Home Latest News KUSHAMIRI MIGOGORO Ni dalili za vita vya tatu vya dunia?

KUSHAMIRI MIGOGORO Ni dalili za vita vya tatu vya dunia?

2288
0
SHARE
Adolf Hitler

NA IGAMANYWA LAITON,

NI miaka 102 sasa imepita tangu kijana mdogo wa Kiserbia alipofanya kitendo ambacho laiti angejua madhara yake asingethubutu kufanya. Kama vile baruti inavyoweza kulipua miamba mikubwa ndivyo kitendo chake cha kufyatua risasi mbili kilivyoyaletea mataifa makubwa ya kipindi hicho katika kile kilichoitwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Katika makala haya tutaangazia ni jinsi gani, ilitokeaje na je, inaweza kutokea tena leo?

Hebu tujaribu kuangalia mambo yalivyokuwa, Juni 28, 1914 saa 5:15 nchini Serbia mambo yalikuwa si shwari shamra shamra za kumpokea mtawala wa Austarilia ya Hungary, Francis Ferdinand, mtawala huyo alikuwa akiitembelea Serbia taifa lililokuwa chini ya mamlaka yake kama koloni, bila kujua kuwa alikuwa akijipeleka katika kifo.

Ikumbukwe kuwa kufika mwaka 1914 uhasama kati ya mataifa yenye nguvu ya Ulaya ulisababisha wasiwasi na kutoaminiana katikati ya mataifa hayo makubwa wakati huo na hatimaye kutokea kwa kambi mbili za upinzani zenye nguvu, yaani miungano miwili mikubwa iliyopingana kati ya Shirikisho la nchi tatu lililokuwa likiundwa na nchi kama Australia ya Hungary, Italia na Ujerumani huku upande wa pili uliokuwa ukifahamika kama Maelewano ya nchi tatu yakiundwa na nchi za Uingereza, Ufaransa na Urusi.

Nchi hizi zote sita zilikuwa na uhusiano wa kisiasa na kiuchumi pamoja na nchi nyingine ndogo ndogo kupitia ndani ya eneo la Balkani eneo lililokuwa likiundwa na nchi kama Serbia, Bosnia (ambayo sasa ni sehemu ya Bosnia na Herzegovina , Kosovo, Monternego, Slovenia ya Croatia na Albania).

Eneo hili lote lilikuwa chini ya utawala wa mataifa yale sita makubwa ya Ulaya Magharibi, utawala huu uliokuwa umeleta msukosuko mkubwa wa kisiasa na hali za hatari huku vuguvugu za kudai uhuru kamili wa kujitawala ukienea katika eneo lote la Balkani.

Hilo ni kama tu makoloni mengine yalivyokuwa yakipingana na utawala wa kimabavu wa nchi zilizokuwa zikizitawala, huku vyama, makundi na taasisi nyingi za siri zenye malengo ya kudai na kupigania uhuru kwa namna yoyote zikiwa zimetapakaa.
Ganvirol Princip kijana mzalendo wa Serbia na wenzake wakiwa katika kikundi, walikuwa wamepanga njama ya kumuua Ferdinand wakati wa ziara yake katika mji wa Sarajevo mji mkuu wa Bosnia.

Kumbuka kuwa Austria na Hungary ilikuwa ni nchi iliyokuwa na mfungamano na nchi za Italia, Ujerumani wakiunda shirikisho la Nchi Tatu huku Bosnia ikiwa chini ya Austria-Hungary.

Hivyo kwa Princip na wenzake kumuua kiongozi mkuu wa Australia ya Hungary ingeonekana kitendo cha kishujaa na cha kizalendo kwa namna moja au nyingine kingeweza kuchochea vuguvugu la wao kudai uhuru wa nchi yao-Serbia.
Juni 28, 1914 wakati Ferdinand akiwa amefika Sarajevo na kutembezwa katika viunga vya mji huo kijana mmoja mshirika na kikundi cha Princip akatupa bomu dogo katikati ya msafara huo, lakini kwa kuwa hakuwa na uzoefu wa kulenga shabaha akakosea hivyo mpango wao wa kutaka kumuua Ferdinand haukufanikiwa.

Wakati huo teknolojia, ufanisi na hali za kiusalama za nchi nyingi duniani zilikuwa hafifu na zisizo na uwezo wa hali ya juu ukilinganisha na kipindi cha sasa, hivyo ilikuwa rahisi kwa wale vijana kujipenyeza katikati mwa msafara na kutupa bomu.

