Home Uchambuzi KUTAFUTA MCHAWI NI KUTOWAJIBIKA KWA MAAMUZI YA SERIKALI YENYEWE

KUTAFUTA MCHAWI NI KUTOWAJIBIKA KWA MAAMUZI YA SERIKALI YENYEWE

1305
0
SHARE

Suala la ndege yetu kuzuiwa Canada lisifanywe ni suala la ushabiki kama ushabiki wa mpira. Ni suala la nchi hili na mjadala wake uwe na hadhi hiyo.

Kitendo cha Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto. Hakuna mwanasiasa anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi. Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi sana ‘ My Country, Right or Wrong ‘. Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda.

Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe na iwe tayari kutoa majibu. Sisi kama vyama vilivyo nje ya Serikali ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote.

Pia ni haki yetu kupata taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali. Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa. Majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo. Hili ni suala la kisheria na suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele.

Nchi kudaiwa sio dhambi. Hata mataifa makubwa duniani yanadaiwa. Watu binafsi tunadaiwa sembuse Serikali? Mimi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa na wengine wamenipeleka mahakamani. Sio dhambi kudaiwa. Muhimu ni 1) Deni limetokana na nini? Ni maamuzi mabovu ya kisiasa? 2) unalipa deni hilo au kuweka mikakati ya kulipa?

Serikali yetu inafahamu kuwa nchi yetu ina madeni mengi na miongoni mwa madeni hayo yameshaamuliwa na Mahakama. Kinachopaswa ni kuwa na maarifa ya kupita ili kuzuia mali zetu nje kuzuiwa kama ilivyo kwa ndege hii. Serikali iwe wazi kuhusu suala hili la ndege. Je ile ya Boeing ( Terrible Teen ) ipo salama? Madeni mengine yenye amri ya mahakama ni yepi? Kwanini Serikali inasubiri kuhojiwa ndio itoe Taarifa?

Hii ni nchi yetu sote. Hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwa pindwa. Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka ndege kuzuiwa, iachane na tabia ya hovyo ya kutafuta mchawi ‘ kwamba eti wanasiasa ndio wamesababisha ‘. Kutafuta mchawi ni kutowajibika kwa maamuzi ya Serikali yenyewe.

Zitto Kabwe