Home Makala KOREA KASKAZINI NA MAREKANI ZINACHOKOZA VITA YA TATU YA DUNIA

KOREA KASKAZINI NA MAREKANI ZINACHOKOZA VITA YA TATU YA DUNIA

1951
0
SHARE

NA LUQMAN MALOTO


Mgogoro wa Kinyuklia kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini una uchokozi mkubwa kuliko unavyoonekana. Suala siyo silaha za nyuklia, bali nani mwenye nazo na washirika wake ni akina nani?

VITA 2017

Wakati huu wasiwasi ukiwa ni mkubwa kwamba Korea Kaskazini zitapigana wakati wowote, vema ifahamike kuwa mgogoro ni lilelile suala la silaha za nyuklia.

Machi 6, 2017, Korea Kaskazini ilizindua makombora manne ya masafa marefu na kuyatega kuelekea Bahari ya Japan. Uzinduzi wa makombora hayo ulilaumiwa mno na Marekani pamoja na Korea Kusini.

Uzinduzi huo, ulijenga picha kubwa kwamba Korea Kaskazini imekaa kishari muda wote na kwamba hata maonesho ya makombora hayo ilikuwa ni alama kwamba ipo tayari kwa vita wakati wowote. Mpaka wakati huo tayari Korea Kaskazini ilikuwa imeshapokea vitisho kutoka kwa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson aliziomba nchi za Japan, Korea Kusini na China, kushirikiana na Marekani katika kutafuta mwafaka wa kidiplomasia katika mgogoro wa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini pasipo kumwaga damu.

Aprili 15, 2017, wakati wa Sikukuu ya Sun ambayo ni siku ya maadhimisho kitaifa Korea Kaskazini ya kuzaliwa mwasisi wa nchi hiyo, Kim II-sung ambaye ni babu wa kiongozi wa sasa taifa hilo, Kim Jong-un, nchi hiyo ilitangaza kuzindua bomu lingine la masafa marefu.

Aprili 16, 2017, Korea Kaskazini ilipanga kuzindua bomu la hydrogen na kabla yake, ilizindua roketi zenye kuwezesha uzinduzi wa bomu hilo hatari la masafa marefu lakini uzinduzi huo haukufanikiwa baada ya kutokea hitilafu za kiufundi.

Hata hvyo, inaaminika kuwa kutofanikiwa kuzinduliwa kwa bomu la hydrogen ambako kunaelezwa na Korea Kaskazini kuwa ni hitilafu za kiufundi, inadaiwa ilikuwa kuwazuga Wamarekani, kwani tayari bomu hilo lipo tayari kwa kazi pamoja na makombora mengine ya nyuklia.

Rais wa Marekani, Donald Trump, alitoa tangazo kuwa Serikali ya Korea Kaskazini inaongozwa na magaidi, kwa hiyo wataipiga ili kutatua tatizo la ugaidi huo.

Hiyo ndiyo sababu ya vikosi vya Marekani kuisogelea Korea Kaskazini, vikiwa tayari kwa mashambulizi dhidi ya nchi hiyo kama Rais Trump alivyotangaza.

Uamuzi wa Marekani kuikabili Korea Kaskazini unaitwa na Trump kuwa ni kutafuta ufumbuzi wa silaha za nyuklia, vilevile kuondosha utawala wa kigaidi. Korea Kaskazini imesema kuwa ipo tayari kwa mapambano.

TATIZO NI WATAWALA

Kwa nini hali imefikia kuwa tete katika Peninsula ya Korea Kaskazini kiasi cha kuwepo matarajio kuwa wakati wowote moto utawaka? Kimsingi hakuna tatizo kubwa kama kuwepo kwa watawala wenye kiburi.

Hulka za viongozi waliopo madarakani hivi sasa Marekani na Korea Kaskazini, ni sababu ya vita kuonekana ndiyo suluhu badala ya mazungumzo. Marekani yupo Trump, Korea Kaskazini wanaye Jong-un. Wote jeuri.

Wakati Korea ya Kaskazini ikiongozwa na baba yake Jong-un, Kim Jong-il, zipo nyakati ilitokea mivutano. Marekani iliishutumu Korea Kaskazini kwa kuingilia shehena zake za mafuta. Marekani ilipolalamika tu, Jong-il aliomba radhi kwa ajili ya nchi yake.

Hata hivyo, tangu Jong-un aingie madarakani mwaka 2012, hali imebadilika kabisa. Kabla yake, Korea Kaskazini ilikuwa inachukua tahadhari pale ilipokuwa ikipewa shinikizo la kuachana na silaha za nyuklia, hata hivyo kwa sasa ni tofauti.

