Home Makala KOREA KASKAZINI NA MAREKANI INACHOKOZWA VITA YA TATU

KOREA KASKAZINI NA MAREKANI INACHOKOZWA VITA YA TATU

5579
0
SHARE

NA LUQMAN MALOTO


Mgogoro wa Kinyuklia kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini una uchokozi mkubwa kuliko unavyoonekana.

Suala siyo silaha za nyuklia, bali nani mwenye nazo na washirika wake ni akina nani?
Tafsiri ya juu katika mtazamo wa Marekani dhidi ya Korea Kaskazini na umiliki wake wa silaha za nyuklia ni utawala wa dunia, yaani Hegemony.

Marekani inataka kuwa baba wa mataifa yote duniani.
Hegemony ni nadharia ya dola moja kuongoza nyingine kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Taifa moja linakuwa kiranja wa mataifa mengine duniani.
China, Urusi na Marekani ndiyo wanaopambana sasa hivi kujisimika ukuu wa Hegemony. Kila mmoja anataka awe kiranja wa dunia kiuchumi, kisiasa na kijeshi.
Katika mchuano huo, kila taifa lina washirika wake. Nchi hizo tatu, kila moja hutaka iungwe mkono zaidi duniani ili itawanye mabavu yake. Hapohapo, kati ya nchi hizo, kila moja hujua mataifa madogo yenye kupingana nayo.
Ni hapo unaikuta Korea Kaskazini kama adui wa Marekani lakini mshirika wa China na Urusi. Ni hapo unaiona Marekani ikiingiwa na kiwewe, maana uimara wa Korea Kaskazini kinyuklia ni pigo kwake.
Hivyo basi, matakwa ya Marekani kwa Korea Kaskazini kusitisha mipango yake ya silaha za nyuklia, hayaishii tu kwamba ni kwa usalama wa dunia, bali kwa sura pana kuwa ukuu wake kama taifa baba duniani, utakuwa kwenye wasiwasi.

 

KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

Mpaka nusu ya kwanza ya Karne ya 19 ilipokuwa inaelekea kukamilika, Korea ilikuwa moja. Nchi hiyo iligawanywa mara mbili na Marekani pamoja na Urusi kupitia iliyokuwa dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR).
Kuanzia mwaka 1910 mpaka nyakati za mwisho za kukamilika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Korea ilikuwa imekaliwa na Japan. Baada ya Japan kuwa mahututi kutokana na athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Marekani na Urusi waliamua kuikomboa Korea.
Japan ilikuwa imetoka kupigwa maeneo mengi iliyokuwa imeyashikilia, vilevile ilikuwa inaugulia maumivu ya shambulio la nyuklia, iliyopigwa na Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki, kisha athari yake kusambaa kwenye maeneo mengi wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Hata mpaka wa kuigawa Korea katika pande mbili ni makubaliano ya Urusi na Marekani. Walichora mpaka, wakauita 38th Parallel kisha Urusi ikaipiga Japan upande wa Kaskazini na kuikamata Korea Kaskazini, halafu Marekani ikaiondosha Japan Kusini, hivyo kuishika Korea Kusini.
Kwa ukombozi huo, Urusi iliijaza upepo dola ya Korea Kaskazini kujitangaza kuwa yenyewe ndiyo Serikali ya Korea yote. Marekani nayo, ilishawishi Korea Kusini kupitia mamlaka zake, kujitambulisha kuwa dola ya jumla katika Korea nzima.
Athari za Urusi na Marekani zilionekana kupitia mifumo yake ya kiuchumi. Urusi kwa sababu ni Wajamaa, waliiambukiza Korea Kaskazini mfumo wa Ujamaa. Marekani na Ubepari wao, waliigeuza Korea Kusini kuwa nchi ya kibepari.
Hivyo basi, Korea Kaskazini tangu kuasisiwa kwake na kutambulika rasmi kama dola ya Jamhuri ya Watu wa Kidemokrasia wa Korea (DPRK), haiivi na Marekani. Viongozi wake wamekuwa jeuri kweli dhidi ya Marekani.
Siku zote, imani ya Marekani ni kuwa Korea Kaskazini inakumbatiwa na Urusi pamoja na China, mataifa ambayo ni mahasimu wake katika safari ya tamaa ya kuitawala dunia kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kijeshi.
Ni kama ambavyo Korea Kaskazini, China na Urusi, huamini kuwa Marekani inaipa Korea Kusini nguvu za kiuchumi na kiteknolojia ili istawi zaidi ya Korea Kaskazini, kisha huo uwe mfano dhahiri wa kushindwa kwa China na Urusi.

 

