Home Habari Kujipitisha kwa wananchi si kosa Kikatiba

Kujipitisha kwa wananchi si kosa Kikatiba

309
0
SHARE

Na LEONARD MANG’OHA

Ni mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge  mwaka 2020 na kuhitimisha kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya Rais, Dk. John Magufuli.

Ni muda wa kila chama kujitafakari ni kwa namna gani kitaingia katika uchaguzi huo, ili kuhakikisha kinajikusanyia viti vingi vya udiwani, ubunge na kura nyingi za urais.

Bado mikutano ya hadhara haijaruhusiwa, vyama vya upinzani vinaendeleza vilio kuhusu mikutano, ili viweze kujijenga kuelekea uchaguzi huo.

Ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), tayari vuguvugu limeanza chini kwa chini, kiasi cha Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally, kushangazwa na baadhi ya wana-CCM walioanza kuugua ugonjwa wa kusaka urais na kuibua makundi ndani ya chama, akisema kuwa  wanawajua na wameanza kuwafuatilia.

Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, kuna watu tayari wameanza kupanga safu za urais wa mwakani na ule wa 2025—hasa wale wanaotaka kuutwaa urais wa Zanzibar baada ya kumalizika kwa muhula wa pili wa Dk. Mohamed Shein hapo mwakani, huku akisisitiza kuwa hawatakuwa na nafasi katika uongozi.

Kutokana na hali hiyo, anadai kuwa wanaofanya kampeni mapema wametangaza vita na yeye na wanatakiwa kujiandaa kwa vita hiyo.

Dk. Bashiru aliwahi kutoa onyo kama hilo Agosti 18, mwaka jana, alipokuwa ziarani Visiwani humo ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia kuhusu mbio za urais Visiwani humo na kuwaonya wana-CCM walioanza kampeni kabla ya muda wake na kuwataka kuzingatia kanuni na katiba ya chama chao.

Katika mkutano na wadau wa habari hivi karibuni, Dk Bashiru alisema chama hicho kina taratibu zake za kupata viongozi, kwani hata rais aliyepo madarakani, atapaswa kuomba ridhaa ya wana CCM ili ateuliwe tena.

Anadai kuwa uongozi wa chama ulio madarakani chini ya Mwenyekiti, Dk. Magufuli, uko imara na hauwezi kuyumba wala kuyumbishwa, na katu hauta mbeba mtu yeyote.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa mwaka 2014, Kamati Kuu ya CCM, iliwapa onyo kali aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, kwa kosa la kuanza kampeni za urais mwaka 2015 kabla ya muda.

Wengine waliokubwa na onyo hilo ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Kwa CCM huu umekuwa ni utaratinu wao wa ndani ya chama—kwamba mwanachama yeyote hatakiwi kujiandaa na uchaguzi kabla ya muda, huku akitoa nafasi kwa rais wa sasa kukamilisha  kipindi chote cha mihula miwili ya uongozi.

Lakini kwa nini licha ya kuwapo utaratibu huu wa ndani, wanachama wanaendeleza vitendo hivi. Ni wazi kuwa heunda hawaupendi utaratibu huo, na ndiyo maana wanajionesha wazi kuwa wanautaka urais.

Ni imani yangu kuwa utaratibu huu uliwekwa, ili kuwadhibiti mabwenyenye na wenye uroho wa madaraka, kutumia mwanya huo kujitayarishia njia ya kuutwaa urais wa nchi kwa nguvu zao.

Tutakumbuka jinsi ambavyo chama hicho kilijikuta katika upinzani wa ndani wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, hali iliyoibua makundi na kuleta mpasuko katika chama.

Mgawanyiko huo ulitokana na pande mbili zilizojitokeza kuutaka urais, kabla ya busara ya baadhi ya wazee wa chama hicho, na hatimaye kupatikana Dk. Magufuli ambaye si watu wengi walimfikiria kuwa angepenya katika kinyang’anyiro hicho.

Utaratibu huu umewekwa na chama kupitia wanachama wake wakati huo, wakiuona kuwa unawafaa, na sasa miongoni mwao wanaukataa kwa kwenenda kinyume cha utaratibu wa chama chao.

Nadhani hili si jambo la kuwapotezea muda kiasi cha kuufanya umma kuhisi ndani ya CCM kuna fukuto la chini kwa chini. Bali ni jambo linaloweza kumalizwa na wana-CCM wenyewe kupitia vikao vyao vya chama.

Kama walivyoweza kukubaliana kuwa na mfumo huo, ndivyo wanaweza kukubaliana na kuuondoa, bila kuathiri usitawi wa chama na shughuli nyingine—hasa zile zinazohusisha mtu mmoja mmoja.

Wana-CCM watambue kuwa Katiba ya nchi inaruhusu kila mmoja ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Kwa mantiki hiyo, kile kinachofanywa na baadhi ya wanachama wake, sio kosa la kisheria, ila ni batili kulingana na utaratibu wa chama chao.

Mwisho.