Home Makala KUFA KWA AZIMIO LA ARUSHA CHANZO CHA KUZALISHA WAKOLONI WAZAWA

KUFA KWA AZIMIO LA ARUSHA CHANZO CHA KUZALISHA WAKOLONI WAZAWA

1173
0
SHARE

NA MOSES NTANDU


Pongezi nyingi zinazoendelea kutolewa na Jumuiya mbalimbali kwa Rais John Magufuli kutokana na jitihada zake za kuusafisha mfumo wa uongozi nchini, hazitoshi kuonesha kumuunga mkono pekee, bali jamii yote ya Watanzania inapaswa kurudi kwenye misingi ya uzalendo.

Watanzania tunapaswa kujitambua, pia kuwa na mapenzi na Taifa bila kujali tofauti za kisiasa ambazo kwa kiwango kikubwa zinaendendelea kuathiri umoja wetu wa kitaifa. Kwa sababu lengo la kuanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 ilikuwa ni kuimarisha demokrasia, lakini sasa lengo hilo linaanza kuyoyoma taratibu.

Matukio mengi makubwa yasiyo ya kizalendo yanayofanyika nchini yanaendelea kuvuruga utulivu tulionao, kumong’onyoa maadili na kusambaratisha uchumi wa Taifa, lakini jamii inatazama na kukaa kimya.

Suala la uzalendo lilianza kupewa kisogo  tangu msingi wake ulipoanza kuvurugwa katika shule za msingi na sekondari ambapo masomo ya uzalendo na itikadi ya Taifa yalikuwa yanafundishwa lakini sasa yameondolewa.

Kosa kubwa tulilolifanya ni kuuza silaha zetu tukiamini tumekwishamaliza vita wakati tulikuwa bado tupo vitani na sehemu iliyosalia ilihitaji umakini mkubwa zaidi ili kumaliza vita.

Tunaona kuwa katika harakati za ukombozi wa kupigania uhuru, viongozi waasisi wa Taifa hili walifanya kazi kubwa  ambayo iliambatana na kulinda na kudhibiti rasilimali za nchi kwa kuweka miiko na miongozo kadhaa iliyothibiti wale waliokuwa na uchu wa kupora rasilimali za umma.

Miiko na miongozo hiyo ndiyo ilikuwa silaha kubwa kwa Taifa katika vita vya kiuchumi na kimkakati ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanafaidi rasilimali za nchi yao. Moja ya silaha hizo zilikuwa ni Azimio la Arusha, mitaala bora ya ufundishaji katika shule zetu toka shule za msingi hadi vyuo vikuu, hii iliimarisha Sera ya Taifa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Tukiwa tunaendelea na safari yetu ya maendeleo, baadhi ya viongozi wetu kwa bahati mbaya au makusudi walishawishi tuachane na miiko na miongozo hiyo ambayo ilikuwa silaha kubwa katika kudhibiti na kujilinda na wakoloni wapya.

Baada ya kulizika Azimio la Arusha, tulianza kudhohofika taratibu bila kujitambua, huku wakoloni wapya wakiibuka miongoni mwetu na kujipenyeza katika kila sekta kwa vazi la Utanzania na uzalendo  wakati hawakuwa wenzetu.

Nakumbuka tukiwa wadogo tulisoma vitabu vya historia na siasa ambavyo vilitufundisha kwa kiwango kikubwa  tumetoka wapi na wazee wetu walifanya nini kutupigania, tulikuwa na uchungu na nchi yetu kwa kuwa tulifundishwa kuwa kuna ndugu zetu walipoteza maisha kwa ajili ya Taifa letu.

Tulijifunza pia mababu zetu walivyonyanyaswa na wakoloni. Wakati mwingine tulioneshwa mababu zetu walivyokuwa wakiwabeba wakoloni kwenye viti, unakuta mkoloni huyo yuko peke yake huku akiwa na bunduki ya gobore, tulisikitika sana na kuwalaumu wazee wetu kuwa walikuwa wajinga kwamba wananyanyaswa na wakoloni wakati wana uwezo wa kukabiliana nao, kwanini wanaogopa gobore?

Kwa kweli ni bora wazee wetu waliogopa gobore na kuwabeba wakoloni kwenye viti, lakini hawakupora na kuharibu rasilimali zetu kama kile kilichokuja kufanywa baadaye na baadhi ya Watanzania walioelimika zaidi kuliko wale mababu zetu.

Pamoja na kosa tulilolifanya la kutelekeza silaha yetu ya Azimio la Arusha, pia bado tumetelekeza somo la itikadi na kuviachia vyama vya siasa ambavyo navyo vingi vilikuja na itikadi zao ambazo kimsingi hazikidhi mahitaji na masilahi ya Taifa.