VITA YA KOREA

Chokochoko za Marekani, Urusi na China ni sababu ya Vita ya Korea kuanzia mwaka 1950 mpaka 1953. Korea Kusini ilishawishiwa kujitangaza kuwa Serikali ya Korea nzima, vilevile Korea Kaskazini ilitakiwa kujitangaza kuwa mtawala wa dola nzima ya Korea.
Mwanzo wa Vita ya Korea ni Marekani kuitangaza Korea Kaskazini kuwa iliivamia Korea Kusini, hivyo mapambano yalianza. Awali ilionekana kama Marekani isingetumia msuli mkubwa kuikabili Korea Kaskazini.
Hata hivyo, Marekani ikiwa imeweka kambi ya vita ambayo hufahamika kama Chosin Reservoir Campaign, Novemba 27, 1950, ilishambuliwa kwa kushtukizwa na China, hivyo mapigano makali yalitokea.
China iliamua kuishambulia Marekani ili kuudhoofisha mpango wake wa kuipiga Korea Kaskazini. Mapambano hayo ambayo yalidumu kwa siku 16 kati ya China na Marekani, huitwa Battle of Chosin Reservoir. Yalianza Novemba 27 mpaka Desemba 13, 1950.
Battle of Chosin Reservoir shabaha kuu ilikuwa ni China kuimaliza nguvu Marekani mapema, lakini baadaye vikosi vya Umoja wa Mataifa, Uingereza na Korea Kusini, waliungana na Marekani kuikabili China.
Kuanzia hapo moto ukawaka jumla katika Vita ya Korea, kufikia wakati huo ikawa ni Korea Kaskazini dhidi ya Korea Kusini. Vikosi vya Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza, Canada na mataifa mengine washirika walikuwa upande wa Korea Kusini.
Upande wa Korea Kaskazini kulikuwa na China, Urusi (USSR), Ujerumani Mashariki, Bulgaria, Jamhuri ya Czech na mataifa mengine ambayo ni washirika wa mfumo wa kiuchumi wa kijamaa.
Mwisho kabisa, utaona kuwa tafsiri ya Vita ya Korea ni uhasimu wa kihistoria kati ya Ujamaa dhidi ya Ubepari. Korea Kaskazini na Korea Kusini ni nchi ndogo lakini ziligonganisha wababe wa dunia kwa sababu za kimaslahi kati ya Ujamaa na Ubepari.

 

SILAHA ZA NYUKLIA

Vurugu zote za Korea Kaskazini na umiliki wa silaha za maangamizi, zilianza mwaka 1962, wakati walipoanzisha mchakato wa kumiliki zana za maangamizi ambao wenyewe waliuita all-fortressization.
Mwaka 1963, Korea Kaskazini iliiomba Urusi iisaidie jinsi ya kuwa na silaha za nyuklia. Hata hivyo, Urusi ilipingana na wazo hilo la silaha, lakini ikawa tayari kuiwezesha nchi hiyo kuwa na mpango wa amani wa nishati ya nyuklia.
Urusi ikiwa chini ya USSR, iliisaidia Korea Kaskazini kwa kusomesha wanasayansi wa nyuklia, vilevile iliwezesha kuanzishwa kwa kituo kikuu cha utafiti wa sayansi ya nyuklia cha Yongbyon, ambacho ndiyo kimekuwa roho ya nyuklia ya Korea Kaskazini.
Mwaka 1964, baada ya China kufanya jaribio lake la kwanza la nyuklia kwa mafanikio, Korea Kaskazini iliiomba China iwasaidie jinsi ya kukuza sayansi yao ili kufikia hatua ya kumiliki silaha za nyuklia lakini Serikali ya China ilikataa.
Unaweza kuona kuwa Urusi na China pamoja na kuwa washirika wa Korea Kaskazini lakini hawajawahi kuiamini kuhusu kumiliki silaha za nyuklia ndiyo maana zilikataa maombi hayo.
Ulipofika mwaka 1965, kituo cha nyuklia cha Yongbyon kilianza kazi rasmi na baada ya kupata mafanikio, mwaka 1979, Korea Kaskazini walitengeneza kituo cha pili cha Yongbyon.
Baada ya Korea Kaskazini kuwa na utaalamu wa kutosha wa sayansi ya nishati ya nyuklia kwa msaada wa Urusi, mwaka 1980, Korea Kaskazini kwa kutumia kemikali za uranium, walianza kujitengenezea silaha za nyuklia.
Mwaka 1985, baada ya Korea Kaskazini kubanwa, ilikubali kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Silaha za Nyuklia (Non-Proliferation Treaty, NPT), lakini haikukamilisha baadhi ya vipengele.
Ripoti ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati za Atomia (IAEA) mwaka 1993, ilieleza kuwa Korea Kaskazini, ilikataa kukaguliwa ili kuthibitisha kama kweli ilikuwa imeachana na utengenezaji wa silaha za nyuklia. Baada ya hapo, Korea Kaskazini ilijiondoa kwenye mkataba wa NPT.
Kupitia makubaliano ya mwaka 1994, Marekani iliiahidi Korea Kaskazini kuachana silaha za nyuklia, badala yake ingeipa mitambo miwili ya kutumia maji yenye kuipa uhai nishati ya nyuklia (light water reactors). Marekani iliamini Korea Kaskazini ingekubali ofa hiyo kubwa ili kupata unafuu wa kutunza nishati yao ya nyuklia.
Hata hivyo, kila baada ya mazungumzo kati ya Korea Kaskazini na Marekani, viongozi wa Korea Kaskazini huzungumza na Urusi pamoja na China, kisha kujadiliana kuhusu mapendekezo ya Marekani na shinikizo lake la kuzuia silaha za nyuklia.
Marekani na Korea Kaskazini wamekuwa wakishtumiana mara kwa mara. Silaha za nyuklia ni sehemu moja lakini sababu zipo nyingi. Marekani inaamini kuwa Korea Kaskazini hupewa kiburi na China pamoja na Urusi ili kuivimbia.
Oktoba 9, 2006, Korea Kaskazini walifanya jaribio lao la kwanza la silaha za nyuklia kwa mafanikio makubwa. Kuanzia hapo, Korea Kaskazini iliwekewa vikwazo vya kiuchumi na Umoja wa Mataifa.
Januari 6, 2007, Korea Kaskazini ilijitangaza rasmi kuwa taifa lenye silaha za nyuklia.

Hali hiyo ilizidi kujaza wasiwasi mkubwa duniani, hivyo kuifanya Marekani kujiona kama nchi iliyoshindwa kuidhibiti Korea Kaskazini.
Mpaka kufikia Septemba 9, 2016, Korea Kaskazini ilifanikisha majaribio matano, kisha likajitangaza kuwa taifa lenye nguvu za kutosha kwa silaha za nyuklia, vilevile teknolojia ya nyuklia kwa jumla.

ITAENDELEA WIKI IJAYO