Home Habari Kuoa msichana chini ya miaka 18 marufuku

Kuoa msichana chini ya miaka 18 marufuku

1024
0
SHARE

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania imekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba, vipengele vya sheria vinavyoruhusu mtoto wa kike wa miaka chini ya miaka 18 kuolewa ni batili, Serikali ifanye mabadiliko

Mahakama imetamka kwamba, kifungu cha 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Serikali ifuate maelekezo ya Mahakama Kuu kubadilisha vifungu hivyo, ili umri wa ndoa uanzie miaka 18.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulisomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Edie Fussi, baada ya jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Winfrida Korosso na Dk. Mary Lavira kusikiliza rufaa hiyo.

Jopo hilo kwa pamoja lilikubaliana kwamba Mahakama Kuu haikukosea katika uamuzi wake uliotolewa mwaka 2016, na kusema kwamba watoto wote ni sawa bila kujali jinsia.

Serikali ilikata rufaa dhidi ya Mwanaharakati wa Haki za Binadamu na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto wa kike kusoma, Rebeca Gyumi.

Jopo lilisema kwamba sheria haiwezi kumkinga mtoto wa kike kwa kuruhusu aolewe chini ya miaka 18 kwa madai kwamba huko kuna ulinzi zaidi, wakati kuna madhara ikiwamo mimba za utotoni, magonjwa na unyanyasaji wa kijinsia.

“Sheria mbalimbali zinamkataza mtoto chini ya miaka 18 kuingia mikataba mbalimbali, hawezi kuingia mikataba mingine, basi hata huu mkataba wa ndoa hawezi kuingia ni mgumu zaidi.

“Kifungu cha 13 na 17 vya Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Serikali ifuate maelekezo ya Mahakama Kuu kubadilisha vifungu hivyo,” lilisema jopo hilo katika uamuzi wake.

Mahakama Kuu ilibatilisha watoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18, na kuamuru Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili umri wa ndoa uanzie miaka 18.

Upande wa Serikali ulikata rufaa na kuwasilisha sababu mbalimbali Julai, 2019 wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Miongoni mwa sababu za  kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha ndoa inayofungwa na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18, Serikali inadai kuwa lengo ni kuwalinda watoto dhidi ya ngono na kupata watoto nje ya ndoa.

Akizungumzia uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema ni mapema mno kutoa maoni.

“Unajua suala hilo linagusa imani za watu, kwa hiyo ni mapema mno kuzungumzia suala hilo, nadhani tupeane muda mpaka tukutane na Mufti (Sheikh Mkuu), kisha tutazungumza,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Programu ya Harakati na Ujenzi wa Nguvu ya Pamoja kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai, alisema ni jambo ambalo wamelipigania kwa muda mrefu, kwa sababu lilikuwa linakinzana na sheria na miongozo mingine ikiwamo Sheria ya Mtoto.