Home Makala Kuna ombwe kwenye usimamizi wa migodi

Kuna ombwe kwenye usimamizi wa migodi

1802
0
SHARE

(caption)Wachimbaji wadogo wakimwelekeza jambo mwandishi wa makala haya Sidi mgumia kwenye machimbo ya Kwedijava, Handeni mkoani Tanga.

NA SIDI MGUMIA, ALIYEKUWA HANDENI

Kukosekana kwa usimamizi thabiti wa shughuli za migodi nchini kuna hatarisha afya za wananchi na uharibifu wa mazingira kwa ujumla.

Kwa mujibu wa sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010 iliyofanyiwa mabadiliko makubwa mwaka 2017 kwa pamoja zimebeba dhamira ya kusimamia kikamilifu shughuli za uchimbaji wa madini migodini kwa kushirikisha kila mdau.

Kutozingatiwa na kusimamiwa kwa sheria hizo kunaibua kasoro na udhaifu kwenye maeneo mengi yenye migodi nchini.

Wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliana na kasoro hizo hasa kwenye maeneo yenye machimbo ya madini ya dhahabu.

Miongoni mwazo ni uharibifu wa mazingira hali inayohatarisha afya za  baadhi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa machimbo hayo.

Handeni ni moja kati ya wilaya 10 za mkoa wa Tanga ambayo pamoja na kujaaliwa  rasilimali ya madini ya dhahabu, bado wilaya hiyo iko nyuma kiuchumi.

Milima ya Magambazi ambayo iko pembezoni mwa wilaya hiyo ndio inayobeba idadi kubwa ya migodi ya wachimbaji wadogo.

Milima hiyo ya Magambazi iliyoko ndani ya Kata ya Kang’ata iko umbali wa Kilometa 30 kutoka Handeni mjini hadi Magambazi, idadi kubwa ya wakazi wa maeneo hayo wanamaisha duni na tegemeo lao kuu ni kilimo na ufugaji unaotegemea zaidi uoto wa asili.

Uchimbaji wa madini unaokwenda sambamba na ukataji wa miti umekuwa ukiiathiri jamii kubwa ya Magambazi na Handeni kwa ujumla, wachimbaji wadogo wengi wao hufikia hatua ya kutafuta kila namna kuhakikisha wanafanikisha matakwa yao.

Katika hatua hiyo hapo ndipo panapoharibiwa vyanzo vya maji kwa kukata miti ili kupata sehemu za kuanzisha maduara.

Aidha ongezeko la wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje wilaya hiyo yanawafanya wakazi wa eneo hilo lenye pilika pilika za uchimbaji wa dhahabu kutokuwa salama kiafya kutokana na uwapo wa ngono zembe.

Mbali na uharibifu wa mazingira na mazingira hatarishi ya afya, lakini pia ongezeko la watu huibua migogoro ya ardhi ya mara kwa mara.

Kwa ujumla eneo hilo linakusanya wachimbaji wadogo wadogo ambao shughuli zao hutegemea na mahali panapoweza kuwapatia dhahabu.

Si jambo la ajabu kwa wachimbaji hao kuchimba mashimo na kuyaacha kwakuwa hayana mali.

Hatua hiyo inawapa sura ya wazi kuwa wachimbaji wadogo wao ndio waharibifu wakubwa wa mazingira.

Ipo dhana kuwa kukosa zana za kisasa za uchimbaji wa madini ndiko kunakotajwa kuzalisha athari nyingi kwa mazingira.

Kukosa zana bora na utaalamu sahihi wa uchimbaji wa madini kunaisukuma jamii ya wachimbaji wadogo waliokuwa katika  machimbo ya Magambazi na baadae kutimkia kwenye machimbo mengine yakiwemo ya Kwedijava.

Moja ya sababu kuu ya wachimbaji wadogo kuondolewa Magambazi ni ukosefu wa zana za kisasa, hatua iliyoisukuma serikali kulibinafsisha eneo hilo kwa wachimbaji wakubwa.

Tayari serikali ya Wilaya ya Handeni imeshawakaribisha wawekezaji wageni ambao kwa kutumia teknolojia ya kisasa inaelezwa kuwa  watachimba kwa ufanisi na wakati huo huo kulipa kodi  kubwa, hata hivyo uamuzi huo unaonekana kuwa mwiba kwa wachimbaji wadogo ambao wanategemea kuendesha maisha yao kupitia migodi hiyo.

Kampuni CANACO ndio imepewa dhamana ya kuendeleza shughuli za uchimbaji Magambazi.

Kampuni hii ni kubwa na tayari wamepewa haki ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini kiasi cha madini kilichopo katika eneo hilo.

Mmoja wa mameneja wa kampuni hiyo ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini alisema kuwa pamoja na kuwapo kwa mvutano, lakini wao wapo kihalali na walishafanya mazungumzo na waliokuwa wakifanya shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo.