Baada ya bomu lile kushindwa kumuua Ferdinand, akiwa na bastola ndogo Princip alijaribu kulikaribia gari ili afyatue risasi lakini naye akaambulia patupu, akiwa amekata tamaa akavuka barabara na kwenda katika mgahawa mmoja uliokuwa karibu ili kutafakari.

Ferdinand alikasirishwa na tukio lile na kumwamuru dereva wake ageuze gari, bila kutambua akawa anaelekea uelekeo ulipokuwa ule mgahawa aliokuwa amekaa Princip aliyekuwa kafura kwa hasira baada ya kutofanikiwa kwa jaribio lake.

Wakati gari  lenye muundo wa T-ford la Ferdinand likipaki karibu na mgahawa, Princip alitoka nje na kufyatua risasi mbili na kumuua Ferdinand na mke wake Sophia.

Princip na wenzake walifungwa kifungo cha maisha katika gereza lililokuwa katika ngome iitwayo Teheresienstadt inayopatikana katikati ya majiji ya Dresden na Prague huko ulaya ya kati (waliepuka adhabu ya kunyongwa kwa kuwa walikuwa bado hawajafikisha miaka 20).

Princip alifia humo wakati vita ikiendelea.
Ukawa ni mwanzo wa mambo kuchacha, uchunguzi rasmi haukupata wa uthibitisho uliohusisha serikali ya Serbia katika mauaji ya Ferdinand lakini Hungary ilikuwa imeazimia kukomesha uasi wa wanaharakati wa nchi za Balkani ili kujaribu kutuliza hali.

Nicholaus Hartwing aliyekuwa balozi wa Urusi katika nchi ya Serbia alijaribu kutaka pande hizo mbili zikubaliane, lakini alifariki muda mfupi kabla ya kukutana na wajumbe kutoka Australia ya Hungary ili kutuliza mambo yaliyokuwa yameanza kuharibika.

Kufika Julai 23, Austria- Hungary iliitumia Serbia orodha ya matakwa waliyopaswa kutimiza na Serbia ikakataa kutimiza baadhi, uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukakoma.
Julai 28, kiongozi wa Austaria ya Hungary akiwa amehakikishiwa kwamba Ujerumani itamuunga mkono akatangaza vita dhidi ya Serbia.

Urusi ilikuwa ikiunga mkono Serbia na hivyo ikajaribu kuitisha Australia ya Hungary kwa kutuma wanajeshi takribani milioni moja mpakani na Australia ya Hungary, mambo yakazidi kuchachamaa. Julai 31 Ujerumani ikatangaza vita dhidi ya Urusi na siku mbili baadaye ikatangaza vita dhidi ya Ufaransa.

Kwa sababu mipango ya vita ya Ujerumani ilihusisha kupitia Ubelgiji, Uingereza ikaionya Ujerumani kwamba itatangaza vita dhidi yake kama ingewaingiza Wabelgiji kwa namna yoyote katika vita hivyo. Majeshi ya Ujerumani yakaingia Ubelgiji Agosti 4, vita vikachachamaa na Uingereza ikatangaza vita dhidi ya Ujerumani.
Wakati matukio hayo yakishika kasi kuna baadhi ya mambo yaliyokuwa yakichochea moto wa vita baina ya mahasimu wawili wa yale makundi mawili yaani Shirikisho la nchi tatu na maelewano ya nchi tatu.

Kabla ya mwaka 1914 watu wengi huko ulaya walikuwa wakitukuza na kupenda vita walikuwa wakiona kuwa vita ni kitu chenye faida na chenye kuheshimiwa na baadhi ya viongozi walifikiri kwamba vita vingefanya nchi zao ziwe na umoja na kuwachochea watu waungane.

