Home Makala KIVULI CHA LOWASSA CHAWATESA WAGOMBEA CCM MBEYA

KIVULI CHA LOWASSA CHAWATESA WAGOMBEA CCM MBEYA

1261
0
SHARE

NA GORDON KALULUNGA


CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM) tayari kimeanza chaguzi zake

kuanzia ngazi ya mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa.

Nafasi ambazo zitawaniwa ni nyingi zikiwemo nafasi za mabalozi, wenyeviti, wajumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa (NEC), wasemaji wa chama hicho ngazi za kata, wilaya, mikoa (Waenezi) na nafasi nyingine za chama na jumuiya zake.

Katika kikwazo ambacho kitajitokeza kwa baadhi ya wagombea ni makovu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hasa kwa kundi kubwa lilionekana kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Wale ambao walionekana kumuunga mkono kiongozi huyo na hawajawahi kuonekana kumtusi baada ya jina lake kuenguliwa ndani ya chama hicho na kuhamia Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), bado wanatazamwa chongo na baadhi ya wenzao hasa wenye maamuzi kwa propaganda kuwa hawana mapenzi mema na CCM.

Hisia hizo zinatanabaishwa kuwa zitawaumiza wengi watakapojitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya CCM mwaka huu. Safu hii inaanzia katika mkoa wa Mbeya ambako kwa sasa nafasi ya uenyekiti inashikiliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi.

Chama hicho kimepiga marufuku kuanza kampeni mapema (kampeni ambazo si rasmi) sambamba na michezo iliyozoeleka katika siasa ya ukarimu (rushwa).

Ngazi hiyo ya uenyekiti ni ngazi kubwa na ya heshima hivyo baadhi ya makada wameanza kutajwa kuwa wanafaa kuwa katika nafasi hiyo katika mkoa wa Mbeya na tayari safu hii imeanza kudokezwa majina yao na hapa yanawekwa bayana.

Baadhi ya majina hayo ni pamoja na jina la mwanasiasa mkongwe mkoani Mbeya, Allan Mwaigaga maarufu kama Mwaji Group ambaye ni mfanyabiashara na anamiliki mabasi ya Ndenjela.

Kiongozi huyu amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini na amewahi kuwania mara kadhaa nafasi ya ubunge katika michakato ya ndani ya chama hicho ndani ya jimbo la Mbeya Mjini na hata Mbeya Vijijini lakini kura hazikutosha.

Anatajwa kuwa ni kiongozi ambaye anao ushawishi wa kisiasa na hasa anapodhamiria jambo fulani huwa anashupalia na kufika nalo mwisho.

Kwa sasa katika jimbo la Mbeya Mjini ambalo linaongozwa na Mbunge, Joseph Mbilinyi (Chadema), ndilo linalomuumiza kila mwanachama mtiifu wa CCM baada ya wananchi kuwaamini wagombea wengi wa Chadema kuanzia ngazi ya udiwani na ubunge na mpaka sasa halmashauri hiyo inaongozwa na Mstahiki Meya kutoka Chadema.

Hivyo chama hicho kinaendelea kujipanga katika safu zake za uongozi ili kupata viongozi ambao wanaweza kusaidia kuwarejeshea imani wapigakura wa jimbo hilo na majimbo mengine ambako madiwani wa vyama vya

upinzani hasa Chadema wakizidi kuongezeka kila uchaguzi mkuu unapoitishwa.

Zambi alifanya kosa la kiufundi mwaka 2015 ambapo akiwa kamakamanda mkuu wa (vita), akaacha majimbo na kwenda kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mbozi ambako nako alipoteza nafasi hiyo kabla hajaukwaa Ukuu wa Mkoa alionao sasa.

Mbali na Mwaigaga, viongozi wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rungwe ambaye pia ni mmiliki wa mabasi yaliyoandikwa Rungwe Express. Kiongozi huyo ni Kamanda wa Jumuiya ya vijana wa CCM Mkoa wa Mbeya (UVCCM). Anatajwa kuwa ni mmoja wa viongozi ambao wanao upendo mkubwa sana kwa wanachama wa chama hicho bila kujali rika au uwezo wa kifedha na ni mtu wa msaada kwa chama na mtu mmoja mmoja.

Taarifa zinasema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisaidiakukitafutia kura chama hicho kila jimbo la Mkoa wa Mbeya na Songwe na kuwasaidia kifedha baadhi ya wagombea wa CCM ingawa bado haijathibitika kuwa aliwasaidia kiasi gani kila mmoja pamoja na baadhi ya madiwani wa kata za jimbo la Mbeya Mjini.

Kwa upande wa vijana wengi, huyu amekuwa akitajwa kuwa kipenzi chao ingawa wengi wao si wapiga kura katika mkutano mkuu wa chama hicho ngazi ya Mkoa.

Mwingine anayetajwa ni Kachero mbobezi ambaye ni mstaafu wa idara ya usalama wa Taifa, Salmin Said ambaye katika siasa za Mkoa wa Mbeya anazielewa vema na kipenzi cha wanasiasa wa pande zote.

Kiongozi huyu pamoja na weledi wake inaelezwa kuwa kinaweza kumpata kilichowahi kumpata aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Robert Mboma, alipowania nafasi ya Ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini akaukosa kwa sababu ya wapiga kura kuwa na hofu ya kuongozwa kwa amri za kijeshi.

Lakini yaweza kuwa tofauti kwa kiongozi huyu ambaye ni mkazi wa Iwambi katika Jimbo la Mbeya Mjini. Aliyewahi kuwa diwani wa Kata ya Utengule Usongwe Jimbo la Mbeya Vijijini kwa miaka 15 Mwalimu Jacob Mwakasole pia ni mmoja wa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Kiongozi huyu ni mcheshi na aliwahi kuwa katika kampeni za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri kuu Taifa kwa upande wa Prof. Mark Mwandosya dhidi ya mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda, Tom Mwang’onda ambapo Prof. Mwandosya aliibuka mshindi.

Hawa ni baadhi tu ya wanaotajwa, wiki ijayo tutaona mahojiano ya mmoja baada ya mwingine wakizungumzia kutajwa kwao katika nafasi hiyo na mitazamo yao mwaka 2015 kuwa nani alikuwa anamuunga mkono mgombea gani wa nafasi ya urais.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440 749 na Barua pepe ambayo ni kalulunga2006@gmail.com