Home Makala Kushiriki kuwachagua viongozi ni haki yako mwananchi

Kushiriki kuwachagua viongozi ni haki yako mwananchi

256
0
SHARE

NA NASHON KENNEDY 

“MIMI sihangaiki kupiga kura mwaka huu, maana sioni faida yake, watakaokwenda kupiga kura wao wakapige tu”,

Hiyo ni kauli ya Joseph Maiko mkazi wa Nyakato katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza niliyepanda naye daladala nikielekea kazini hivi karibuni jijini Mwanza.

Maiko ni mjasiriamali. Anafanya ujasiriamali wa kuuza juisi ya matunda jijini Mwanza. Ndiye shughuli inayompatia kipato chake halali kwa siku, anaona hakuna umuhimu wa yeye kushiriki kwenye zoezi muhimu la kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu.

Anadai ameshiriki mara kadhaa katika kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya mtaa, wilaya hadi taifa lakini anaona hajapata mafanikio yoyote yale.

“Sijaona mabadiliko, maisha ndio yanazidi kupanda na watoto wanahitaji kusoma, ni bora siku hiyo ya kura niende sokoni kulangua matunda”, anasema.

Wapo akina Maiko wengi ambao kwa namna moja au nyingine na wao wanaelekea kukata tamaa na kutoshiriki katika kupiga kura ili wawachague viongozi wao.

Watu wa aina hii wakifanya hivyo watakuwa wamepoteza haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Katika uchaguzi wa mwaka huu kwa nafasi ya rais, unawahusisha wagombea 15 ingawa ushindani mkubwa upo kwa vyama vitatu vya siasa, CCM, ACT-Wazalendo na Chadema.

CCM imemsimamisha Mwenyekiti wake, Dk. John Magufuli, ambaye mgombea mwenza wake ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tundu Lissu- Chadema na Salum Mwalimu Juma- Mgombea mwenza, Leopard Mahona-NRA, mgombea mwenza- Hamisi Ally Hassan, John Shibuda ni mgombea wa Chama cha Ada-Tadea, ilihali Hassan Kijogoo ni mgombea mwenza, Mtamwega Mgahywa-SAU, Mgombea mwenza akiwa ni Zakia Musa Abeid, Cecilia Mwanga- kutoka Demokrasia Makini, mgombea mwenza wake akiwa ni Tabu Musa Juma, Yeremia Maganja- NCCR-Mageuzi-mgombea Mwenza wake akiwa Amba Hamissi Haji, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na mgombea mwenza wake ni Hamida Abdallah Kuweishil na Philipo Fumbo(DP) na mgombea mwenza wake , Zaina Juma Hamis.

Wagombea wengine waliotangazwa na NEC ni pamoja na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje Dk. Benard Membe-ACT –Wazalendo huku mgombea mwenza wake akitajwa kuwa ni Profesa Omar Fakih Hamad, Twalib Kadege-UPDP) na mgombea mwenza, Ramadhan Ali Abdallah, Hashim Rungwe(Chaumma) na mgombea mwenza wake Mohamedi Massoud Rashid, Mazrui Khalfan Mohamedi (UMD) huku Mashavu Alawi Mohammed akiwa ni mgombea mwenza wake na Seif Maalim Seif( AAFP) na mgombea mwenza wake , Rashid Rai.

Lakini wagombea wengine wawili majina yao hayakuweza kupitishwa na NEC kuwania nafasi ya urais kutokana na kutokidhi vigezo. Wagombea hao ni David Mwaijojele wa CCK na Maisha Mapya Muchunguzi wa NLD.

Kura ni dhamana na haki ya msingi ya kila mwananchi aliye na sifa za kupiga kura kama ambavyo zimeainishwa na NEC.  Kwa wasiofahamu, karatasi ya kupigia kura iko kama karatasi zingine isipokuwa inakuwa na thamani kubwa hasa wakati inapokwenda kutumbukizwa kwenye sanduku la kupigia kura.

Inapotumbukizwa tu hugeuka na kuwa chombo kizito na chenye thamani kubwa kinachoenda kuwaweka viongozi madarakani. Haiitwi karatasi tena.