Itikadi ambayo ilifundishwa na TANU na baadaye CCM ilifundishwa kipindi kile tukiitwa chipukizi wa chama kupitia shule za msingi kwa kufundishwa mashuleni katika masomo ya siasa na historia ambayo masomo yalituimarisha kujitambua na kujua umuhimu wa rasilimali za nchi na utaifa wetu. Je, leo hii watoto wanafundishwa nini juu ya itikadi huko mashuleni kuanzia shule za misingi na sekondari?

Kutokana na mfumo tulionao wa vyama vingi, kila chama kina itikadi yake na mfumo wake wa kuandaa vijana wake hii kwa namna moja au nyingine inatugawa kwa kuwa kila mmoja anakuwa na imani yake badala ya kufuata imani na itikadi moja ya Taifa.

Ni vyema sasa vyombo vinavyohusika kuja na mfumo mmoja utakaotuunganisha Watanzania wote na kuachana na itikadi na imani za vyama vya siasa, badala yake tufuate itikadi moja ya Taifa na ijengwe vyema kutoka shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.

Vijana waliozaliwa kuanzia mwaka 1992, wana miaka 25 sasa wanaelewa nini kuhusu uzalendo na itikadi ya Taifa letu? Ikiwa hawafungamani na chama chochote cha siasa ama wapo katika vyama tofauti vya siasa, bado hawatakuwa na msimamo. Vyama vyetu vya siasa havifuati mfumo uliowekwa na waasisi wetu kwa mfumo wa kiutawala wao, huiga mifumo ya kimagharibi ambayo mingi ni ya kibepari.

Pia vyama tulivyonavyo vinapingana kisera hadi kiitikadi, jambo ambalo ni kosa kubwa maana itikadi ndiyo misingi ya Taifa, maana inalenga kuwajenga vijana kiimani na kulinda rasilimali za Taifa lao. Ni bora tupingane katika sera lakini suala la itikadi na miiko ya Taifa liwe jambo la kitaifa ili kuimarisha uzalendo na umoja wa kitaifa.

Tanzania ijayo baada ya miaka 20 ama 50 itakuwaje ikiwa misingi ya itikadi ya Taifa inazidi kumomonyoka kila kukicha? Idadi ya makundi inazidi kujigawa kupitia vyama vya siasa. Siasa katika Taifa hili imekuwa ni vita watu hadi wanatoana uhai kisa ni masuala ya siasa, mbona hao waliotuletea mfumo huu wanaishi kwa amani na utulivu.

Udhaifu huu umetusababishia kuzalisha Taifa la vijana wavivu wasiopenda kufanya kazi, kwa kweli inaumiza sana ukizunguka mitaani unakuta magenge ya vijana wakicheza kamari kwa lengo la kutafuta pesa nyingi kwa njia za mkato.

Vijana wengi wanaocheza kamari wanaita ‘mikeka’, kundi kubwa ni la vijana wa kati ya miaka 18 – 35. Je, vijana hawa wanahamasishwa muda gani kufanya kazi na kuachana na imani za kutegemea kupata pesa nyingi kwa urahisi bila kufanya kazi.

Pamoja na jitihada kubwa zinazoendelea za ukombozi wa Taifa kutoka kwa wakoloni wapya wa kiuchumi, basi tuunge mkono jitihada za rais kwa kujisahihisha na kudhibiti mmomonyoko huu wa maadili ili vijana wawe na mwamko wa kufanya kazi badala ya kutegemea pesa kirahisi ambazo huwapeleka katika vitendo viovu.

Kwa mujibu wa mamlaka husika, hadi kufikia mwaka Agosti mwaka 2016, kulikuwa na vituo 2684 vya kuchezesha kamari maarufu kama ‘kubeti’, jambo linaloashiria kuwa hadi sasa kutakuwa na zaidi ya vituo 3000 vya michezo hiyo.

Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, katika uwasilishaji wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2017/18, alisema Serikali imeamua kukusanya mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha (Kamari), hii inamaanisha kuna namna ya kukubali na kuruhusu michezo hiyo kuendelea kushamiri, hili ni kosa.

“Serikali imeona kuna uwezekano wa kuweza kupata mapato kwenye michezo ya kubahatisha, hivyo kuanzia Julai mosi mwaka huu, mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha yatakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema Waziri Dk. Mpango.

Tunapaswa kutazama madhara yatokanayo na michezo ili kulinusuru Taifa kwa mustakabali wa baadaye tujisahihishe.

Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia njema ya kulikomboa Taifa kutoka kwa wakoloni wapya walioibuka, baada ya taifa kuachia silaha yake ya Azimio la Arusha na masuala ya itikadi. Kutokana na nia hii njema, Serikali inapaswa kuandaa silaha mpya za kisasa yenye uwezo mkubwa ili kuzibiti wakoloni hawa wapya kwani tuna wakoloni wazawa na wageni zaidi kuliko walowezi ambao wamejikita na wanakuja kila siku na mbimu mpya ikiwemo hizi za kamari na umomonyoaji wa maadili katika shule zetu.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe mosesjohn08@yahoo.com na namba ya simu 0714840656.