Home Latest News Kuhamia Dodoma ni kuwakomboa walipa kodi

Kuhamia Dodoma ni kuwakomboa walipa kodi

1675
0
SHARE
Eneo la katikati ya mji wa Dodoma

MIAKA 43 iliyopita Chama cha TANU kilichokuwa kinatawala Tanzania Bara kilifanya uamuzi wa kihistoria kupitia vikao vyake halali na kufanya tafakuri jadidi.

Uamuzi wenyewe ulikuwa wa kuyahamisha makao makuu ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka yalipo sasa hivi yaani Dar es Salaam na kuyapeleka Dodoma.

Uamuzi huo ulizingatia mambo mengi lakini moja ambalo lilizungumzwa sana ni kwamba Dodoma ni katikati ya nchi kutoka katika kona takriban zote yaani Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Mantiki yake ni kwamba kwa sababu serikali kuu kati yake ni kutoa huduma kwa wananchi wote basi ni vyema huduma hiyo ikawa katikati ya nchi ili kila aiihitajiye asiwe mbali nayo.

Bila shaka ulikuwa ni uamuzi wa busara sana ingawa yaliyojiri baada ya uamuzi huo ni historia ndefu sana ambayo itahitaji watafiti wa historia na masuala ya utawala wa siasa kututanabahisha hasa kwanini imetuchukua miaka 43 kufikia hapa tulipo, na badala ya kuwa na serikali ikifanya kazi kutoka kituo kimoja tumejikuta tunaendesha serikali moja kutoka vituo vikuu viwili kutegemea msimu wa mwaka.

Watu wanauliza maswali mengi ambayo majibu yake si rahisi kuyapata moja kwa moja, bila shaka vizazi vijavyo vitauliza na kutaka majibu ingawa majibu yenyewe wanayo watu wa kizazi kilichopo sasa madarakani na watangulizi wao. Kwanini imetuchukua miaka 43 kufanya uamuzi wa kutenda kilichokuwa kimeamuliwa na ngazi ya juu kabisa ya kisiasa katika nchi ya utawala wa chama kimoja?

Kwanini vyombo vya juu kabisa vya maamuzi katika utawala wa chama kimoja, katika mazingira ya chama kushika hatamu kwelikweli, vilifanya maamuzi makubwa na mazito na kuitangazia dunia nzima lakini utekelezaji wake ukasuasua kiasi cha kusababisha hasara kubwa kiuchumi na kuacha maswali mengi ya utashi wa kisiasa na kijamii wa utekelezaji wake?

Wiki iliyopita hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameamua kutumbua jipu kubwa kuzidi yote nchini. Alitumia jukwaa kubwa kuzidi yote ya chama tawala kilichotokana na TANU na ASP kutangaza si sera ya kuhama bali utekelezaji wa uamuzi wa kuhamia Dodoma.

Kwa wale waliokuwa wakifuatilia kwa karibu suala la kuhama kwa makao makuu ya serikali lilikuwa ni tamko la kushtukiza na ambalo hawakulitarajia kutolewa kwa staili hiyo.

Rais Magufuli hakusimama pale kuomba utekelezaji bali alitoa tamko la ahadi kwamba katika kipindi chake kilichobaki kabla ya 2020 serikali itakuwa imehamia Dodoma.

Kama vile hiyo haitoshi juzi katika sherehe za Mashujaa ambazo zilifanyika Dodoma kiongozi huyo alirejea kwa ufasaha zaidi kwamba katika kipindi cha miaka minne na miezi minne ambacho kimesalia katika uongozi wake wa miaka mitano hadi 2020 serikali yote itakuwa imehamia Dodoma.

Hilo likafuatiwa na tamko la Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa kwamba yeye Waziri Mkuu atahamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu.

Tamko la Waziri Mkuu Majaliwa limekuwa ni changamoto kwa mawaziri wengine ambao bila shaka itakuwa hayumkiniki wao kuendelea kuwa Dar es Salaam wakati mkuu wao wa kazi yupo Dodoma moja kwa moja si kwa ziara ya kushiriki vikao kama ilivyozoeleka kwa miaka takriban 43!

Kwanini tunaupigia chapuo uamuzi wa kuhama kwa vitendo kwenda Dodoma? Kwa nini tunasema kwamba kutokuhamia Dodoma ni kitendo cha kukisaliti chama cha TANU na waasisi wake ambao walichukua madaraka baada ya uhuru na kufanya tafakuri na kuona ni muhimu kuyahamisha makao makuu ya serikali ili kuipeleka karibu na wananchi?

