Home Latest News Kupwaya kwa demokrasia kutaigharimu Afrika baada ya Covid-19

Kupwaya kwa demokrasia kutaigharimu Afrika baada ya Covid-19

297
0
SHARE

NA FREDERICK FUSSI

DEMOKRASIA ni utaratibu au mfumo wa kuipanga dunia kiutawala ili iwe sehemu salama ya kuishi. Utaratibu huo unaelekeza walio wengi kuchagua wachache ili wawe watawala na viongozi wa wengi katika uongozi na utawala angalau kwenye kila Taifa duniani. 

Mfumo huu hauwezi kuwa bora kwa asilimia 100 ndio maana ni mfumo wenye mafanikio kwenye nchi fulani fulani na ni mfumo uliofeli au wenye mapungufu kwenye nchi nyingine hasa Afrika. Kila matatizo makubwa yanapoikumba dunia, hitimisho lake mara nyingi imekuwa ni kuipanga upya dunia katika utaratibu au mfumo mpya wa maisha. 

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, iliyopiganwa kwa takribani miaka minne mfululizo tangu Julai 28 mwaka 1914 hadi Novemba 11 mwaka 1918, vita ili hitimisho lake lilizalisha ‘Jumuiya ya Mataifa’ yaani ‘The League of Nations’. Lengo kuu la Jumuiya ya Mataifa ilikuwa ni kuupanga upya ulimwengu kiutawala ili usirudie makosa yaliyosababisha kuibuka kwa Vita ya Kwanza ya Dunia. 

Nini sasa kilipelekea ulimwengu kupangwa upya kufuatia matokeo ya vita ya kwanza ya dunia? Inakadiriwa zaidi ya askari milioni tisa walipoteza maisha wakati raia zaidi ya milioni 21 walipata majeraha. Uchumi wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele kwenye vita kama vile Ujerumani, Urusi, Uingereza na mataifa mengine ya bara la Ulaya ulidorora. 

Sasa basi Jumuiya ya Mataifa ikalazimika kuundwa na mawazo yaliyotolewa na Rais Woodrow Wilson wa Marekani huku akitoa hoja 14 za kwanini Jumuiya ya Mataifa iundwe, lengo ikiwa ni kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa vita mpya kwa njia za mazungumzo ya amani. 

Ikumbukwe kuwa Marekani haikuwa mstari wa mbele kivile katika vita hii, wao walikuwa wanashughulika na biashara ya Kimataifa na kusafirisha bidhaa mbalimbali miongoni mwa makundi hasimu yote yaliyopigana vita, hivyo uchumi wao uliendelea kuimarika katika muda wote wa vita kwa sababu pia vita haikupiganwa ndani ya ardhi yao. 

Usipokuwa mstari wa mbele kwenye vita unapata nguvu za kuimarisha uchumi wako na hatimaye unaibuka Taifa lenye nguvu sana baada ya vita kuisha. Hii ndio ilikuwa nafuu kwa Marekani kuelekea kwenye ukuu wa ulimwengu kiuchumi na kijeshi.

Embu jaribu kuwaza, wakati kitovu cha vita ya kwanza ya dunia kilikuwa ni mataifa ya Ulaya Kusini Mashariki kule Austria-Hungary, kitovu cha ugonjwa wa homa ya mapafu ‘Covid-19’ kilikuwa jiji la Wuhan China Disemba 1 mwaka 2019 alipotangazwa mgonjwa wa kwanza. Wakati maambuzi ya Covid-19 yakidhibitiwa kwenye kitovu cha mlipuko nchini China, wakati huo huo maambukizi yameshika kasi nchini Marekani na ndio Taifa linaloongoza kwa vifo na idadi ya watu walioambukizwa. Kwa hiyo China ipo ‘busy’ kushughulikia ukuaji wa uchumi wake wakati huo Marekani inapigania vita ya virusi vya Covid-19 huku karibuni sekta zote za uchumi na uzalishaji zikiwa chini ya kifungo yaani “Lockdown”. Embu jaribu kuwaza ni kitu gani kipya kitazaliwa baada ya vita ya ugonjwa wa Covid-19 kuisha ili kiweze kuupanga upya ulimwengu? Embu tuendelee kuangalia nini kilizaliwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama pa watu kuishi mfumo wa utawala wa nchi nyingi duniani uliathiriwa na Sera na Mipango ya ‘Jumuiya ya Mataifa’ hasa kuchochea mawazo ya kuwa na Serikali ziongozwe kwa misingi ya wengi wape yaani ‘demokrasia’ kama njia ya kuifanya dunia na mataifa mbalimbali yatulie.