Jong-un ukimtisha ndiyo unamwongezea kiburi. Mwaka 2013 wakati alipotoa tamko lake la kwanza kuhusu silaha za nyuklia, Jong-un alisema, Korea Kaskazini haiwezi kuachana na silaha za nyuklia kwa sababu haitapiga bila kuchokozwa.

Mwaka 2012 kabla ya kifo cha Jong-il, Korea Kaskazini ilitangaza kuachana na silaha za nyuklia, hivyo Marekani ikaanza kuipa misaada. Jong-il alipokufa na kuingia Jong-un mambo ya maelewano yamekuwa magumu. Jong-un aliingia na sera kuwa silaha za nyuklia ziendelezwe iwe isiwe.

Jong-un anapokutana na Trump ambaye ana kiburi binafsi cha mafanikio ya kimaisha, jumlisha kile kwamba anaongoza taifa kubwa lenye nguvu zaidi ulimwenguni, ndiyo maana hali inakuwa katika sura kuwa vita ya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini haikwepeki.

Urusi wanaamini kuwa Trump na Jong-un wote wana matatizo ya kiburi lakini wanasema Trump ni tatizo kubwa zaidi. Wanamkosoa kwa kukosa busara na uvumilivu katika kushughulikia matatizo ya kimataifa.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa wa Urusi, Dmitry Kiselyov ambaye ni swahiba wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, anasema kuwa tatizo kubwa linalozifanya Marekani na Korea Kaskazini kuingia vitani ni kuwa na viongozi wenye uwezo mdogo wa kuchanganua siasa za kimataifa.

Upande wa pili, Urusi inapata pigo kwa sababu walicheza karata nyingi kuhakikisha Trump anashinda Urais Marekani kwa imani kuwa sera zake zingeweza kuidhoofisha Marekani kimataifa lakini kwa Korea Kaskazini ni kama bomu linairudia.

Uamuzi wa Trump kuivamia Korea Kaskazini ndiyo hasa Urusi inataka lakini inakuwa bahati mbaya kwamba anayevamiwa ni ‘mtoto wake’, vilevile jirani yake, hivyo hakuna namna Korea Kaskazini inaweza kupigwa bila Urusi kuathirika.

Urusi kama ilivyo kwa China, wanatamani kuona Marekani inatekeleza matumizi mabaya ya nguvu na rasilimali zake maeneo ya mbali ili zenyewe ziwe zinatoa misaada ya chinichini, kwa imani kuwa mwisho Marekani itayumba kiuchumi na kisiasa.

Rais 44 wa Marekani, Barack Obama, alifanikisha mazungumzo ya kidiplomasia ya kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo, Trump kwa hulka yake, anaona njia aliyotumia Obama ni udhaifu, kwamba kiongozi wa nchi kubwa kama Marekani lazima uogopwe.

DAUD NA GOLIATH

Korea Kaskazini ni nchi ndogo. Ukubwa wake ni kilometa za mraba 120,540. Ina watu wanaokisiwa kufika 25 milioni. Pato lake la taifa (GDP) kwa mwaka ni dola 40 bilioni, yaani Sh89 trilioni. Pato la mtu mmoja (GDP per capita) ni dola 1,800 ambazo ni Sh4 milioni.

Korea Kaskazini inazidiwa eneo kwa karibu mara nane na Tanzania ambayo eneo lake ni kilometa za mraba 947,303. Tanzania GDP ni dola 150 bilioni, Sh337 trilioni na GDP per capita ni dola 3,097 ambazo ni Sh6.7 milioni.

Pamoja na udogo huo wa eneo na kipato lakini Korea Kaskazini ina jeshi kubwa. Inakadiriwa kuwa askari 1.2 milioni. Kwa idadi hiyo, maana yake inazidiwa na Marekani pamoja na China peke yake. Hivyo, hata Urusi inazidiwa idadi ya askari na Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini inapitia vipindi vigumu kiuchumi, inazidiwa mbali na Korea Kusini. Sababu ni kwamba Korea Kaskazini muda wote inawaza kujilinda na hutumia robo nzima ya GDP kila mwaka kwa ajili ya bajeti ya ulinzi. Ndiyo maana inaweza kumiliki nyuklia wakati ni taifa maskini. Upande wa pili, inaathiriwa na vikwazo wa kiuchumi ambavyo inaishi navyo tangu mwaka 2006.

GDP ya Korea Kaskazini ni Sh89 trilioni, kwa hesabu kuwa hutumia robo yake kwa ajili ya ulinzi hata nje ya bajeti zao, maana yake kiasi cha juu cha matumizi ya jeshi la Korea Kaskazini ni Sh22 trilioni.

Mwaka jana, Jeshi la Marekani lilitumia dola 590 bilioni, Sh1,322 trilioni. Fedha hizo ni ndani ya bajeti. Si kama Korea Kaskazini ambao hutumia fedha zao kwa ajili ya jeshi nje ya bajeti.

