Home Makala KUJIUZULU NI UTAMADUNI ULIOPOTEA NA NYERERE

KUJIUZULU NI UTAMADUNI ULIOPOTEA NA NYERERE

811
0
SHARE
Ali Hassan Mwinyi na Abdallah Natepe (kulia) walijiuzulu uwaziri kwa hiari kutokana na kashfa zilizoibuka chini ya himaya zao.

*Vigogo wa Serikali wajiuzulu! Wakale wapi?


NA HILAL K. SUED

“Tukio limetokea ambalo ni vigumu kulizungumzia, lakini pia haiwezekani kulinyamazia.”

Nukuu hii ni ya Edmund Burke, Raia wa Ireland mwanafalsafa na mtunzi wa vitabu aliyeishi karne ya 18 akielezea maana ya ‘kashfa’.

Kwa kifupi, kashfa ni tukio linaloenezwa kwa kasi katika jamii kuhusu tuhuma za kosa au uovu unaotendwa na wakuu katika mamlaka za serikali au katika jamii au fedheha ambayo inachukiza jamii. Inaweza ikawa ni tukio la ukweli au ni zao la tuhuma za uongo au mchanganyiko wa yote mawili.

Aidha, kashfa zinazoonekana au kujikita katika masikio ya jamii ndizo zenye kuudhi, kwani kutenda dhambi kwa siri si kosa. Hivyo kosa huja pale mkosaji anapogundulika.

Baadhi ya kashfa huenezwa na ‘wapiga filimbi’ ambao huibua uovu ndani ya Serikali, mashirika au hata kutoka vikundi mbalimbali katika jamii. Kwa mfano, wizi wa mabilioni kutoka akaunti ya Escrow ya Benki Kuu (BoT) ambayo ilikuja kujulikana kama ‘Kashfa ya Escrow’ au ile nyingine kubwa iliyokuja miaka sita nyuma iliyojulikana kama ‘Kashfa ya Wizi wa EPA.’

Aidha, kashfa zisizo za ukweli ndani yake zinaweza zikasababisha kuwachafua watu wasio na hatia, lakini pia jitihada za kuzifunika kashfa, zinaweza zikakuza kashfa hizo hasa iwapo jitihada hizo za kuifunika zitashindwa.

Mfano wa hili ni ile kashfa ya Watergate iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Rais wa Marekani katika miaka ya 70, Richard Nixon. Kashfa hiyo ilikuwa kubwa pale jitihada za rais huyo za kutaka kuifunika zilishindikana na hivyo kumlazimu kujiuzulu urais.

Hapa Tanzania kashfa ni msamiati ambao haupo katika mamlaka za Serikali na katika jamii pia. Nasema hakuna kitu hicho kutokana na ukweli kwamba uitikiaji wake kwa wahusika wa kashfa hizo na mapokeo yake kwa mamlaka za Serikali na jamii umetoweka.

Ule utamaduni ambao husukumwa na maadili (principles) ya kwa wakubwa wanaokumbwa na kashfa kujiuzulu nyadhifa zao hakuna tena. Aidha, kilichotoweka ni jinsi baadhi ya Watanzania wanavyochukulia mapungufu hayo kwa namna ya kutoguswa au kutojali kinachoendelea.

Kuna baadhi ya wananchi wanahoji: “Vipi waziri ajiuzulu? Kwani yeye ndiye alikuwa anaendesha ile treni ya abiria iliyorudi nyuma na kuua mamia ya watu? Au yeye ndiye alikuwa anaendesha ile meli iliyozama na kuuwa maelfu?” Bila shaka mnafahamu ninachokizungumzia hapa.

Kujiuzulu kwa mawaziri au wakubwa wengine walio katika taasisi husika zinazokumbwa na matukio kama haya huwa ni kielelezo kizuri cha mfumo wa Serikali yenye kuwajibika, utawala bora na wa uwazi na si unaotokana na maneno tu ya wanasiasa wakiwa majukwaani.

Kujiuzulu ni hatua za kijasiri zinazoueleza umma kwamba cheo ni dhamana kutoka kwa wananchi na hivyo mkuu husika anaguswa na kuumizwa sana na jambo kama hilo kutokea chini ya eneo la uangalizi wake, hata kama litaonekana kuwa ni ajali, ameguswa nayo na kumuumiza sana.

Nimetaja ajali kwa mwonekano wake tu kwa jamii maana mara nyingi uchunguzi wa kina huwa haufanyiki. Tuchukulie matukio niliyoyagusia hapo juu ya MV Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria na kuua watu karibu 1,000 miaka zaidi ya 20 iliyopita au lile la miaka sita baadaye la treni ya abiria iliyorudi nyuma na kuua watu karibu 300.

Uchunguzi wa kina na wa dhati kabisa ungeonyesha kwamba maafa yote hayo yalitokana na uzembe mkubwa kwa baadhi ya watendaji, hali ambayo wakubwa wakiwamo mawaziri, walipaswa kuyafahamu na kuyashughulikia kabla.