Cheche za Vita ya Kwanza ya Dunia zilitokana na masuala ya utawala, kadhalika cheche zilizochochea Vita Kuu ya Pili ya Dunia zilitokana na sababu za utawala. Haijathibitika bado endapo ‘mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu Covid-19’ ulitokana na sababu ya China kutafuta ushawishi wa kiutawala ili kusambaza falsafa yake ya utawala yaani ‘Meritocracy’ katika mataifa mbalimbali duniani ama lah. 

Mauaji ya aliyekuwa Mrithi wa Austria-Hungary Franz Ferdinand pale alipouawa yeye pamoja na mkewe Sophia na mauaji hayo kutekelezwa na aliyekuwa Mhafidhina wa nchi ya Serbia Gavrilo Princip Juni 28 mwaka 1914 ndio sababu hasa zilizopelekea cheche kuibua mfululizo wa matukio yaliyochochea mapigano makali ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambayo baada ya kumalizika ilizaa ‘Umoja wa Mataifa’ (United Nations) ili kuendeleza sababu zilizile za kuupanga ulimwengu kama ilivyokuwa kwa iliyokuwa ‘Jumuiya ya Mataifa’ (league of Nations). Sababu za cheche za Vita ya Pili ya Dunia nazo ni za kiutawala, kwa sababu inaaminika vita hii ilianza Septemba 1 mwaka 1939 pale ambapo nchi ya Ujerumani wakati huo ikiongozwa na kiongozi aliyekuwa na ndoto ya kuitawala dunia Adolf Hitler alipoivamia nchi ya Poland. 

Ndipo washirika wa Poland, yaani Uingereza na Ufaransa wakatangaza vita na Ujerumani kama sehemu ya kumtetea mshirika mwenza Poland asinyanyaswe na matamanio ya kiutawala ya Ujerumani ya Hilter. Inasadikiwa pia vita hii ilichochewa na kitendo cha Japan kutaka kutawala ukanda wa Bahari ya Pacific na eneo lote la bara la Asia kwa kuanza kuvamia eneo la Manchuria lilikokuwa chini ya utawala wa nchi ya China mnamo Septemba 19 mwaka 1931. 

Vita sasa ikawa baina ya pande mbili pinzani, Ujerumani, Italia na Japan kwa upande mmoja, ambao mwishoni mwa vita waliangukia pua dhidi ya ushindi wa ushirika wa Urusi, Marekani, China na Uingereza. Hii ndio ilikuwa vita iliyokuwa na mauaji makuu takribani watu zaidi ya milioni 73 wanakadiriwa kupoteza maisha. 

Kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945 kuliibua “Umoja wa Mataifa” ambapo washindi wa vita ile Urusi, Marekani, China Uingereza pamoja na Ufaransa wakajipachika cheo cha ukuu wa ulimwengu na wao wakawa ndio wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mpaka leo. 

Hawa wakuu wa ulimwengu ndio wanaamua utawala wa ulimwengu uendeshweje. Je mapambano ya vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 yatawaibua mataifa yepi kuwa washindi na hatimaye wawe wakuu wa ulimwengu na kuwaamulia Mataifa mengine jinsi ya kuendesha shughuli zao za utawala? Je Demokrasia itaendelea kuwa ndio mfumo wa ulimwengu kupangwa na kujiendesha? Au tutarajie aina mpya ya mfumo kutoka kwa mshindi wa vita ya Covid-19?

Umoja wa Mataifa unashikilia ajenda za haki za binadamu pia ndio mwanzilishi wa Malengo Endelevu ya Milenia (MDGs) na sasa yanaitwa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs). Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanatakiwa kujiendesha kwa misingi ya kidemokrasia ili waendelee kula raha za matunda ya Umoja wa Mataifa kama vile kupewa mikopo na ruzuku kupitia vyombo vya fedha vya kimataifa kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). 

Fuatilia sehemu ya pili ya makala haya kwenye Safu hii Alhamisi ijayo.