Kwa miaka yote 43 tumekuwa tukiendesha serikali kutoka katika vituo viwili jambo ambalo kiuchumi limekuwa ni mzigo mkubwa sana. Kama tumekuwa tukilalamika kwamba gharama za kuendesha serikali yetu ni kubwa ni wazi kwamba moja ya sababu za kuongezeka maradufu kwa gharama hizo ni kuwa na vituo viwili vya uendeshaji wa serikali.

Tuna ikulu mbili, nyumba za kuishi mbili mbili za takriban kila kiongozi. Viongozi wakuu wana makazi kote kote na hili si jambo la busara sana kwa serikali ya nchi masikini kama Tanzania.

Wakati wa vikao vya Bunge viongozi wakuu wa wizara huondoka na msururu wa wasaidizi wa ngazi mbalimbali na kuhamia Dodoma. Kwa kufanya hivyo na kwa mujibu wa sheria za kazi hao wote wanaoandamana na hao wakubwa ikiwa ni pamoja na wakubwa wenyewe wanahesabiwa kwamba wapo nje ya kituo cha kazi.

Kwa lugha nyingine ni kwamba viongozi na watumishi wote wa wizara wanaotokea Dar es Salaam kwenda Dodoma wanahesabiwa kwamba wapo safarini na hivyo hulipwa posho zote stahiki za mtu anayekuwa nje ya kituo cha kazi.

Aidha, ofisi kama ya Bunge inakuwa na shughuli Dar es Salaam na Dodoma. Kwa wanaokuja Dar es Salaam kwa ajili ya vikao vya kamati mbalimbali za Bunge wanahesabiwa kwamba kituo chao cha kazi ni Dodoma na wanapokuja Dar es Salaam wanakuwa nje ya kituo hivyo bila shaka wanapata stahiki zote astahilizo mfanyakazi anapokuwa nje ya kituo.

Ukiachilia mbali gharama hiyo ya uendeshaji ambayo ni kubwa na bila shaka imekuwa ikiwaumiza walipa kodi wa nchi hii pia kuna gharama inayolipwa na raia wanaotaka huduma za serikali na vyombo vyake kutokana na kuzagaa kwa huduma hizo.

Chukua mfano mtu ambaye anataka kuanzisha biashara ya uvuvi anapokuwa anataka huduma ya serikali kuu anakumbana na nini. Kwanza wizara ya uvuvi ipo Vetenari jirani na kituo cha TAZARA jijini Dar es Salaam. Akitoka hapo anapigwa uhamisho kwenda wizara ya biashara mtaa wa Lumumba. Akitoka Lumumba anatakiwa aende kwenye Mazingira Regent Estate na akitoka huko apigwe danadana kwenda TFDA huko External na pengine aishie kuambiwa arejee Ubungo ambako TBS walipo na kadhalika. Ili mradi shughuli za serikali zimetapakaa kote katika jiji la Dar es Salaam ambalo lina msongamano mkubwa mno na unaofanya raia kuziona huduma za serikali yao kuwa ni adhabu.

Tayari kuna hoja mbalimbali zinazotolewa na wachambuzi mbalimbali kuhusu gharama za kuhamisha shughuli za serikali. Wengine wanadai kwamba gharama hizo ni kubwa lakini hawajiulizi ni gharama kiasi gani inatumika katika kuendesha mifumo miwili inayofanana mmoja Dar es Salaam na mwingine Dodoma.

Pengine wanaohoji wanazo sababu za msingi. Wengine wanasema kwanini ni kiongozi huyu ndiye ameamua kuchukua uamuzi na kwanini waliotangulia hawakufanya hivyo. Jibu lake ni kwamba kila kitu kina wakati wake. Waliotangulia hawakuliona hilo kama kipaumbele lakini huyu ameamua kulishughulikia hilo kwa sababu ni wazi kabisa kwamba kuna gharama kubwa sana walipa kodi wanaibeba bila ya sababu yoyote ile.

Dodoma ni Tanzania na maendeleo yake yatasaidia kuifanya Dar es Salaam ipumue. Hivi sasa ni wazi Dar es Salaam imevimbiwa sana na kama hatua za makusudi kama hii ya kuhamisha shughuli za serikali hazitachukuliwa tena haraka  ni wazi kwamba hata tujenge njia za juu nyingi kiasi gani mwisho wa siku litakuwa ni jiji la hovyo sana ambalo hata hiyo huduma ya serikali kuipata itakuwa ni mateso badala ya faraja.

DK. GIDEON SHOO, +255 784 222 293