Home KIMATAIFA Kurejea kwa Bemba DRC mwanzo mpya wa harakati

Kurejea kwa Bemba DRC mwanzo mpya wa harakati

887
0
SHARE

ASHA BANI NA MTANDAO

MWANASIASA maarufu wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo – DRC, Jean-Pierre Bemba amerejea rasmi nyumbani baada ya kukaa miezi kumi ugenini.

Bemba alirudi DRC hapo wiki hii kutoka Brussels nchini Ubelgiji kwa kutumia ndege binafsi na kupokewa na umati wa watu waliokusanyika katika Jiji la Kinshasa ambao walimlaki.

Washirika wake Bemba, wanasema amerudi rasmi DRC kumsaidia mpinzani Martin Fayulu ambaye anasisitiza kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Ni ziara ya pili ya mwanasisia huyo nchini DRC baada ya kuachiliwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya kutumikia kifungo cha miaka kumi gerezani.

Kwa mujibu wa BBC, Bemba alihutubia kwa mara ya kwanza umati wa watu uliokusanyika na kuwaeleza kile ambacho upinzani unadai ndio ukweli kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu huo.

“Mahakama ya Katiba inapaswa kuimarisha demokrasi nchini mwetu, badala yake imekuwa kama saratani inayoharibu taasisi zetu. Mmeona jinsi Bunge letu limekuwa na watu ambao hawakuchaguliwa ndio wamelitawala… hiyo inachafua jina la nchi yetu ugenini. Sio viongozi tu walio na haki ya kujenga nyumba,” anasema Bemba wakati akizungumza na wananchi.

Kwa sasa Bemba amepanga kubaki nchini kwake DRC kwa muda mrefu kama njia na mkakati wa kuongoza mfululizo wa maandamano aliyopanga kwa lengo la kudai haki ya uchaguzi huo.

Bemba alirudi DRC kuonesha azma ya kutaka kugombea katika uchaguzi wa mwaka jana, lakini ombi lake lilitupiliwa mbali na Tume Huru ya Uchaguzi.

Alirudi Ubelgiji na kutangaza kuungana na Moise Katumbi, mgombea mwingine wa upinzani, pamoja na Fayulu kupitia muungano wa Lamuka.

Umati uliokusanyika safari hii haukuwa mkubwa ikilinganishwa na uliokuwepo wakati Bemba aliporudi DRC kwa mara ya kwanza kutoka uhamishoni Agosti mwaka jana baada ya kuishi kwa zaidi ya muongo mmoja nje ya nchi hiyo.

Kiongozi mwenza wa upinzani, Moise Katumbi alirudi kutoka uhamishoni mwezi mmoja uliopita.

Bemba aligombea urais dhidi ya Rais Joseph Kabila mwaka 2006 na alishindwa.

Alikaa kwa miaka 10 katika Mahakama ya ICC ambako alishtakiwa kwa uhalifu uliotekelezwa na wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kabla ya kuondolewa mashtaka na hatimaye kuachiwa huru baada ya kukata rufaa.

Wakati Bemba anarudi DRC, Rais Felix Tshisekedi ameingia katika makubaliano ya Serikali ya Muungano na kiongozi aliyemtangulia Joseph Kabila, ambaye ana idadi kubwa ya wawakilishi bungeni.

JEAN-PIERRE BEMBA NI NANI?

Bemba alizaliwa mwaka 1962 katika Mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Equateur. Baba yake, bilionea Bemba Saolona alikuwa rafiki wa karibu wa Mobutu Sese Seko.

Ni baba wa watoto watano, amemuoa binti wa Mobutu na kusababisha kupewa jina ‘Mobutu Mdogo’ kwa sababu ya uhusiano wake wa karibu na kiongozi huyo wa zamani wa taifa hilo lenye utajiri wa madini Afrika.

Novemba 1998, Bemba alibuni kundi la waasi – MLC katika mkoa wake wa nyumbani wa Equateur.

Vikosi vyake baadaye vilihusika katika mzozo kati ya mwaka 2002 na 2003 nchi jirani ya DRC, vikipagana kwa ushirikiano na vikosi vilivyokuwa watiifu kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ange-Felix Patasse, ambaye alikuwa akipingwa na aliyekuwa mkuu wake wa majeshi wakati huo, Francois Bozize.

Agosti 1999, MLC ilisaini mkataba wa amani wa Lusaka ambao ulinuia kufikisha kikomo mapigano nchini DRC.

Aligeuza MLC kutoka kundi la waasi na kuwa chama cha kisiasa baada ya kusainiwa makubaliano ya amani ya mwaka 2002.

Bemba alihudumu kama mmoja wa makamu wanne wa Rais wa DRC kwenye Serikali ya umoja kati ya mwaka 2003 na 2006.

Kama mgombea mkuu wa chama chake, aliwania urais mwaka 2006, lakini akashindwa na Kabila kwenye marudio.

Mwaka 2007, mapigano kati ya wapiganaji watiifu kwake na jeshi yalizuka mjini Kinshasa na kusababisha vifo vya takriban watu 100.

Bemba alikimbilia nchini Afrika Kusini akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Baadaye alikimbilia uhamishoni na familia yake.

KUKAMATWA KWAKE

Mei 2008 alikamatwa na mahakama ya ICC mjini Brussels, Ubelgiji kujibu mashtaka ya uhalifu uliotendwa na vikosi vyake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama ya ICC imemwondolea Bemba makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ambayo alikuwa amepatikana nayo.

Alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kutokana na makosa hayo.

Bemba alipatikana na hatia Machi mwaka 2016 kwa makosa ya uhalifu, uliotokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kati ya mwaka 2002 na 2003 na akahukumiwa Juni 21.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo kutokana na rufaa aliyoiwasilisha kupinga hukumu hiyo.

Alilaumiwa kwa kushindwa kuwazuia waasi wake wasiwaue na kuwabaka watu.

Jaji Christine Van den Wijngaert pia amesema majaji waliomhukumu mwaka 2016 walikosa kuzingatia juhudi zake za kujaribu kuzuia uhalifu huo punde baada ya kufahamishwa kwamba makosa hayo yalikuwa yakitokea.

Kesi hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa ICC kuangazia ubakaji kama silaha wakati wa vita.

Aidha, ilikuwa mara ya kwanza kwa mshtakiwa kuhukumiwa kwa makosa yaliyotekelezwa na watu wengine waliokuwa chini ya mamlaka yake. Juni 8, mwaka jana aliachiwa huru.