Kina thamani kwa sababu ndicho huenda kufanya maamuzi ya mgombea yupi kutoka chama gani cha siasa anayefaa kuchaguliwa kuwaongoza wananchi.

Hivyo basi watu wa aina ya Maiko watambue umuhimu wa karatasi (shahada) walizo nazo za kupigia kura. Kuacha kutoenda kupiga kura kwanza hakumuondolei mtu matatizo aliyo nayo kama aliyo nayo Maiko.

Lakini pili kwa kukosekana kwa kura yake moja inaweza kuifanya nchi ikawapata viongozi wabovu. Ni kweli Maiko kama walivyo wananchi wengine wanakabiliana na changamoto kwenye maeneo yao, ambayo hata hivyo chini ya uongozi wa Dk. John Magufuli changamoto nyingi kwa sasa zimepatiwa ufumbuzi.

Lakini suluhisho la kuondokana na changamoto hizo sio kwa wao kutoshiriki katika kupiga kura na kuwachagua viongozi, bali wanatakiwa washiriki kupiga kura ili wawapate viongozi makini watakaoweza kushughulikia changamoto walizo nazo.

KARATASI YA KURA

Muundo wa karatasi ya kupigia kura (shahada) kwa mwaka huu ni ya kawaida, tofauti yake ni kuwa yenyewe imebeba majina ya wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Lakini pia ipo shahada nyingine kwa ajili ya kuwachagua wabunge na madiwani, ambayo shahada zote mbili huwa na majina ya wagombea udiwani na ubunge wa vyama vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Wagombea kwa shahada ya nafasi ya urais imewekwa kwenye mfumo wa kuonyesha picha mbili za wagombea wanaokuwa pamoja, picha hizo ni za  mgombea urais na mgombea mwenza wake. Mfano mgombea urais kwa tiketi ya CCM ni Dk. John Magufuli na mgombea mwenza wake ni Samia Suluhu.

MPIGA KURA

Katika uchaguzi wa mwaka huu, kwa mujibu wa NEC jumla ya Sh bilioni 331.7 ztatumika kukamilisha zoezi la uchaguzi kwa mwaka huu, ambapo jumla ya wapiga kura milioni 29.2 wamejiandikisha kupiga kura za madiwani, wawakilishi, wabunge na Rais huku jumla ya vituo 80,155 vya kupigia kura vimeishaandaliwa.

Anachotakiwa kufanya mpiga kura ni kuwahi asubuhi kwenye kituo cha kupigia kura na kufuata taratibu za NEC kwa kujipanga kwenye mstari na akiwa na shahada yake na kuingia kwenye chumba maalumu cha kupigia kura.

Mara baada ya kuingia bila kulazimishwa au kushurutishwa na mtu yeyote yule au kiongozi, amchague mgombea mmoja kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani kwa kuweka alama ya vema yaani tiki kwenye kisanduku kilicho mbele ya mgombea anayemtaka.

Alama ya vema (V) ikipitiliza kwenye kisanduku ama akatiki alama ya vyema kwenye picha ya mgombea kura yake itakuwa imeharibika.

Hivyo kuna umuhimu wa kuwa makini katika eneo hili la upigaji wa kura, lakini kwa wale wanaosema hawatapiga kura, watambue kuwa kura yao moja ni muhimu sana itakayosaidia wao kupata viongozi bora na sio bora viongozi.

Kituo cha kupigia kura kwa kawaida ni lazima kibandikwe bango kubwa lenye maandishi yanayosomeka “Kituo cha Kupigia Kura”, na siku ya kupiga kura kwa mujibu wa NEC kitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni.

Akishamaliza anatakiwa aikunje karatasi yake mara mbili kisha aitumbukize kwenye sanduku la kura, ambalo huwa limeandikwa kwa maandishi makubwa juu yake, mfano,  kura za urais, udiwani na ubunge na masanduku hayo huwa yana rangi tofauti kama ambavyo itakuwa imeelekezwa na NEC ambacho ndicho chombo chenye jukumu la kusimamia uchaguzi.

