Home Habari KUHAMIA DODOMA: Machungu yaibuka

KUHAMIA DODOMA: Machungu yaibuka

1653
0
SHARE

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

HARAKATI za kuhamishia Serikali mkoani Dodoma, zimeanza kuwa chungu kwa baadhi ya wakazi wa mkoa huo, RAI limedokezwa.

Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), mwishoni mwa mwezi uliopita inadaiwa kutoa notisi ya siku 28 kwa watu ambao hawajakamilisha malipo ya viwanja vyao.

CDA imewatahadharisha wasiokamilisha  malipo yao ndani ya kipindi hicho kuwa viwanja vyao vitapokwa na mamlaka hiyo.

Kutokana na agizo hilo kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wanaomiliki viwanja hivyo kuvikosa, kwa kile kinachodaiwa kuwa siku zilizotolewa ni chache.

Maeneo ambayo hivi sasa yanaonekana kuwa keki ni pamoja na, Kisasa, Nkuhungu na Kikuyu.

Akizungumza na RAI kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja kati ya watu wanaodaiwa kupewa notisi hiyo alisema; “CDA wametoa muda mfupi sana sisi wenye viwanja vitatu na wengine wenye zaidi ya vitatu tunaweza kupoteza maeneo yetu, maana hali ya fedha katika wakati huu ni ngumu mno.

“ Tangu Rais atangaze Serikali yake kuhamia Dodoma hali ya maisha imezidi kuwa ngumu,  maisha yanakoelekea yatakuwa magumu zaidi hivyo hatutaweza kuokoa maeneo yetu”.

Katika mabadiliko ya mkoa huo makundi mbalimbali yameanza kunufaika wakiwamo madalali wa nyumba na viwanja pamoja na ombaomba.

Rais Magufuli alitoa kauli ya kuhamia Dodoma Julai 23, 2016 wakati akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu maalumu wa chama hicho.

“Nitahakikisha katika awamu ya uongozi wangu, Serikali inahamia Dodoma, najua viongozi wengine wote nao watanifuata, kwa kuwa sasa miundombinu ya Dodoma inaweza kukidhi mahitaji yote” alisema.

Katika kuchagiza ndoto hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema atahakikisha ifikapo Septemba mwaka huu atakuwa ameshatekeleza agizo la Rais.

Waziri Mkuu alisema uamuzi huo usichukuliwe katika dhana ya kisiasa kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodai bali ni utekelezaji wa sheria ndogo tu zilizotungwa na Bunge.

“Nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma ifikapo Septemba,” alisema Majaliwa wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo ya siku ya Mashujaa wiki iliyopita.

Baadhi ya mawaziri tayari wameonekana kuunga mkono mpango wa kuhamia Dodoma akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ambaye alitangaza kuhamia Dodoma kuanzia wiki hii.

“Mchakato wa kuhamia Dodoma umekwisha, kilichobaki kwa sasa ni utekelezaji, mimi na manaibu mawaziri wangu tunahamia wiki ijayo ili tukamkaribisheWaziri Mkuu, Kassim Majaliwa anayehamia Septemba mwaka huu,”alisema.

Alisema kila kiongozi anayehamia Dodoma, inabidi awakute walio chini yake ili wampokee, hivyo aliwataka watendaji walio chini yake watangulie kwa ajili ya kumpokea.

Dodoma kuwa na miji miwili

Akizungumza na RAI Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Paskasi Muragiri, alisema Mji wa kiserikali utaanzia katika eneo la Ihumwa kisha Kijiji cha Mtumba mpaka katika eneo la Ikulu ndogo ya Chamwino.

Alisema katika maeneo hayo kutakuwa na ofisi za wizara pamoja na za mabalozi, wakati mji wa kibiashara utakuwa sehemu ambayo kwa sasa ni Mji wa Dodoma.

“Hilo lilipangwa katika Master Plan ya mwaka 2010-2030 ya kuhakikisha Makao Makuu ya Nchi yanakaa vizuri  kuanzia kwenye barabara za kuingia na kutoka, ili kusiwe na msongamano,” alisema.

Bei za viwanja

Aidha, alitaja bei za viwanja kuwa wanauza kwa Square 1 kwa Sh 5,500 mpaka 10,000 katika viwanja vya makazi.

‘’Kitaalamu  maeneo hayo tunayaita Medium  Density na maeneo tunayouza  kwa sasa  ni Miganga na Mkalama yaliyopo nje kidogo ya Mji wa Dodoma.

“Viwanja kwa ajili ya uwekezaji mkubwa  Square 1 inauzwa kwa Sh 1,330. Maeneo haya kitaalamu tunayaita Low Density na kwa hapa Dodoma ni Itega na Ndejengwa’’ anasema

Ardhi ipo ya kutosha

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi huyo aliwatoa hofu Watanzania wanaokwenda Dodoma, kuwa ardhi ipo ya kutosha.

‘’Hata wakija kuanzia sasa mpaka miaka 30 watapata ardhi tuna maeneo mengi ndio maana Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianzisha Mamlaka ya CDA kwa ajili ya kazi kama hii,’’alisema

Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa angalizo kwa wale wanaotaka kununua viwanja wasinunue bila ya kupitia CDA.

‘’Viwanja tusinunue kienyeji, tufuate taratibu watatokea wapigaji wa dili watu wataumia, wewe njoo ofisini kwetu kama unataka kiwanja utapata’’ alisema.

Eneo la wawekezaji lipo

Ofisa Uwekezaji wa CDA, Abeid Msangi, alisema wametenga maeneo maalumu ya Itega na Njendengwa kwa ajili ya kujenga hoteli kubwa, ‘Apartments’ na nyumba ndogo ndogo za ghorofa.

