Home Latest News Kuna mengi tutayaona zaidi ya Vardy, Ibrahimovich

Kuna mengi tutayaona zaidi ya Vardy, Ibrahimovich

868
0
SHARE
zlatan Ibrahimovic
zlatan Ibrahimovic
zlatan Ibrahimovic

ALLY KAMWE NA MITANDAO,

KAMA unafikiri hisia za mashabiki wa soka England zitaishia kwenye fainali za Euro 2016 au Copa America pekee, kaa chini na ufikirie tena.

Kitu kikubwa kinachovuta hisia za mashabiki wa soka hivi sasa ni dirisha la usajili kwa ajili ya msimu ujao katika ligi mbalimbali barani Ulaya.

Usajili umekuwa gumzo kubwa kwenye vichwa vya mashabiki wenye hamu ya kuona namna vikosi vyao vitakavyoimarishwa kuelekea msimu wa 2016-17.

Tayari mpaka wakati huu, sajili mbalimbali zimeshakamilika huku tetesi nyingine zikizidi kupamba moto.

Mashabiki wa Arsenal wanasubiri kusikia ni lini Jamie Vardy atamwaga wino Emirates, huku mashetani wekundu wa Old Trafford wakikesha getini kumpokea Zlatan Ibrahimovic.

Msimu uliopita klabu za Premier League zilitumia zaidi ya pauni bilioni 1 kwa ajili ya usajili tu, lakini wakati huu kukiwa na ongezeko la pesa za haki za matangazo ya TV, matumizi ya pesa kwenye usajili yanatarajia kuongezeka pia.

Ukikitaja kikosi cha Manchester United, ujio wa Mourinho unakupa picha halisi ni usajili wa aina gani klabu hiyo itaufanya kwa kuzingatia falsafa za kocha huyo.

Ni lazima Mourinho atatamani mafanikio makubwa kwenye msimu wake wa kwanza akiwa na United. Atataka kubeba kombe sambamba na kufuzu UEFA msimu ujao.

Kuyatimiza haya ni lazima mabosi wa United wawe tayari kutoa pesa kwa Mourinho na si ajabu wakali hawa wa Old Trafford wakavunja rekodi yao ya matumizi ya usajili msimu huu.

Lakini wakati huohuo, majirani zao wa jiji, Man City wana Pep Guardiola ambaye amepewa kazi ya kuhakikisha anaifanya klabu hiyo kuwa tishio barani Ulaya.

Taarifa zinasema Guardiola amekabidhiwa fungu la pauni milioni 250 kwa ajili ya kufanya usajili wa kishindo katika dirisha hili.

Tayari mpaka sasa ameshafanikiwa kuinasa saini ya kiungo wa Borrusia Dortmund, Ilkay Gundogan.

Wakati haya yakiendelea katika jiji la Manchester, pale London kuna vita nyingine ya makocha wa Arsenal na Chelsea.

Arsene Wenger amekuwa na sifa ya ubahili. Kwa zaidi ya miaka 10, kocha huyu amesajili wachezaji wawili tu kwa dau lililozidi pauni milioni 20, Mesut Ozil na Alexis Sanchez.

Lakini kutokana na tishio la Man City, United na Chelsea, Wenger ameanza fujo kwenye dirisha hili la usajili kwa kutoa pauni milioni 30 kiungo Granit Xhaka.

Kwa upande wa Chelsea hawana cha kupoteza zaidi ya kumhakikishia fungu kubwa la usajili kocha wao, Antonia Conte.

Kutumia pesa si kazi ngumu hata kidogo kwa bosi wa ‘The Blues’, Roman Abramovich, hivyo ujenzi wa matajiri hawa wa jiji la London utaanzia kwenye fujo za dirisha la usajili.

Miongoni mwa majina makubwa yanayotajwa kutua Chelsea katika dirisha hili la usajili ni kiungo wa AS Roma, Radja Nainggolan na Paul Pogba.

Chelsea ni lazima wahakikishe wanatumia fedha zaidi ili kuvutia wachezaji hawa kuwa tayari kuacha kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao.

Liverpool walio chini ya kocha mwenye mbwembwe nyingi, Jurgen Klopp, wanatamani kurudi kwenye michuano ya Ulaya sambamba na kubeba taji la Ligi Kuu walilokosa kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Ni kama jicho la Klopp katika kuiunda upya Liverpool amelitupa zaidi nchini Ujerumani.

Mpaka sasa tayari ameshainasa saini ya kipa wa Mainz, Lorius Karius. Ikumbukwe kuwa Mainz ni klabu aliyowahi kuifundisha kabla.

Mbali na kipa huyo, bado Klopp ameweka rada zake kuwawinda wakali wa Borrusia Dortmund na Bayern Munich.

Inaaminika mpaka dirisha hili likifungwa, lazima Mjerumani huyu atakuwa ameinasa saini moja kati ya Marco Reus au  Mario Gotze, tusubiri tuone.

Lakini bado Liverpool wako kwenye mawindo ya kuinasa saini ya kiungo wa Leicester City, N’Golo Kante, ambaye anatajwa kupigiwa chapuo na kiungo Mbrazil wa timu hiyo, Philippe Coutinho.

Kuna mengi yatatokea katika dirisha hili la usajili, lakini kubwa zaidi ni matumizi makubwa ya pesa yanayotarajiwa kufanywa na klabu kubwa za nchini humo.

Hakika tunakwenda kushuhudia usajili mkubwa na wakihistoria awamu hii. Siku zote heshima hujengwa na pesa na kila kocha anataka heshima pale England hivyo lazima pesa itumike ya kutosha!