Mwananchi akishamaliza kupiga kura yake, atapewa maelekezo na NEC ya kurudi kwenye makazi yake hadi hapo NEC kama chombo kilichopewa jukumu la kutangaza matokeo itapotangaza matokeo yake.

Kama mpiga kura hakutendewa haki wakati wa zoezi la kupiga kura anatakiwa kusajili malalamiko yake kwenye fomu maalumu ambayo huwa kwenye vituo vyote vya kupigia kura.

Bila ya kufanya hivyo, malalamiko yake hayawezi kupewa uzito wowote na Tume, maana kimsingi ili hoja ya mlalamikaji ionekane ni ya muhimu ni lazima isajiliwe.

HAKI YA KUPIGA KURA

Kila raia wa Tanzania aliye na shahada ya kupiga kura ana haki ya kupiga kura. Mtu asikubali kubaguliwa kutopiga kura kwa sababu ya dini yake, rangi yake au maumbile yake au kwa namna yoyote ile kupewa vitisho.

Wanaowatisha na kuwabagua wananchi ili wasipige kura wanavunja sheria halali ya nchi na wanatakiwa kufikishwa mahakamani mara moja.

Kama kuna mtu anayejitokeza kumbagua mtu asishiriki kwenye zoezi la kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kutoa taarifa hiyo mara moja kwenye tume ili hoja yake iweze kusajiliwa na kushughulikiwa ili apate haki yake ya kikatiba kupiga kura.

Licha ya watu wenye sifa ya kuwachagua wagombea wanaowataka kutoka kwa wale halali waliopendekezwa na vyama vya siasa, kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 1985 (Sura ya 343) na kile cha 63 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vinabainisha watu wanaoruhusiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura wakati wa uchaguzi.

Watu hao ni Msimamizi wa Kituo, msaidizi wake, mawakala wa vyama vya siasa, msaidizi wa mlemavu au mgonjwa anayepiga kura, mwangalizi wa uchaguzi wa ndani au wa nje ya nchi aliyeruhusiwa na tume kwa maandishi na mgombea.

Wengine ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ofisa wa NEC na wandishi wa habari ambao nao wataruhusiwa kuingia kwenye vituo vya kura ili kuona zoezi la upigaji kura linavyoendelea kwa idhini ya msimamizi wa uchaguzi.

Uchaguzi huu ni muhimu kwa sababu ndio utakaokwenda kuamua hatima ya serikali ijayo ya awamu ya tano, ili iweze kuondoa na kuzimaliza changamoto zinazowakumba akina Maiko ambao wanaonekana kukata tamaa ya maisha.

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa aina yake, umekuwa ukizungumziwa kila mahali na mnyukano mkubwa uko kwa wagombea watatu Dk. John Magufuli (CCM), Tundu Lisu (Chadema) na Benard Membe wa ACT- Wazalendo ambapo picha kadhaa za ushindani zimeonekana kwenye mitandao maarufu zikishindanishwa.

KUHESABU KURA/MATOKEO

Baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kura, kura zitahesabiwa kwenye vituo na matokeo ya udiwani, ubunge na rais yatabandikwa nje ya mbao za matangazo kwenye vituo hivyo.

Hapa wasimamizi wa uchaguzi watatangaza matokeo ya jumla ya ubunge na udiwani isipokuwa matokeo ya jumla ya urais yatatangazwa na NEC.

Kabla la zoezi la kuhesabu kura, msimamizi atahakiki idadi ya wapiga kura wa kituo chake kwa kulinganisha na idadi ya karatasi zilizotumika  kupigia kura na idadi ya karatasi ambazo hazikutumika na kutoa taarifa kwa tume.

Nahitimisha kwa kuwaomba akina Maiko wajitokeze na kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ambayo ni haki yao ya kikatiba katika kuwapata viongozi bora watakaokuwa mwarobaini wa changamoto zinazowakabili badala ya kulalamika.

Njoo, wewe, yule na wale wote mliojiandikisha mjitokeze kwa wingi mkapige kura Oktoba 28 mwaka huu.

0756 823 420/ 0684 214 114