Anasema eneo la Itega limeishajaa kwa sasa, ila Ndejengwa wametenga zaidi ya ekari 1500 kwa ajili ya uwekezaji mkubwa.

“Kuonyesha kwamba tulijipanga mapema katika eneo Uwekezaji, kule Ndejengwa miundombinu iliishafika mapema kule kuna maji, umeme pamoja na barabara za lami na Taasisi nazo zimeishafika kununua maeneo hayo,’’ anasema Msangi

Bei za nyumba za paa

Uchunguzi uliofanywa na RAI umebaini bei za kupanga nyumba kwa sasa zimeongezeka kutokana na agizo hilo la Rais.

RAI lilizungumza na msemaji wa Chama cha Madalali Mkoa wa Dodoma (MSG), Yassin Mbijima, ambaye alikiri kuwepo kwa hali hiyo kutokana na Rais kutangaza Makao Makuu ya Nchi kuhamia mkoani humo.

Mbijima alisema wamekuwa wakipata kazi ya kutafuta nyumba za kupanga kwa wingi tofauti na zamani.

‘’Maisha Dodoma yamebadilika, kila mtu anataka nyumba ya kupanga, mfano Area D, C, Ipagala, Nkuhungu na Kisasa, ukitaka kupanga ni lazima uwe na zaidi ya Sh 700,000, hiyo ni kodi ya mwezi,’’alisema

“Kwenye upangaji wa vyumba nako bei imepanda ambapo awali walikuwa wakipangisha kuanzia Sh 30,000 hadi 50,000, kwa mwezi, lakini sasa wanapangisha kuanzia Sh 70,000 mpaka 100,000 kwa chumba kimoja.

“Natoa wito kwa wale wanaotaka nyumba mkoani Dodoma kuwa waangalifu,  waende kujiridhisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) au Manispaa pindi wanapouziwa,” alisema.

Ombaomba wachekelea

Aidha, RAI lilizungumza na baadhi ya ombaomba waliopo mkoani hapa, ambapo waliishukuru Serkali kwa kukubali kuhamia Dodoma.

Mmoja wa ombaomba hao, Zaituni Masima ambaye huomba katika Stand ya Mkoa wa Dodoma, anasema bahati imewafuata kwao.

“Kila siku wanasema turudi Dodoma sasa wametufuata, ukitaka niendelee kuzungumza na wewe nipe fedha.’’

Baada ya kupewa alimwita rafiki yake ambaye naye hutumia eneo hilo la Stand kuomba fedha, ili naye atoe maoni yake.

Rafiki yake huyo aitwaye Hawa Ndahani, alimpongeza Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge.

“Mimi nilikuwa Dar es Salaam, nilirudishwa na yule Mkuu wa Mkoa mweupe (Mecky Sadick), nilihuzunika sana ila Mungu hamtupi mja wake wanatufuata sasa,’’ anasema

Viongozi wa dini wafunguka

Kwa upande wake Kaimu Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Ahmed Said alisema hii ni zaidi ya fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma.

Sheikhe Said aliitaka Serikali kutenga maeneo makubwa kwa shughuli za maziko, kwani watu watakaoingia katika Mkoa wa Dodoma watakuwa wengi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo (UMKD) Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Dk. Eliya Mauza, ameitaka Serkali kutenga eneo la pamoja kwa ajili ya maombi.

“CDA watenge eneo la pamoja kwa ajili ya maombi bila kujali dini ya mtu, pamoja na hayo waangalie namna ya kugawa viwanja kwani unakuta sehemu moja kuna makanisa saba na misikti mitatu, wagawe kulingana na eneo,’’ anasema.

RAGE: Kulikuwa na hujuma Serikali kuhamia Dodoma

Akizungumza na RAI mapema wiki hii, aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, ambaye pia aliwahi kuwa mtumishi katika Mamlaka ya Ustawishaji wa Mji wa Dodoma (CDA), alisema suala la kuhamia Dodoma lilikuwa limeshaamuliwa muda mrefu na Mwalimu Julius Nyerere, ila lilihujumiwa.

“Hakuna kitu kinachouma kama kupanga mikakati, lakini ukashindwa kuitekeleza. Nasema hivyo kwa sababu maofisa wa Mji wa Abuja-Nigeria, walikuja kujifunza kwetu kwa maana ya kunakili ‘master plan’ ya Mji wa Dodoma. Sasa Serkali ya Nigeria imeshahamia huko Abuja.

“Nikiri tu hadharani kuwa kulikuwa na hujuma za makusudi kuchelewesha kuhamia Dodoma, kwa sababu wakati ule, kulikuwa na sheria ambayo inazuia wizara kujengwa Dar es Salaam, lakini nilishindwa kuelewa nini kilisababisha sheria hiyo ikabadilishwa na wizara zikaanza kujengwa Dar es Salaam badala ya Dodoma.

“Uamuzi huu wa Rais Magufuli ni wa wakati muafaka, hili suala linawezekana halina mjadala, ila lazima Rais apeleke bungeni sheria nyingine tena kuzuia wizara kujenga Dar es Salaam, wote wakajenge Dodoma, ndiyo maana hata Ofisi ya Tume ya Uchaguzi wamekwenda kujenga Dodoma. Kwa hiyo, kama wangefuatilia mapema, leo ingekuwa mbali sana. Kiujumla Dodoma imepangwa vizuri, miundombinu yake mizuri. Ni jambo ambalo linawezekana kabisa, ingawa kasema mwisho wa miaka yake mitano watahamia huko, lakini nadhani hata ndani ya miaka miwili inawezekana,” alisema.