Home Latest News Kukuza demokrasia ni jukumu la wote

Kukuza demokrasia ni jukumu la wote

228
0
SHARE
Waziri wa Katibu na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba

NA ANNA HENGA 

TANZANIA imeridhia mikataba mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na kikanda na kuwa sehemu yake. Mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu [Ibara ya 21(2) na (3)]. 

Vile vile Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Haki za Kisiasa (ICCPR, 1966). Hivyo Tanzania inawajibika kuendelea kulinda misingi ya demokrasia, hususan kuhakikisha kuwa viongozi wanaochaguliwa katika ngazi mbalimbali za serikali wanapatikana kupitia uchaguzi zinazoaminika na zinazoratibiwa na kuendeshwa kwa namna inayofuata misingi ya kidemokrasia.

Kwa kuzingatia hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekamilisha kazi ya kuboresha daftari la wapiga kura huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika mwaka huu 2020 kwa ajili ya kuchagua viongozi mbalimbali wakiwemo Rais, Wabunge na hata madiwani.

Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulifanyika kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya pili ulianza Aprili 17 na kukamilika Mei 4 mwaka huu Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar. Katika uboreshwaji huo ambao ulifanyika huku Taifa likikabiliana na janga kubwa la maambukizi ya virusi vya Corona, jumla ya vituo vilivyotumika kwa awamu ya pili ni 4,006 kwa nchi nzima.

Hii ni dhahiri kuwa mchakato huu una lengo kuu la kukuza na kuendeleza demokrasia nchini Tanzania. Ushiriki wa sekta isiyo rasmi katika ujenzi wa demokrasia ikiwa vijana wengi wako katika sekta isiyo rasmi hapa nchini, vijana hawa wanaume kwa wanawake wanao wajibu mkubwa wa kulinda na kukuza demokrasia. 

Imekuwa ni kawaida kuona makundi mbalimbali ya watu kutoka katika sekta isiyo rasmi kutumika katika shughuli za uchaguzi hapa nchini. Katika sekta isiyo rasmi yapo makundi ya wafanyabiashara wadogowadogo kama vile mama ntilie, machinga pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine hutumika katika kampeni za kisiasa na baadaye kubaki kuwa wahanga wa ufukara na umasikini mkubwa baada tu ya uchaguzi kumalizika. Ni vyema sekta hii ikaangaliwa upya ili kuweza kukuza na kulinda demokrasia nchini. 

Nimepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wajasiriamali kutoka katika sekra isiyo rasmi na kwa uwazi kabisa wameweza kueleza ushiriki wao katika masuala ya demokrasia hapa nchini; Mama Ntilie Scola Kamata (38) anasema anatambua wazi kuwepo kwa uchaguzi mkuu lakini suala hilo haliko akilini sana badala yake anachokifikiria zaidi kwa sasa ni usalama wa afya yake kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona. 

Hali halisi ni kwamba kwa wakati huu ugonjwa wa Corona umekaa zaidi kwenye akili za walio wengi, wengi wao wanasema, suala la uchaguzi ni muhimu lakini kwa namna ambavyo ugonjwa huu unavyoambukiza ndio inatia shaka. 

Wataalamu wa afya wanahimiza watu kupunguza mikusanyiko pamoja na kuchukua tahadhari nyingine zote zilizotolewa na wataalamu wa afya hapa nchini. Hata hivyo kuna baadhi ya wananchi kutoka katika sekta isiyo rasmi, waliokuwa na sifa za kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura walishindwa kujiandikisha kutokana na hofu ya kupata maambukizi ya Covid-19. Jambo la kushangaza ni kwamba katika hatua hiyo ya uboreshwaji wa daftari, wapo baadhi ya wananchi hususani katika sekta isiyo rasmi wenye sifa ya kujiandikisha kama wapigakura walijitokeza kuhakiki taarifa zao lakini wanasema wanahitaji kadi hiyo kwa ajili ya shughuli nyingine kama za kufungulia akaunti benki na wala si kupiga kura. 

Mwendesha pikipiki Hemed Salim (35) anasema ‘kiukweli maandalizi yamefanyika ya kuboresha daftari la wapiga kura, lakini kushiriki katika uchaguzi ni chaguo langu na itategemea na hali itakavyokuwa ya kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya Corona’ Kwa tathimini ya muda mfupi suala la maambukizi ya Covid-19 limeshakaa sana katika vichwa vya walio wengi na wana hofu kuwa huenda wasiweze kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi. Vilevile hali ya uchumi imeyumba sana hasa kwa wafanyabiashara wadogowadogo kama vile machinga pamoja na wanaofanya biashara ya usafiri maarufu kama bodaboda kwa kuwa watu wengi wamepunguza safari zisizo za lazima. 

Kukutana na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana katika sekta isiyo rasmi Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzisha uhakiki wa taarifa kupitia simu za mikononi imesaidia vijana wengi kushiriki kuhakiki taarifa zao ikiwa ni hatua ya awali ya ushirikishwaji wa vijana katika sekta isiyo rasmi katika uchaguzi mkuu. 

Ingawa baadhi ya vijana hawa wengi wanaendelea kusisitiza kwamba kujiandikisha inasaidia kupata kitambulisho ambacho kinaweza kutumika katika shughuli nyingine mbalimbali ukiachia mbali uchaguzi. Kwa upande wake Mamantilie Rehema Kassim (48)anasema wazo la kushiriki katika uchaguzi mkuu hana kwa sasa na kwamba anawaachia vijana waliotimiza miaka 18 nao waweze kushiriki.

Anaendelea kusema ‘maisha yamebadilika sana ninachokiwaza zaidi ni namna gani ya kupambana na maisha ili niweze kujikimu kimaisha maana uchumi wangu binafsi umepungua’. Mama huyu ametoa ombi lake kwamba kabla ya kufika kipindi hicho cha uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itoe elimu ya kina ya namna sahihi ya wafanyabiashara wadogo wadogo wanavyoweza kushirikishwa katika uchaguzi mkuu. Vilevile kama ambavyo elimu ya kujikinga na Corona ilivyoanza kutolewa mapema, ni muhimu zaidi hata kuelekea uchaguzi mkuu wanaohusika kuanza kutoa elimu mapema ili kuwapa watu hamasa na kuwaondoa hofu ya kupata maambukizi ya homa kali ya mapafu kwa kuwa bado dawa haijapatikana. 

Rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, dhana ya umuhimu wa uchaguzi inakamilika pale ambapo wananchi wanaposhiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi na hatimaye kupiga kura. Hivyo napenda kutoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uwanja wa ushindani wa kisiasa ni huru na wa salama kwa makundi yote hususani wanawake na vijana walioka katika sekta isiyo rasmi. 

Ni vyema kila mwananchi akawa na imani kuwa serikali wanayoipa dhamana ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano itahakikisha upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya kibiashara ikiwa ni pamoja na sera bora zinazowalinda wafanyabiashara wadogo katika sekta isiyo rasmi. 

Naamini kwamba utamaduni wa ushindani katika siasa ndio msingi wa kupatikana kwa uongozi bora katika mataifa mengi ulimwenguni ikiwemo nchi zinazoendelea kama Tanzania.