Hesabu hiyo, inakupa jawabu kuwa matumizi ya Jeshi la Marekani kwa mwaka mmoja, yanatosha kuhudumia vikosi vyote vya ulinzi vya Korea Kaskazini na ununuzi wa silaha kwa miaka 60.

Kwa mantiki hiyo, vita ya Korea Kaskazini dhidi ya Marekani ni sawa na simulizi ya Biblia kati ya mtoto mdogo Daud na Goliath ambaye ni jitu kubwa lenye rekodi ya kushinda mapigano mengi ya kivita.

Daud na utoto wake, alimpiga Goliath kwa sababu alipewa uwezo maalum na Mungu. Ni kama ambavyo Korea Kaskazini ikiipiga Marekani, itakuwa hadithi sawa na Daud, kwamba Korea Kaskazini itakuwa imepewa nguvu maalum na Mungu ili kuipiga Marekani (Goliath).

Ni kweli Korea Kaskazini kwa silaha ilizonazo inaweza kuua watu wengi lakini si kuipiga Marekani. Hiyo ni habari nyingine ambayo kwa ulimwengu wa kawaida haiwezi kutokea. Nasisitiza; labda Korea wapewe nguvu maalum na Mungu.

VITA KUU YA TATU?

Uchokozi huu unaweza kuipeleka dunia kwenye Vita Kuu ya Tatu ya Dunia. Marekani inafahamu kuwa kiburi cha Korea ya Kaskazini kipo kwenye mwavuli wa China na Urusi.

China ndiyo ambayo inaweweseka zaidi, wakati Marekani na Korea Kaskazini wakitambiana. China ni jirani na Korea Kaskazini, vilevile yenyewe ndiye mfadhili mkuu wa nchi hiyo, hivyo hakuna namna yoyote ya Korea Kaskazini kushambuliwa bila China kuathirika.

Suala la wakimbizi kutoka Korea Kaskazini kukimbilia China litatokea endapo mapigano yataanza. Hivyo, China itajikuta kwenye misukosuko ya wakimbizi na kupigania usalama hasa Kaskazini-Mashariki ambako inapakana na Korea Kaskazini.

Vipi China ikiifanya Marekani kama wakati wa Vita ya Korea kwa kuishambulia kwa kushtukiza kama ilivyotokea katika Battle of Chosin Reservoir mwaka 1950? Marekani bila shaka itajibu kisha vita itatanuka.

China ikishaingia vitani lazima na Urusi itaingia, hapohapo Uingereza haiwezi kuacha swahiba wake anachangiwa, lazima ataingia. Huo ni mtazamo mdogo tu ikiwa China itafanya jaribio la kuisaidia Korea Kaskazini dhidi ya Marekani.

China haitaki vita na imekuwa ikionya mapigano kwamba hayatasaidia. Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ameonya kuwa kati ya Marekani na Korea Kaskazini, hakuna nchi ambayo itakuwa salama.

Wang anaamini upo mlango wa mazungumzo, hivyo ametaka Korea Kaskazini na Marekani wasikimbilie kwenye mapigano. Wakati huohuo ameonya kuwa endapo China itachokozwa hawatasita kujilinda.

Je, Korea Kaskazini wakizidiwa na kuamua kupiga hovyo makombora yao ya sumu? Ni hapo kwenye wasiwasi kwamba madhara ya kuivamia Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia ni makubwa mno kwa ulimwengu.

Hata hivyo, Marekani wanatamba kuwa wanazo zana za kutosha kudhibiti nyuklia za Korea Kaskazini zisisababishe madhara makubwa.

Baada ya Jong-un, anayefuatia kwa cheo Korea Kaskazini ni Choe Ryong, aliyesema kuwa hali imekuwa ya vita kwa sababu ya matamshi ya Trump.

“Tutajibu vita kwa vita na vita ya nyuklia kwa mtindo wetu wa mashambulizi ya kinyuklia,” alisema Ryong kuthibitisha kuwa nchi yao tayari ipo tayari kwa vita.

Kila mwenye kuwaza vizuri, lazima ataomba Korea Kaskazini na Marekani wasipigane. Hofu ya uongozi wa Jong-un ipo kwenye mwisho mbaya wa Saddam Hussein wa Iraq na Muammar Gaddafi wa Libya, kwamba Marekani wakimkamata wanaweza kumfanya vibaya.

Ni hofu hiyo ambayo inasababisha uwezekano wa Korea Kaskazini kuachia nyuklia uwe mkubwa, kwamba damu nyingi imwagike kuliko kukaribia kifo cha aibu kama cha Gaddafi na Saddam huku akijiona.