Pia matangazo ya viongozi wa majeshi, makamanda na majenerali yalikuwa yamewahakikishia na kuwapa kiburi na kujiamini kwa kila nchi kuwa lazima wangeshinda vita, kila upande uliamini ungeshinda vita na kuuona upande mwingine dhaifu, hakuna aliyetarajia kuwa vita ile ingechukua miaka mingi kumalizika.
Isitoshe katika miaka hiyo kulikuwa na msisimko mkubwa sana wa uzalendo uliokuwa ukienea katika shule, vyuo vikuu, vyombo vya habari na wanasiasa walihamasisha watu wawe wazalendo na kujitukuza.
Pia miungano ya Ulaya ambayo ilikusudiwa kulinda watu dhidi ya vita nayo ilichangia kwa kuwa serikali kubwa za Ulaya zilitegemeana ili kupata ulinzi kila serikali ilihisi kwamba usalama wake ulitegemea serikali nyingine za muungano na hivyo ilihisi inapaswa kuitetea serikali hizo hata kama ilimaanisha kuwa serikali hizo ndizo zilizowachokoza maadui.

HALI BAADA YA VITA
Kitabu kimoja cha kihistoria kilimnukuu mwanajeshi mmoja mstaafu aliyeshiriki katika vita hiyo na akisema; “Vita hivyo….viliathiri fikra na tabia za kizazi kizima, maadili yakaporomoka, utu ukapotoka na udugu wa binadamu wote ukasinyaa, miliki nzima nzima zikatoweka vita hivyo vilivyosababisha maafa makubwa, vilikuwa mwanzo tu wa karne nyingi zenye umwagaji damu katika historia ya mwanadamu, mapinduzi na maandamano yakawa mambo ya kawaida, watu milioni 10 hivi walikufa na milioni 20 wakawa walemavu kwa muda wa miaka minne tu”.

Vita vya kwanza vya dunia viliisha Novemba 11, 1918 biashara zikafungwa na watu wakashangilia kwa vifijo na nderemo barabarani hata hivyo shangwe yao ilikuwa ya muda tu.

Punde tishio kubwa na la hatari zaidi lilikuwa njiani, iliibuka homa ya Hispania iliyoua watu karibu mara sita ya vita yenyewe, kusambaa kwa homa ya Hispania kulichangiwa na vita ya kwanza ya dunia, wanajeshi waliokuwa wamesambaa sehemu mbalimbali duniani ulaya walipokuwa wakirudi makwao walieneza ugonjwa huo haraka.

Miaka iliyofuata baada ya vita ilikuwa ni ya njaa na hali mbaya kiuchumi, watu wengi barani ulaya hawakuwa na chakula, wakati wa vita ya kwanza ya dunia vikiendelea majeshi ya muungano yalizuia chakula kisiingizwe Ujerumani hali iliyosababisha Wajerumani zaidi ya 750,000 kufariki kwa njaa pia zaidi ya watu milioni mbili walikufa njaa nchini Urusi mwaka wa 1921.

Kufikia mwaka  1923 fedha za Ujerumani hazikuwa na thamani  miaka sita baadaye uchumi duniani kote uliporomoka mwishowe mwaka 1938 vita nyingine ya dunia ilianza ikiwa kama tu mwendelezo wa vita ya kwanza,

VITA YA TATU YA DUNIA?

Hakuna anayejua, inawezekana au isiwezekane hali zilizosababisha kutokea kwa vita mbili kubwa za dunia zingali dalili zake zikionekana hata leo. Mataifa makubwa kuwekeza kwa hali na mali katika kujihami kwa silaha hatari na za kisasa kila kukicha, mataifa moja moja kujitukuza kuliko mataifa mengine na kuhamasisha uzalendo wa hali na mali, miungano yenye nguvu ya mataifa makubwa ya kujilinda na kujihami dhidi ya maadui wa aina yoyote, vuguvugu za kizalendo na kupinga uonevu.

Hivi sasa tunashuhudia kuanzia mashariki ya kati hadi ulaya ya mashariki, huku baadhi ya mataifa makubwa yakiingia katika mizozo mikubwa ya kugombea vijieneo vidogo, hivi sasa Urusi inang`ang`ana na Jimbo la Crimea huku Ukrania ikitetewa na baadhi ya mataifa kuipinga Urusi.

Marekani pia ikiionya China dhidi ya visiwa vidogo vinavyomilikiwa kwa kushirikiana na Japan, hali ni zile zile kama tu zilizokuwa miaka ya 1914 utofauti ukiwa ni aina ya silaha zitakazotumika kwamba tofauti mwaka 1914 zilikuwa zikitumika silaha duni iwapo vita vingine vya dunia vikitokea hakuna kitachosalimika kutokana na ukali na wingi wa maghala makubwa ya silaha yaliyotapakaa katika kila ardhi ya mataifa makubwa.