Home Makala Kuna sinema ndani ya siasa za upinzani

Kuna sinema ndani ya siasa za upinzani

2235
0
SHARE

MUDHIHIR MUDHIHIR

Sinema ni maigizo yenye kusudi la kuwasilisha jambo au hali iliyowahi kutokea au hali iliyopo. Ili kuwavutia watazamaji, watunzi wa sinema mara nyingi hukoleza chumvi katika maudhui kwa kubuni uongo usiyofikirika. Hata hivyo ndani ya sinema kila uongo huwa ni jaribio tu la kuficha ukweli, na kila upuuzi husheheni dhamira isiyopaswa kupuuzwa. 

Katika baadhi ya vituko vya kisiasa hapa Tanzania, hutokea kwa mtu makini akatamani kuufananisha upinzani wetu wa kisiasa na viroja vya kwenye sinema. Unamuona mhusika kwenye sinema anauhiari umasikini na hata kifo kwa ajili ya kupigania haki na uhuru. Halafu unamkuta mhusika huyo huyo nje ya sinema ni kichekesho cha mtaa kwa sababu ya kurambishwa asali na maziwa.

Hivyo vyama vya siasa ndani ya kambi ya upinzani hapa Tanzania vina agenda ya Watanzania au ni agenda za vikundi vidogo vya wanasiasa wanaoweza kuhesabika kwa vidole? Wengi wetu tulitaraji kuwa na wapinzani wa kutuangazia gizani ili tuione njia ya huko wanakotaka kutupeleka. Badala yake wao ndiyo wanaotaka mwanga ili tuwaone. Hizi ni siasa za kujianika, kulialia na kuomba huruma. 

Kwa nini vinara wa upinzani walalame ndani na nje ya Tanzania kuwa wanazuiwa kufanya mikutano ya hadhara? Kwa nini wasifanye mikutano hiyo katika Majimbo ambayo wana Wabunge, au katika Kata ambazo wana Madiwani, na katika Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambamo wana Wenyeviti? Mikutano ya hadhara ni lazima ifanyike katika viwanja vya Jangwani, Mwembeyanga, Ilulu, Nangwanda, Kirumba na Sheikh Amri Abeid?

Wapigakura waliyochagua upinzani katika majimbo, kata, mitaa, vijiji na vitongoji wanayo kiu ya kuwaona na kuwasikiliza wawakilishi wao. Viongozi waliyochaguliwa nao wanao wajibu wa kuwatembelea wapigakura wao, lakini hawafanyi hivyo japo hawazuiliwi na mamlaka yoyote. Vilio vya kuminywa demokrasia tunavyovisikia humu nchini na nje ya nchi yetu vina dhamira gani?

Chama cha siasa si mtu au kikundi cha watu bali ni watu. Hata chama cha walevi au cha wachawi nguvu yake ni wanachama wake. Mwaka 1995, NCCR Mageuzi chama ambacho kilikuwa ni tishio kwa CCM kilimpa utukufu aliyeshindikana CCM kikapigwa chini. Mwaka 2015, CHADEMA wakamsafisha kwa madodoki waliyemchafua kwa ufisadi akiwa CCM nacho kikala mweleka. Anayejipiga kofi hapaswi kulia.

Umadhubuti wa chama cha siasa katika siasa za ushindani unapatikana katika maeneo makuu matano. Panahitajika Ilani ambayo haina budi kujikita katika mahitaji muhimu ya wananchi na mahitaji ya ustawi wa taifa kwa ujumla wake. Chama kinacholenga kuchafua washindani wake badala ya kuweka mkazo katika kuonyesha mwelekeo wake hakinusuriki kupigwa mweleka. Ndani ya upinzani hapa kwetu Ilani yenye umakini ni ya kutafutwa. 

Bila ya shaka tunakumbuka yaliyojiri katika sinema ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995. Chama ambacho kulikuwa na umaarufu mkubwa na wasomi wenye majina ya kutajika kilihamishwa kutoka katika Ilani yake na kutekwa na vuguvugu la CHAVDA.  Vuguvugu hili likavuruga mwelekeo wa chama hiki kuanzia ukumbi wa mdahalo pale Kilimanjaro Hotel na hadi katika viwanja vya kampeni. 

Ilani makini ikaiokoa CCM  kupitia tundu la sindano katika uchaguzi wa mwaka 2015. Chama kingine ambacho kilijijengea umaarufu mkubwa na kuwa tishio kwa CCM ikaachana na habari ya Ilani yake kikakumbatia kikundi cha watu wenye majina makubwa. Hawakutambua mapema kuwa vigogo hawa walishapoteza haiba ya kisiasa. Ilikuwa sinema ya mwanakondoo kubatizwa na papo kutawazwa uaskofu.

Kampeni za vyama vya siasa katika kambi ya upinzani zilipambwa kwa dhamira ya kuleta mabadiliko. Lakini vinara wa kambi ya upinzani hawakutanabahi kwamba walikuwa wanacheza sinema. Walikuwa wanaimba mabadiliko ambayo hawayaishi. Wenzao wa CCM walikuwa na manju mpya, mashairi mapya na vina vipya. Yalikuwa mabadiliko halisi. Wao walikuwa ni wale wale, katika yale yale na kwa namna ile ile.

