Home Makala KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI KUNAMHARIBIA RAIS

KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI KUNAMHARIBIA RAIS

644
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU,

MAKALA iliyoandikwa na Prof. Zulfiqarali Premji na gazeti la ‘The Citizen’ (Alhamisi, Julai 20) mwaka huu, imenifanya niandike na kuyarudia baadhi ya maeneo ya ya maudhui  ya andiko lake kwa lugha ya Kiswahili, ili Watanzania ambao Kiingereza, kimewapita pembeni.

Prof Premji anasema kuwa kiongozi mwenye visheni ndiye anayeweza kuivusha nchi wakati wa hali mbaya. Na kwamba Rais Magufuli, kiukweli, anajitahidi kujaribu kuwaweka pamoja wananchi wa Tanzania na kuwapunguzia umaskini.

Anatamani kwamba wanachi wa nchi nyingine za Kiafrika, wangeiga mfano wa uongozi wake. Magufuli ameonesha kwa vitendo, kwa kutimiza yale aliyowaahdi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kuboresha maisha ya watu nakupunguza makali ya umaskini, ni mchakato wa muda mrefu. Kuna vizuizi vikubwa na changamoto nyingi na anachukua hatua za kutanzua vizuizi hivyo.

“Historia inandikwa upya, na labda, ataweza kukumbukwa kama kiongozi shupavu kama Julius Nyerere na Nelson Mandela. Kwa hiyo, Dk Magufuli angetazama upya msimamo wake kuhusu uhuru wa kutoa maoni. Nisingependa kuona urithi wake unaharibiwa na mwonekano wake kuwa ni kiongozi anayetumia mabavu na kwa hiyo, Dk. Magufuli anapaswa kuangalia msimamo wake kuhusu uhuru wa mawazo.”

Ana ainisha kuwa uhuru wa kusema ni suala nyeti, na inatakiwa umakini wa kuwianisha. Anashauri kuwa wadau wa vyombo vya habari na Serikali, wanahitaji kujishusha na kuwa na mjadala mahususi, ili waweze kuelewana.

Anaongeza kwamba pamoja na mambo mengi mazuri, ambayo yanasemwa juu yake dunia nzima, Rais Magufuli ajaribu kuyaweka sawa mambo haya, ili asiharibu mwonekano wake. “Itakuwa ni jambo la kukatisha tamaa, na labda atakuwa hakutendewa haki kama historia itamwonesha kwamba aliendesha utawala wa kiimla.”

Ananukuu ripoti ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (2017), Tanzania imeshuka kutoka namba ya 71 (2016), na kushika nafasi ya 83 katika nchi ambazo haziheshimu kanuni za uhuru wa habari. Ripoti inasema kwamba hali hiyo imetokana na kuvibana vyombo vya habari.

Anakariri maneno ya aliyekuwa Rais wa Marekani, Thomas Jafferson ambaye aliandika kwamba vyombo huru vya habari ni nguzo mojawapo ya kuendeleza demokrasia.

“….Vyombo huru vya habari, sio utashi wa mtu, bali ni ‘kiungo muhimu’ cha demokrasia yenyewe. Bila ukosoaji makini na kuandika taarifa zinazoaminika kwa weledi. Serikali haiwezi kutawala kama hakuna uwezekano wa serikali kujua wananchi wake wanafikiria nini, wanafanya nini na wanataka nini.”

Prof  Premji anasema uhuru wa kusema una ukomo. Hakuna nchi iliyo na uhuru bila mipaka, kwa sababu uhuru kama huo utaingilia haki na za watu wengine, na hii haikubaliki. Mwisho wa siku, uhuru kama huo utaharibu mwonekano wa serikali kama itaendelea kuvifungia au kuvidhibiti vyombo vya habari, ili viandike yale yanayopendeza tu.

Andiko la Prof. Prewmji limenifanya litupie macho yanayotokea kwingineko duniani hivi sasa, kwa sababu linatoa mfano halisi ya mambo hayo. Pamoja na vyombo vya habari kuminywa, wananchi huwa wanahamasishana kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi na kufanya mandamano, hata kama polisi wanazuia.

Matatizo ya kisiasa ya serikali ya Venezuela, kwa mfano, yametokana na rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, kutaka kuvinyamazisha vyombo vya habari. Wandishi wa kigeni na wa ndani, wamepigwa marufuku kuandika habari zinazo husiana na maandamano hayo. Lakini yeye anawahamasisha wafuasi wake wapeleke vita hiyo kwenye mitandao.

Wachambuzi wa mambo wanasema Rais Maduro, anaogopa yanaweza kumkuta yaliyomkuta mtangulizi wake, Hugo Chavez—ambaye aliondolewa madarakani kutokana na taarifa zilizokuwa zinaripotiwa na vyombo vya habari na kuandikwa katika mitandao ya kijamii kuhusu utawala wake.

Waziri wa Habari wa Venezuela, Luis Jose Marcano, ambaye kitaaluma ni mwanahabari, amekuwa akiviandama na kuvitisha vyombo vya habari vinavyomkoa Rais Maduro, na anaonesha upendeleo kwa vyombo vya habari ambavyo hufungamana na upande wake—jambo ambalo wachambuzi wanasema kuwa sio jema kwa mustakabali wa uchumi wa nchi hiyo. Tayari kuna dalili kwaamba Rais Maduro anataka kutorokea nchi nyingine.

Wandishi wa habari wa Venezuela, kama ilivyo hapa Tanzania, wamekuwa ‘neutralised’ na kujawa na hofu. Kama hilo halitoshi, ukandamizaji wa kisiasa unawagopesha kiasi kwamba serikali ikishamalizana na vyama vya siasa, kundi litakalofuata ni la wandishi wa habari. Viongozi wa serikali kote duniani, hawaipendi mitandao ya kijamii—wanaona kwamba inawaharibia kwa kuwa inawaanika.

Rais John Magufuli, aliwahi kutamka mbele ya wandishi pale Ikulu, kwamba angekuwa na uwezo, angeifunga mitandao ya kijamii.

Viongozi wa nchi nyingine za Kiafrika, Afrika Kusini, Misri, Uganda na Zimbabwe, ni baadhi tu ya nchi zinazotaka mitandao ya kijamii idhibitiwe. Lakini hata katika nchi zilizoendelea kama Ujerumani, zimetunga sheria kali sana dhidi ya mitandao. Hapa Tanzania, Bunge lililopita, lilifanikiwa kutunga sheria kandamizi ya makosa ya mtandaoni na kuweka vifungu vya kuwatoza faini kubwa au kifungo au vyote pamoja watakaopatikana na hatia.

Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, David Mahlobo, anataka mitandao ithibitiwe kwa kile anachoona kwamba vinakuza mgogoro ndani ya chama cha African National Congress na kashfa zinazomwandama Rais Jacob Zuma. Vyombo vya habari ambavyo havimwungi mkono Rais Zuma, vinaelezwa kwamba vimekosa uzalendo na kuwa vinaweza kuvuruga amani ya nchi.

Hata hapa Tanzania, kuna kundi kubwa tu, la watu wanafikiri kwamba kumkosoa Rais Magufuli ni kukosa uzalendo. Haiwezekani watu wote wakawa na fikra moja na mtizamo mmoja kuhusu mambo yote na wakati wote. Tunu za kidemokrasia hujengwa kutokana na kutofautiana katika mawazo na mtazamo.

Rais Magufuli anatakiwa kuwa makini na watu wanaomsifia tu, awasikilize kwa makini zaidi  wanaomkosoa maana nao wanaitakia Tanzania mambo mema.