Home Latest News Kuna Serikali ya Magufuli na ya CCM

Kuna Serikali ya Magufuli na ya CCM

2035
0
SHARE

Rais John Magufuli (katikati) akiwa na Makamu wake, Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim MajaliwaELIAS MSUYA

WAKATI wa kampeni, Rais John Magufuli alitumia muda mwingi kueleza jinsi Serikali itakavyokuwa. Alikuwa akiita “Serikali ya Magufuli’.

Alisema Serikali ya Magufuli itaunda Mahakama ya mafisadi na wezi; itajenga barabara na ahadi nyingine lukuki.

Makada wengi wa CCM hawakumwelewa, walidhani itakuwa kama viongozi wenzake tu. Isitoshe wengi wao walikuwa wakiota vyeo tu. Baadhio ya wagombea ubunge walikuwa wanawaza tu kuwa mawaziri baada kushinda ubunge.

Wengine walikuwa wanaota nafasi ya Uwaziri Mkuu. Yaani kila mtu alikuwa na ndoto zake za kula maisha tu.

Kumbe Dk. Magufuli alikuwa anafikiria Serikali yake atakayoiongoza, tofauti na mtangulizi wake Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Sasa mwezi mmoja umepita Rais Magufuli akiwa madarakani, kila mtu anaona makeke yake. Hakuna cha Baraza la mawaziri wala nini. Alichofanya ni kuteua tu Waziri Mkuu. Kazi imeanza kwa kasi; leo amevamia Hazina, mara yuko bandarini, mara yuko TRA (Mamalaka ya Mapato) na taasisi nyingine.

Ndani ya mwezi mmoja Rais Magufuli ameshafanikiwa kuokoa zaidi ya Sh trilioni moja za kodi, huku akisimamisha kazi vigogo kadhaa.

Yaani kwa sasa idara za Serikali zimekuwa moto, watu wanatafutana, hakuna kulala. Hiyo ndiyo Serikali ya Magufuli.

Rais Magufuli ameondoa utawala ule wa chama dola. Tulishazoea kuona Rais ambaye pia anakuwa Mwenyekiti wa CCM anavyoendesha nchi. Wale viongozi na makadawa chama wanapata upendeleo kwenye sehemu nyeti kama vile idara za Serikali, wanapata tenda kwenye mashirika ya umma na mengineyo.

Sasa utaratibu huo haupo. Kwanza Dk. Magufuli mwenyewe hana hata mpango na CCM. Ni kweli atapewa uenyekiti wa taifa muda si mrefu, lakini inavyoonyesha kwake hicho siyo kipaumbele.

Kwa sasa hata wale makada walioshiriki bega bega kwenye kampeni zake wakitarajia kulipwa fadhila wameachwa solemba. Wengine hata matumaini ya kupata uwaziri yameyeyuka. Wengine walishazoea kusafiri usiku na mchana nje ya nchi, wengine walishajiwekea kampuni zao na marafiki zao, kazi ni kula tu.

Pale bandarini wakubwa walikuwa masilahi yao, walikuwa wanavuna fedha nyingi. Sasa Magufuli akawaingilia.

Utajiuliza, waliokuwa mawaziri wa Uchukuzi kabla ya uchaguzi, kina Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe waliweka utawala wao pale bandarini, kumbe hakuna lolote. Sasa Dk. Magufuli kaufumua wote.

Kule TRA amefumua, Tanesco nako amefumua, ilimradi kila mahali. Huo ndiyo ulikuwa utawala wa CCM tangu tupate uhuru. Mambo yalikuwa yakienda shaghalabaghala, utadhani ndani ya miaka 10 hatukuwa na rais nchi hii!

Sasa Serikali ya Magufuli imeingia madarakani. Haya yote tunayoyaona leo ni matokeo ya utawala mbovu wa CCM. Sisemi kwamba kwenye vyama vya upinzani hakuna ufisadi, la hasha. Ila nasema mfumo ambao Dk. Magufuli anashughulika nao uliundwa na chama chake.

Siyo bandarini tu wala TRA, ukifika kwenye viwanja vya ndege hali mbaya. Badala ya kuingiza mapato, vimekuwa ndiyo sehemu ya kupitishia dawa za kulevya. Yaani Tanzania ndiyo imekuwa kituo cha kupitishia dawa za kule Afrika Mashariki! Hivi nchi hii ilikuwa uongozi kweli?

Katika Wizara ya Maliasili na utalii ndiyo usiseme, kwani majangili yalikuwa yakitamba usiku na mchana. Tukabaki kutajiwa tu orodha ya majangili, mara wako 40, mara wako huko mara kule, lakini hawakamatwi!

Ikafika mahali mpaka wanyama pori wakapandishwa ndege na kuepelekwa nje ya nchi. Nchi hii iliyo na utawala wake, majeshi yake na ulinzi wa kila aina.

Yaani nchi ilikuwa imelala watu wanakula watakavyo. Sasa tunaona tofauti ya utawala ndani ya chama hicho hicho kimoja.

Naisema CCM kwa sababu ndiyo iko madarakani kwa muda wote wa uhuru kwa miaka 54 sasa. Hata kama kuna makada wa vyama vya upinzani waliiba hapa na pale, walipaswa kushughulikiwa na Serikali ya CCM.

Kuna mambo mengi ambayo Dk. Magufuli atayafanya na yataiweka uchi CCM kwa waliyokuwa wakiyafanya miaka ya nyuma bila aibu.

Hata kule bungeni, kuna wabunge wa CCM waliozoea kujipendekeza kwa chama chao hata kama hawana hoja za msingi. Safari hii inabidi wajipange kweli kweli kwa sababu rais mwenyewe hatabiriki.

Siyo wabunge tu wa CCM, hata wale makada wa chama hicho waliozoea kujikombakomba ili wapewe vyeo vya ukuu wa wilaya na mikoa itabidi wajipange upya, kwani kwa sasa mambo yamebadilika.

Yaani nchi ilikuwa imefikishwa pabaya kwa sababu ya ubabaishaji tu. Jiji la Dar es Salaam pekee kama lingesimamiwa vizuri lingeweza kuongeza pato la Serikali mara dufu.

Rasilimali zilizopo nchini kama zitasimamiwa vizuri, zinaweza kabisa kuiondoa nchi yetu kwenye lindi la umasikini.

Tunahitaji mtu atakayevunja mwiko wa kubebana ndani ya chama kama anavyofanya sasa Rais Magufuli. Hakuna kuangalia sura ya mtu, ila ni kuhakikisha masilahi yote ya nchi.

Hapo ndipo tunapoona tofauti kati ya Serikali ya CCM na Serikali ya Magufuli.