Lakini si sahihi kabisa kusema kwamba utamaduni wa kujiuzulu kwa wakubwa haukuwapo kabisa. Ulikuwapo katika utawala wa Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kama vile ilivyo kwa mema na mazuri mengi  yaliyokuwapo wakati ule na ambayo yalitoweka na Mwalimu.

Ni vyema nikataja hapa katika matukio matatu makuu ya mawaziri wa Serikali kujiuzulu kutokana na kashfa zilizotokea chini ya maeneo yao, wawili walikuwa ni Wazanzibari. Watatu hawa walijiuzulu mara moja bila ya msukumo au mivutano yoyote.

 

Kwanza katikati ya miaka ya 70, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano, Ali Hassan Mwinyi (Mzanzibari), alijiuzulu mara moja baada ya kuibuka kwa ripoti za mauaji ya kikatili ya raia katika mikoa ya kanda ya Ziwa yaliyofanywa na maofisa usalama chini ya wizara yake.

 

Wakati anajiuzulu, Mwinyi alisema ni kashfa kubwa kwake vitendo hivyo kufanyika chini ya wizara yake bila ya kufahamu/kufahamishwa. Hiyo ni sawasawa na kusema kwamba ameshindwa kazi aliyopewa.

 

Waziri mwingine Mzanzibari ni Abdallah Natepe, ambaye pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mwanzoni mwa miaka ya 80 pale wafungwa watuhumiwa wa uhaini waliokuwa mahabusu katika Gereza la Keko walipotoroka. Natepe alijiuzulu mara moja na alisema anabeba lawama zote kwa aibu hiyo kutokea chini ya wizara yake.

 

Na Waziri Mkuu pekee aliyejiuzulu kwa hiari bila ya mivutano au shinikizo lolote ni Edward Lowassa katika kipindi cha mwanzo tu cha Jakaya Kikwete.

Katika kashfa hizo mbili kuhusu mawaziri, si Mwinyi aliyeshika silaha na kuua raia huko Kanda ya Ziwa na wala Natepe aliyewafungulia milango wale mahabusu ili watoroke Gereza la Keko.

Kwa kukumbushia tu, katika matukio ya kuzama kwa MV Victoria na kuanguka kwa treni, Limford Mboma ndiye aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC wakati ule) ambalo kitengo cha usafiri katika maziwa (Marine Services) kilikuwa chini yake.

Mkuu huyo hakujiuzulu pamoja na wito kumtaka kufanya hivyo kwani alionekana kabisa kutoguswa na vifo vyote hivyo vilivyotokea katika taasisi ziliziokuwa chini ya uangalizi wake.

Ni kweli, kuna mawaziri kadhaa ambao wamejiuzulu katika awamu za tawala zilizofuatia kutokana na kashfa kubwa zilizoibuka dhidi yao, lakini wote hawa walijiuzulu baada ya misukumo na mivutano mikubwa, ikiwemo shinikizo kutoka kwa jamii, vyombo vya habari na wanaharakati wengine.

Hawa ni pamoja na mawaziri chini ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa, Professor Simon Mbilinyi aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dr Hassy Kitine (Mambo ya Usalama wa Taifa) na Iddi Simba (Biashara na Viwanda).

Chini ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ni Andrew Chenge, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, Prof Sospeter Muhongo na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.

Hakuna utamaduni wa kujiuzulu kutokana na kashfa siku hizi; kilichobakia ni kung’ang’ania tu madaraka kwa kwenda mbele. Hata kuna baadhi yao sasa hivi wako tayari kutishia ‘kumwaga mboga’ iwapo wengine ‘watamwaga ugali’ ili tu wabakie madarakani au hata kwenda ‘kutubu’ katika nyumba za ibada au kusomewa dua za kumwepusha kuachia madaraka.

Katika hili, utawala wa Awamu ya Tano wa Rais John Magufuli umeingia na ‘gia’ ya ‘utumbuaji majipu’ ingawa utumbuaji huu kwa vigogo serikalini unaonekana kujikita zaidi dhidi ya watendaji wazembe kuliko wanaokumbwa na kashfa kama vile ufisadi au kuwa na vyeti feki. Hata hivyo baadhi ya wanaotumbuliwa huangukia mahala laini (soft landing) yaani baada ya muda hupewa wadhifa mwingine.

Ali Hassan Mwinyi alikuwa ni rais pekee aliyelifukuza baraza lake lote la mawaziri. Mapema mwaka wa 1990 baada ya manung’guniko mengi kutoka kwa wananchi kutokana na utendaji mbovu wa majukumu yao, Mwinyi aliwaita Ikulu mawaziri wake wote. Bila kukawia aliwaambia anataka wote waandike barua hapo hapo za kujiuzulu nyadhifa zao.

Akasimama Joseph Warioba aliyekuwa Waziri Mkuu na kuuliza: “Hata mimi?” Mwinyi akamjibu: “Naam, hata wewe, kwani Katiba yetu inasema waziri mkuu ni waziri pia.”