Home Makala Kukumbatiwa humfanya mtu aliyenyanyaswa kusahau unyanyasaji aliotendewa

Kukumbatiwa humfanya mtu aliyenyanyaswa kusahau unyanyasaji aliotendewa

980
0
SHARE

NA LEONARD MANGOHA NA MITANDAO

Makala iliyochapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) imemnukuu Mtalamu wa Saikolojia, Grace Destiny, kuwa kusalimiana kwa kukumbatiana ni zaidi ya salamu kutokana na mtu kunafanya mawasiliano yanayowasilisha moja kwa moja hisia za upendo baina ya watu wanaokumbatiana.

Mtalamu huyo wa saikolojia ya uhusiano na familia anasema kukumbatiwa ni ishara ya kukubalika na salamu na kwamba kuna manufaa zaidi kwa jinsia ya kike. 

Kupitia makala hiyo mtaalamu huyo anasema kuwa mwanamke na mtoto wa kike wanahitaji kukumbatiwa jinsia ya kiume na pale wanapokosa kukumbatiwa huwa wanakuwa na hisia za upweke.

”Mtu anapokumbatiwa hujihisi kuwa na hakikisho la juu ya usalama wake na hii humfanya atulie kiakili,” anasema mwanasaikolojia huyo.

 Anasisitiza kuwa wazazi wa kike na kiume wanapaswa kuwakumbatia watoto wao ili kuwaepusha na hisia za upweke ambazo watataka zijazwe na watu wengine. 

Anasisitiza kuwa wazazi wa kiume wanapaswa kuwakumbatia watoto wao wa kike kwani huwajengea uwezo wa kujiamini na kuhisi upendo wa baba zao.

“Kukumbatiwa ni muhimu kwa mfano mwanamke ambaye ananyanyaswa na mume wake, anaweza kuliwazwa au kubembelezwa tu kwa kukumbatiwa na hiyo ikamfanya asahau unyanyasaji aliotendewa na mumewe.

“Kwa jamii kama ya Wanyarwanda, kukumbatiana kunaimarisha hisia za umoja wa kijamii na familia ya kibinadamu kwa ujumla, mgusano wa kimwili hasa kwa jinsia tofauti ni muhimu ,” ”, anasemam mwanasaikolojia huyo.

Grace anasema, kukumbatiana hujenga hisia za udugu wa kaka na dada miongoni mwa jamii kama ya Wanyarwanda na kujihisi wako salama.

Grace ameeleza hayo alipokuwa akielezea BBC kuhusu utamaduni wa jamii ya kinyarwanda ambayo husalimiana kwa kumkumbatiana.

Kukumbatiana ni ishara kuu ya salamu ya watu wa kabila la Wanyarwanda, salamu hii ikiwa ishara ya furaha na upendo miongoni mwa watu wa jamii hii. Pia ni ishara ya furaha na upendo miongoni mwa watu wa jamii hiyo.

Huenda likawa jambo lisilo la kawaida kwa baadhi ya jamii nyingine za Afrika Mashariki hasa mtu kumkumbatia mtu yeyote anayekutana naye barabarani, lakini kwa jamii ya Wanyarwanda ni jambo la kawaida. 

Katika jamii hiyo kukumbatiana ni ishara ya upendo na furaha ya ndani ya moyo ambayo mtu anakuwa nayo kwa mtu mwingine 

Salaam hiyo ya jadi inaelezwa kuwa imekua ikiendelezwa kizazi hadi kizazi na huambatana na maneno kama vile ”Amashyo” ambapo anayekusalimia hukutakia kuwa na ng’ombe wengi na ”Yezu Akuzwe” akimaanisha ”Yesu atukuzwe” na maneno mengine mengi ya kutakiana kheri. 

Kutpitia utamaduni huo unaweza kumkumbatia mpenzi wako, baba yako, ndugu yako awe wa kike au wa kiume, baba mkwe, mama mkwe, mme mwenza, rafiki au tu mtu mwingine yoyote yule pale unapomkuta katika tukio au mahali popote mfano, katika familia, harusini, sokoni na hata njiani iwapo atakua na mtu unayemjua, hata kama haumfahamu.

Utamaduni wa kukumbatiana unavyotekelezwa na tamaduni za kisasa?

Kupitia makala hiyo Professa Malonga anasema hata iweje salamu ya kukumbatiana kamwe haiwezi kupotea kwa sababu ya umuhimu wake katika utamaduni wa Wanyarwanda, huku akilinganisha aina nyingine za salamu na anazoziita za unafiki.

Kutokana na mabadiliko na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali za kigeni, baadhi ya Wanyarwanda wanaoishi maeneo ya mijini wameanza kubadili mtindo wa salamu hii, wakijaribu kutosogeleana kimwili na baadhi wakiiga salamu za kawaida za kisasa kama kusalimiana kwa mikono au mabega hasa miongoni mwa vijana.

Hata hivyo wenzao wa maeneo ya vijijini bado wanaendelea kukumbatiana kwa ukaribu wa miili yao, kulingana na mila yao.

”Watu wengine wanakutana na kupeana mabusu, mwingine utamwona akiinama au anachuchumaa. Kwangu mimi salamu hizo ambazo zinatajwa kuwa za kisasa naziona kama za kinafiki”, anasema profesa Malonga.

Kwa mujibu wa makala hiyo zimeelezwa dhana mbalimbali zinazoaminika miongoni mwa watu ambazo zinatajwa kama faida za kukumbatiana ikiwamo khuongeza uwezo wa kinga ya mwili na kupunguza magonjwa ya moyo mbali na kupunguza homoni za Cortisol zinazosababisha msongo wa mawazo, kwa watu wanaokumbatiana mara kwa mara kwa muda wa sekunde kati ya 15 na 20 huwezesha miili yao kuongeza kiwango cha homoni za Oxytocin ambazo huimarisha mahusiano na kuimarisha urafiki zaidi.

Pia inaeleza kuwa utafiti uliofanywa na taasisi ya Marekani ya magonjwa ya akili unaonyesha kuwa kukumbatiana au kusalimiana kwa mikono kunaweza kusamsaidia mtu kupunguza msongo wa mawazo na athari zake, kukumbatiana humfanya mtu ajiamini kwani mtu anapomkumbatia mtu mwingine na kumwona akiwa mwenye furaha huwafanya wote wawili kujihisi wanajiamini. 

Kukumbatiana hutoa funzo la kupenda na kupendwa, na pia kutambua kuwa kila binadamu anamuhitaji mwenzake. huwafanya watu kutojifikiria kuwa ni wapweke na kuwafikiria watu, iwe baina ya wapenzi, ama wazazi na watoto wao, au baina ya watu wengine kukumbatiwa humfanya mtu ahisi anapendwa na kuwa mwenye furaha maishani mwake 

Inaelezwa kuwa baadhi ya Wanyarwanda hasa wanaoishi maeneo ya mpakani na DRC hivi karibuni wameanza kuhofia kusaliamiana kwa kukumbatiana kwa kuhofia maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.