Home Makala KUJITENGA TENA KWA BIAFRA KWANUKIA

KUJITENGA TENA KWA BIAFRA KWANUKIA

1581
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Miaka 50 baada ya jimbo la zamani la mashariki la Nigeria kujitangazia kujitenga na kuwa Jamhuri ya Biafra, kitendo ambacho kiliibua vita mbaya na ya kikatili ya miaka mitatu, nchi hiyo bado inakabiliwa na tishio la kumeguka.

Sasa hivi katika maeneo ya wakazi wa kabila la Ugbo kusini mashariki kuna vuguvugu la wito wa kutaka kujitenga kutoka serikali kuu ya Abuja ma kuunda tena taifa la Biafra.

Na jinsi hali ilivyo hatua za Rais Muhammadu Buhari za kukandamiza harakati hizo zinazidi kuchochoea vuguvugu na kuongeza ari kwa wakazi hao kudai uhuru. Hivyo wachunguzi wa mambo wanaona kwamba serikali ya Buhari inabidi ibadili msimamo na kuanzisha mazungumzo.

Wanamwambia Buhari ni vyema akaelewa vyanzo vya vuguvugu hilo, na wanataja ni pamoja na masuala ya siasa na ya kiuchumi. Wanasema tangu kwisha kwa Vita ya Biafra takriban nusu karne iliyopita, Waigbo ambao ni moja ya makabila makuu matatu nchini humo wamekuwa wakipuuzwa.

Wanasema tangu rais wa kwanza wa nchi hiyo Namdi Azikiwe katika miaka ya 60, ambaye hata hivyo hakuwa na mamlaka kamili (ceremonial figurehead), hakuna mtu mwingine wa kabila hilo alichaguliwa kuongoza nchi.

Aidha wanasema hata katika wadhifa wa umakamu wa rais, hakuna mwingine wa kabila hilo aliyepata wadhifa huo tangu Alex Ekweume katika kipindi cha 1979-83.

Hali ya namna hii iliendelea katika vipindi vyote vya utawala wa kijeshi na Muigbo aliyewahi kuwa mkuu wa nchi kupitia mapinduzi ya kijeshi Meja Jenerali Johnson Aguiyi-Ironsi, aliuawa miezi saba tu baada ya kuchukua madaraka.

Hata katika utawala, serikali ambazo zimekuwa zikiongozwa na watu wa kutoka kaskazini wamekuwa wakilipuuza eneo hasa katika mgawanyo wa maeneo ya serikali za mitaa, mgawanyo ambayo huamua kiasi cha fedha za maendeleo wanazopangiwa.

Sehemu hiyo ya kusini mashariki ina serikali za mitaa 96 tu kati ya jumla ya serikali 774 nchi nzima.

Madai mengine ni kwamba pamoja na utajiri mkubwa wa mafuta yasiyosafishwa yanayotoka eneo hilo, eneo hilo limekuwa likitengewa fedha kiduchu za maendeleo.

Hivyo chini ya Buhari, manung’iniko haya yamekuwa yakiongezeka. Kwa kuwa hakuna Muigbo anayeongoza chombo chochote cha ulinzi na usalama, hivyo wanadai hawana sauti katika maamuzi muhimu ya nchi.

Lakini kitu kilichowakasirisha zaidi Waigbo ni kauli ya Buhari aliyoitoa baada tu ya kushinda urais mwaka 2015. Alisema: “Majimbo yaliyonipa asilimia 97 ya kura hayawezi kuhudumiwa kama yalle yaliyonipa asilimia 5 za kura.”

Kwa wakazi wengi wa kusini mashariki ambao walimpigia kura Jonathan Goodluck, kauli hiyo iliwatia wasiwasi kwamba hawewezi kuhudumiwa sawasawa na wenzao wa kaskazini.

Profesa Victor Ukaougu, mwanazuoni wa Historia katika Chuo Kikuu cha Nigeria anasema karibu changamoto zote ambazo zilisababisha ile vita ya awali bado hazijatafutiwa ufumbuzi hadi sasa.
Anasema Nigeria ni nchi pekee ambayo ilikumbwa na vita kubwa ya wenyewe kwa wenyewe lakini hakuna, miongoni mwa watawala, aliyejifunza lolote chochote.
Mwaka 1999, miezi michache baada ya Nigeria kurudi katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi, kundi jipya la “Movement for the Actualisation of Independent State of Biafra (MASSOB)” lililjitokeza na kuanza kudai uhuru wa Biafra. Kiongozi wa kundi hili alikuwa Ralph Uwazuruike, mwanasheria aliyekuwa akitoa wito wa kuidai Biafra kwa njia za amani.
Hili kundi lilianzisha sarafu za Biafra na pasi za kusafiria. Hata hivyo baadhi ya wanaharakati walianza mapambano na vikosi vya serikali na hata vifo kutokea. Uwazuruike alitiwa mbaroni na kufunguliwa mashitaka ya uhaini, lakini aliachiwa 2007. Kundi hilo likaanza kufifia katika harakati zake.
Mwaka 2014 kundi lingine lililodhamiria kudai kujitenga kwa Biafra – “Indigenous People of Biafra (IPOB)” lilianzisha harakati. Kundi hili lilianzishwa na Nnamdi Kanu huko Uingereza na pia lilisema litaweka madai yake kwa njia za amani, na liliungwa mkono na wakazi wengi wa eneo hilo la kusini mashariki.
Kundi hili liliweza kusaambaza ujumbe wake kwa watu wengi kutokana na kituo cha radio cha RADIO BIAFRA ambacho Kanu alikianzisha mwaka 2009 mjini London lakini kilielekeza matangazo yake kule Biafra na kufikia nchi nyingine nyingi pia.
Kituo hiki cha radio kilisaidia sana kulirudisha suala la madai ya uhuru wa Biafra katika ajenda, hasa miongoni mwa vijana ambao ndiyo waathirika wakubwa na kutengwa kwa jimbo hilo na hivyo kuwafanya wengi kupoteza imani na serikali kuu ya Nigeria.
Oktoba 2015 Kanu alitiwa mbaroni kwa mashitaka ya uhaini baada ya kutua uwanja wa ndege wa Lagos akitokea London. Wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wengine walidai kuachiliwa kwake, lakini aliendelea kushikiliwa bila dhamana.

Hata hivyo Kanu aliachiwa kwa dhamana mwezi uliopita.

 

  • Makala hii imeandikwa kwa msaada wa vyanzo vya Intaneti.