Alisema waliingia katika eneo hilo mwaka 2007 kwa ajili ya kuendesha shughuli za utafiti ikiwa ni  hatua za awali kabla ya kuanza kazi ya ujenzi wa mashine nzito  kwa ajili ya uchimbaji.

Walipoingia walikubaliana na wenyeji na walitumia fedha nyingi kuwalipa fidia ili wafanye shughuli yao kwa amani na utulivu.

Katika kipindi hicho waliendesha utafiti wa kujua mwelekeo na aina ya miamba iliyobeba dhahabu kwenye eneo hilo.

Lakini pia waliangalia tabia za kijiolojia za miamba hiyo bila kusahau thamani ya dhahabu itakayozalishwa.

MKURUGENZI HALMASHAURI

Pamoja na maelezo mazuri ya mmoja wa viongozi wa CANACO, lakini Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni, William Mafukwe anasema kuwa kuna sintofahamu iliyoibuliwa na kampuni hiyo.

Mafukwe anasema Canaco Tanzania Limited ndiye mwekezaji aliyeingia mkataba wa uchimbaji na Serikali, lakini Canaco hiyo imempa kazi Tanzania Gold Field ambao kwa sasa ndio wako kwenye eneo la mgodi wakiwa na mitambo yao na ulinzi wao.

“Wana kila kitu pale,  na hawako tayari kuachia huo mgodi ingawa hawatambuliwi na Serikali, sisi tunamjua Canaco kwasababu makubaliano yao waliyoandikiana sisi hatuyajui, hakuna mahali walisajili makubaliano yao, sisi tumekuja kujua baadae kuwa waliingia makubaliano na hata ulinzi waliouweka ni kwasababu wanajilinda ili Canaco asiingie kwenye mgodi.

OFISA MADINI HANDENI

Katika mazungumzo yake ofisa Madini wilaya ya Handeni Naiman Samana alisema Mgodi wa Magambazi ni mgodi ambao unatarajiwa kuchimba madini ya dhahabu na uko katika leseni ML 525-2014, ukiwa chini ya umiliki wa Kampuni Canaco Tanzania Limited.

“Tunachokijua ni kwamba awali kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kukabidhiana mgodi kati ya Canaco na Tanzania Gold Field wao waliingia mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kuindeleza ile leseni, baada ya serikali kujua suala hilo ililazimu taarifa zao zifike wizarani kwa ajili ya kushughulikiwa.

“Kwa mara ya kwanza hawakuijulisha Serikali juu ya makubaliano yao, lakini baadae Naibu Waziri alipokuja kuutembelea mgodi alihitaji walete makubaliano yao ili Serikali iweze kulifanyia kazi kujua kama ni mkataba halali au la!

MWENYEKITI KIJIJI CHA NYASA

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Nyasa Semeni Msekeni, akiongelea kunyanyaswa na kupigwa kwa wananchi alisema mgodi wa Magambazi ulikuwa wa wachimbaji wadogo ambao walikuwa hawana leseni kwahiyo baada ya mgodi kukabidhiwa kwa mwekezaji wachimbaji wadogo waliondolewa na kwasasa kuna ulinzi mkali ambao mwandishi wa makala haya aliushuhudia.

“Nilichojua mimi mi kuwa hakuna mtu anayepigwa ila mtu akiingia pale anahusishwa na ujangili, kwamba anataka kuiba hivyo anakamtwa na kupelekwa polisi.

“Hakujawahi kuletwa kesi kuwa mtu kapigwa kutoka mgodini, kila wanayemkamata anapelekwa kituoni na tangia walivyopelekwa wachache basi watu wakaacha kuingia mgodini  na hiyo ni tangu mwaka jana, yani mwaka umepita sasa.”

WACHIMBAJI

Abdala Ibrahim Mpuluzi aliyejitambulisha kama Inspekta wa Mgodi wa Kwedijava  anasema ingawa yapo mambo ambayo hayajakaa sawa, lakini wanaamini taratibu za kumleta mwekezaji zimefuatwa.

Anasema bado hawajalipwa, lakini Mwekezaji wanaemtambua ambao ni kampuni ya CANACO  ameshalipa fedha ya  ‘Survey’ ya miaka mitatu, na pia anawalipia leseni kwa kila mwaka na kwamba wao wanachokifanya ni kulipa  mrabaha ambayo ni mapato ya dhahabu inayopatikana.

“Leseni yetu iko hai, huwa tunamkumbusha tu kila muda ukifika na analipia na kututumia risiti. Sisi ni watoto wa Magambazi, ndio waanzilishi wa leseni ya viwanja ‘viinne’, awali watu 38 walianzisha uchimbaji na walikuwa wanakwenda vizuri.”