walisema alikuwa amepatwa na kichomi (pneumonia) na hivyo kukaukiwa na maji mwilini (dehydration).

Haitarajiwi kwamba tukio hili la afya ya mgombea huyo wa chama cha Democratic linaweza kuzorota zaidi hadi kumfanya ashindwe kuendelea na kampeni na/au kujitoa kwenye kinyang’anyiro, kwani zimebaki chini ya miezi miwili hadi siku ya uchaguzi.

Aidha, katika hafla na mikutano mingine mgombea huyo mwenye nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi alisikika akikatiza katiza hotuba zake kwa kwa kukohoa. Mwezi ujao kutafanyika midahalo baina ya wagombea wawili hao hivyo kuna hofu kubwa matukio haya yaweza kujirudia.

Lakini tayari wachunguzi wa mambo wanatoa tahadhari na tathmini – kwamba iwapo hilo la kushindwa kuendelea na kampeni na kujitoa, kitu gani kitafanyika kwa chama hicho kumpata mgombea mwingine katika kipindi hiki kilichobakia, kufuatana na matakwa ya Katiba, sheria na kanuni zilizopo?

Kusema kweli hali ya namna hii ikitokea itakuwa haina mfano wa huko nyuma katika medani ya siasa za Marekani na kwamba wengi hawajui nani atakuwa mgombea mbadala. Je atakuwa Tim Kaine (mgombea mwenza) na ambaye jina lake huwa lipo katika karatasi ya kupigia kura?

Au atakuwa ni Joe Biden, Makamu wa rais wa sasa au Bernie Sanders, mpinzani wa karibu wa Clinton katika kinyang’anyiro cha mchakato wa kuteua mgombea katika chama? Je kutakuwapo vipingamizi kuwaweka hawa katika karatasi za kupiga kura katika kila jimbo nchini humo?

Lakini mwanzo wa jibu kwa maswali haya yanakuja kutokana Katiba ya Baraza Kuu la chama chake – Democratic National Committee (DNC) Charter & Bylaws – ambayo ilifanyiwa mapitio mwaka mmoja uliopita.

Yafuatayo ndiyo maelezo halisi katika Katiba hiyo kuhusu suala kama hili linapoibuka:

“Kikao maalumu cha Baraza Kuu (DNC) kinaweza kikaitishwa na mwenyekiti na kubarikiwa na Wajumbe wa kamati ya Uongozi wa Baraza na wajumbe wa Baraza kupewa taarifa mapema. Na hakuna hatua yoyote inaweza kuchukuliwa hadi kwanza taarifa kamili ya agenda ya kikao hicho kielezwe.

Pamoja na hayo, kikao maalumu cha kujaza nafasi iliyoachwa wazi kitaitwa na Mwenyekiti ambaye ataweka tarehe ya Kikao hicho Maalumu kufuatana na kanuni za muongozo kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha Pili, Ibara ya 8(d) ya Katiba ya Chama.

Inawezekana hii bado haieleweki kinagaubaga. Kwa ujumla muongozo wenyewe unaotajwa unachosha kuusoma lakini yafuatayo ndiyo yatatakiwa kufanyika:

 

  • Ila tu itakavyoelezwa vinginevyo katika Katiba, mijadala yote ya Baraza kuu la Chama itafanyika kwa maazimio ya uwingi wa wajumbe waliohudhhuria kwa kupiga kura halisi au kwa wakala (proxy voting).

 

  • Uhitaji majina mmoja mmoja unaweza ukaombwa iwapo asilimia 25 ya Wajumbe watapiga kura kutaka hivyo

 

  • Akidi ya kuendelea na kikao itapatikana iwapo si chini ya asilimia 40 ya wajumbe wote wa Baraza Kuu (DNC) watakuwepo kwenye kikao, na kama agenda ya kikao ni kujaza nafasi iliyoachwa wazi katika ngazi ya kitaifa, basi sharti wajumbe wote wa Baraza wawepo bila kukosa hata mmoja.