Chaguzi zikishakamilika vyama vya siasa vina wajibu muhimu wa kufanya tathimini. Lazima waweke kwenye mizani nguvu na udhaifu wao; na nguvu na udhaifu wa wenzao. Bila ya kujitathimini chama cha siasa kitakuwa kinajijengea mazingira ya kupunguza nguvu zake na kuzidisha udhaifu wake. Hali hii ndiyo tunayoiona katika vyama vingi ndani ya upinzani hapa Tanzania. Madai ya hujuma kwa hakika ni sinema. 

Kujitathimini ni pamoja na chama kujiuliza iwapo Ilani yake ilikuwa na mvuto mbele ya wapigakura. Chama hakina budi kujiuliza iwapo wagombea wake walikuwa wanauzika kwa misingi ya haiba zao kisiasa na uwezo wao katika kukabili mikikimikiki ya siasa za ushindani. Na kujitathimini kunahitaji pia kuitazama nguvu ya chama kwa mnasaba wa umoja miongoni mwa wanachama. 

Upo msemo wa Kiarabu usemao kwamba kinachojengwa kwa misingi ya batili hicho ni batili. Tumepata kusikia mara kadha wa kadha baadhi ya vinara wa upinzani wakilalama kuwa “ukanda wetu huu haujawahi kutoa Rais”. Na katika uchaguzi wa mwaka 2015 mgombea mmoja wa Urais alisikika akiwalilia waumini ndani ya kanisa kuwa dhehebu lao halijawahi kutoa Rais. Hii ni sinema. 

Hapana ubishi kuwa ndani ya kambi ya upinzani hapa Tanzania, vipo vyama vya siasa ambavyo misingi ya kuasisiwa kwao imebeba chembechembe za ukanda, ukabila, udini na hata ufamilia. Nyakati nyingine wanaoitwa wasomi huibuka ndani ya vyama vya siasa wakateka majukwaa na kuanza kumwaga mihadhara (lectures) kama wamo darasani bila ya kwanza kutambua, mahitaji yetu sisi hadhira yao. Hivi navyo ni viroja vya sinema. 

Wanasiasa makini na madhubuti hawana budi kuyazingatia tuliyoyajadili hapo juu ikiwa wanahitaji kujenga chama imara kitakachokubalika maeneo yote ya nchi. Wanasiasa wa upinzani wasiendekeze vigezo vinavyobeba vikundi vikundi vidogo vya jamii kama vile ukanda, ukabila, ujimbo, ufamilia na kigonjwa cha usomi. Hamuwezi kubagua watu kama mafungu ya nyanya au mkabeza watu kwa sababu ya usomi wenu halafu mkatarajia kushinda uchaguzi na kukamata dola. Hata kidogo.

Uchaguzi ukikamilika chama cha siasa huwa na wajibu wa kulinda kura zake zilizopatikana wakati wa uchaguzi haidhuru kama zilitosha kuleta ushindi au kinyume chake. Ofisi ya chama cha siasa hasa matawini ni lazima iwe wazi na viongozi wake wasiwe adimu na aghali kupatikana. Chama cha siasa cha upinzani hakiimarishwi kwa kulalamikia hujuma za chama kilichoshinda uchaguzi, au kwa maneno ya kejeli, na kuhamasisha chuki na ghasia.

Lengo la kipaumbele kwa chama chochote cha siasa duniani ni kushinda uchaguzi na kukamata hatamu za dola. Dhamira ya wanasiasa shuruti ilenge katika kuwaendeleza wananchi kiuchumi na kuhakikisha kuwa huduma muhimu za kijamii zinapatikana na kuboreshwa, na miundombinu ya kuchochea uchumi na ustawi wa taifa inajengwa. Haya yanawezekana iwapo amani itatamalaki nchini, na taifa likiwa na sifa ya kupendeza na kuvutia kimataifa.

Mwanasiasa anayezurula duniani kuichafua nchi yake hastahili kujinasibu kuwa eti anawapenda wananchi wake. Mwanasiasa anayezurula duniani kuzuia misaada ya kibinadamu, kuwajaza hofu watalii na wawekezaji, ni maigizo ya sinema kutudanganya kuwa anafanya hayo kwa maslahi ya nchi yake na ya wananchi wenzake. Haya hayawezi kuwa ni mawazo ya chama cha siasa, mawazo ya wanachama au kuwa ni mawazo ya Watanzania. Ni sinema ya ovyo kabisa.

Watanzania tunahitaji maendeleo katika sekta ya uzalishaji mali, sekta ya miundombinu na huduma za kiuchumi, sekta ya huduma za jamii, na jitihada katika uwezeshaji wananchi kiuchumi. Chama chenye malengo haya kitawekwa madarakani. Uhodari wa kulichafua taifa, kuwabeza viongozi, kuhamasisha chuki na ghasia ni sinema ambazo hazipendezi, hazina mashiko na hazina soko.

Tanzania ni nchi yetu. Hatuna budi kuienzi, kuitangaza kwa uzuri na kuilinda kwa huba na wivu mkubwa.