Aidha kuna kanuni inayosema kwamba kutakuwa hakuna kupiga kura kwa kupitia wakala (proxy voting) iwapo mjadala ni kujaza nafasi ya ngazi ya kitaifa, lazima kila mjumbe apige kura mwenyewe binafsi.

Kwa ujumla ni kwamba kanuni zipo kama zilivyoorodheshwa ambazo ni kama zinaonyesha hakuna kanuni. Hivyo iwapo Clinton atajiondoa basi Mwenyekiti wa sasa wa Baraza Kuu (DNC) Donna Brazile ataitisha kikao maalum ambacho matokeo yake ndiyo yatatoa mwanga – achilia mbali mkanganyiko huo wa kanuni uliopo.

Swali kubwa ni je, hata baada ya kikao cha Baraza Kuu kuamua nani ajaze nafasi, kunaweza kuwa vikwazo katika kuliweka jina lake katika karatasi za kura siku ya kupiga kura katika kila jimbo (yako majimbo 50).

Hii ni kwa sababu Marekani haina Tume moja ya uchaguzi ya taifa kama hapa Tanzania – kila jimbo lina Tume yake inayofanya kazi chini ya sheria na kanuni za jimbo husika zinazotungwa na mabunge ya majimbo hayo.

Uchaguzi wa Rais (na wa Wabunge wa Senate na Baraza la Wawakilishi) husimamiwa na tume za uchaguzi za majimbo kama wakala kwa niaba ya serikali ya shirikisho – Federal Government.

Hivyo basi haitakuwa rahisi katika kuliwweka jina la mbadala wa Clinton katika karatasi za kupigia kura katika kila jimbo.

Na hali itakuwa ngumu zaidi kwa mfano iwapo Clinton atajitoa ndani ya mwezi mmoja kabla ya siku ya uchaguzi, na hivyo vyama vijiweke tayari kutafuta suluhu ya mahakama na hilo limefanyika huko nyuma ingawa si katika ngazi ya ugombea wa urais.

Mwaka 2002 Mahakama Kuu ya Jimbo la New Jersey iliamuru chama hicho hicho cha Democratic kuwweka jina mbadala la aliyekuwa mgombea wa wa kiti cha Senate la Jimbo hilo siku 15 baada ya tarehe ya mwisho ya uhakiki

Na imekuwa kawaida kwa mamlaka za uchaguzi za kila jimbo kulekeza kamba katika masuala kama haya yanapojitokeza – hasa kuhusu tarehe za mwisho (deadlines).

Hivyo basi katika hali ya kawaida – na ya mazoea – hasa katika chaguzi za nafasi hizi za chini, inatarajiwa iwapo Bi Clinton atashindwa kuendelea na kampeni na hivyo kujitoa, basi mamlaka za uchaguzi katika kila jimbo zitakuwa tayari kuweka juina mbadala katika karatasi za kupigia kura hata pale tarehe ya mwisho ya uhakiki imepita.

Hata hivyo kuna suala jingine linaloweza kuleta vikwazo – iwapo chama pinzani cha Republican kitakwenda mahakamani kudai sheria za kila jimbo kuhusu masuala ya uchaguzi zifuatwe kikamilifu na kutioruhusu kubadilisha majina katika karatasi ya kupiga kura.

Lakini wachunguzi wa mambo wanasema mapambano ya mahakama kuhusu suala hili yanaweza kuchukua muda mrefu na rasilimali fedha nyingi kwa kila upande.

Wanakumbushia ule mpambano wa kimahakama ulioibuka wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000 – hususan uhesabuji kura katika jimbo la Florida. Ilikuwa ni kinyang’anyiro cha urais baina ya George W Bush wa Republican na Al Gore wa Democratic.

Suala hili hatimaye lilitinga Mahakama ya Juu katisa nchini humo (Supreme Court) ambako Bush alishinda kwa maamuzi ya Majaji 5-4 dhidi ya Al Gore.

  • Makala hii imetayarishwa kwa msaada wa vianzo mbalimbali vya Intaneti.