Home KIMATAIFA ‘Kutoroka’ mke wa Mfalme wa Falme za Kiarabu kwazua utata

‘Kutoroka’ mke wa Mfalme wa Falme za Kiarabu kwazua utata

1264
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA NA MTANDAO

Tukio la karibuni la kuondoka kwa mkewe wa pili wa Mfalme wa Dubai Sheikh Mohamed bin Rashid Al Maktoum, Haya binti Al Hussein ni kama mtikisiko kwa familia hiyo ya kitajiri.

Ni mtikisiko kutokana na matukio yaliyoiandama familia hiyo kwa kufuatana kwa kipindi kifupi lakini kigumu na kinachoibua maswali tata juu ya hatima ya himaya hiyo.

Familia hiyo ni kama inaandamwa na mkosi kwa sababu tukio hilo linatokea wakati kukuiwa bado ikiwa katika kumbukumbu ya kuingizwa mjini baada ya kuuziwa dhahabu feki huko nchini Kenya.

Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa kutokana na kuondoka kwa Haya binti Al Hussein ambaye ameondoka na watoto  wanawe wawili wenye umri wa miaka saba na 11, Sheikh Mohamed anadaiwa kutokuwa katika hali nzuri.

Chombo kimoja cha habari nchini Uingereza kinadai kuwa Sheikh Mohamed alionesha kufadhaishwa kwake katika mfululizo wa mashairi yaliyochapishwa kwenye tovuti yake ya mashairi, ikiwa ni pamoja na shairi moja lenye kichwa cha habari ‘Upendo katika macho yako’.

Akitumia taswira ya mtu mwingine Sheikh Mohamed anaeleza kuhusu kutambua aibu  na kuachwa katika hali ya uwendawazimu huku akiomba kusamehewa kwa kutoangalia makosa yake bali kulipa yale matendo yake mazuri.

Katika shairi jingine lililochapishwa katika tovuti ya Dialy Beast amemweleza mkewe huyo kama mwanamke msaliti akitumia baadhi ya maneno kama vile “Wewe huna nafasi yoyote kwangu, Nenda kwa huyo uliyekuwa ‘bize’ naye, labda hilo ndilo nzuri kwako,Sijali ikiwa utaishi au utakufa” alinukuliwa kiongozi huyo.

Mwishoni mwa wiki iliripotiwa kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 45 ameondoka Dubai, na licha ya kuondoka na watoto hao wawili pia pia alichukua kiasi cha pauni milioni 31 zaidi ya sh bilioni 60 kumwezesha kuanza maisha mapya.

Kwa mujibu wa The sun ya Uingereza mwanamke huyo ameomba hifadhi nchini Ujerumani na kufungua madai ya talaka muda mfupi baada ya kuwasili nchini humo. Tovuti moja ya Australia imeeleza kuwa mwanamke huyo aliamua kwenda kwenda Ujerumani badala ya Uingereza kwa kuhofia kuwa mamlaka za Uingereza zinaweza kumrudisha kwa mfalme  huyo.

Hata hivyo taarifa zinadai kuwa mwanamke huyo kwa sasa yupo mafichoni nchi Uingereza na anatarajiwa kusafiri kwenda katika mji wa London.

Taarifa zinadai kuwa tukio hilo limesababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya Falme za kiarabi na Ujerumani baada ya Taifa hilo la Ulaya kukataa ombi la kiongozi huyo kumrejesha mkewe.

Duru mbalimbali zinaeleza kuwa hakukuwa na maelewano mazuri katika ya wawili hao kutokana na mke huyo wa mfalme kutoonekana hadharani tangu Februari.

Sheikh Mohamed bin Rashid Al Maktoum akiwa na mke wake Haya binti Al Hussein

Kuondoka kwa mwanamke huyo kunaibua utata mwingine kuhusu Sheikh Al Maktuom ambaye Machi mwaka jana alikimbiwa na mkwewe mwingine Latifa (33) aliyedai kuwa familia yake imemfunga jela kupitia video moja iliyomwonesha akilalamika kuhusu maisha anayoyapitia katika ndoa yake hiyo. Hata hivyo familia hiyo ya kifalme ya Dubai ilithibitisha kuwa Latifa yuko salama.

Ikumbukwe kuwa Mei mwaka huu Mwanamfalme wa huyo aliingizwa mjini baada ya kutapeliwa Sh milioni 400 nchini Kenya baada ya kulaghaiwa kwa kuuziwa dhahabu bandia ambapo Seneta Moses Wetangula wa Bungoma alihusishwa katika tukio hilo tuhuma ambazo alikanusha kuhusika nazo.

Kwa mujibu wa meneja mmoja wa kampuni inayomilikiwa na Sheikh Mohamed Zlivia alisema matapeli hao waliofanikisha mpango huo walikuwa na ulinzi wa maofisa wa polisi.

Taarifa kutoka mwa maofisa wa Dubai, matapeli hao waliwasiliana na kampuni hiyo wakidai kuwa na tani tano za dhahabu kutoka Ndande Tribe, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) waliyohitaji kuiuza.

Stakabadhi zilizowasilishwa kwa maofisa wa upelelezi na meneja wa kampuni ya dhahabu kutoka Dubai, Ali Zandi, matapeli hao walidai kwamba dhahabu hiyo ilitwaliwa na kuzuiliwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta baada ya kusafirishwa kutoka DRC kwa barabara kupitia Uganda

Hata hivyo katika mkasa huo polisi nchini Kenya walidai kuwa sakata hilo lilianza Septemba mwaka jana matapeli hao walipowasiliana na Zandi, ambaye pia ni mpwa wa Sheikh Mohamed na kumshawishi kwamba wangemuuzia tani 4.6 za dhahabu kutoka DRC na walihitaji pesa za kufanikisha shughuli hiyo.

Duru za polisi zinasema kwamba walaghai hao walitumia wafanyabiashara maarufu akiwemo raia mmoja wa Urusi ili kumshawishi Zandi kwamba walikuwa na dhahabu kutoka Congo ambayo wangeuza Dubai.

Baadae walidai kuwa dhahabu hiyo ilikuwa imezuiwa na maofisa wa forodha katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Zandi akawasiliana na Wetangula amsaidie ili iachiliwe na kusafirishwa hadi Dubai.

Inasemekana Wetangula alisafiri hadi Dubai Desemba mwaka jana ambapo aliwahakikishia kwamba angewasaidia dhahabu hiyo iachiliwe. Safari hiyo ya Wetangula ilitokana na mwaliko wa Zandi.

Taarifa zinadai kuwa Zandi alikataa kutoa kiasi cha Sh 200 milioni ambazo inadaiwa Wetangula aliomba alipwe ili kukamilisha dili hilo jambo ambalo Zandi hakuliafiki na kuamua kusafiri yeye mwenyewe kwenda Kenya kukutana na maafisa wa serikali lakini hakufanikiwa.

Baada ya kufika alipelekwa katika uwanja wa JKIA ambapo alioneshwa makasha yaliyodaiwa kuwa na dhahabu hiyo.

Hata hivyo dili hilo lilihusishwa na watu wenye ushawishi katika Serikali ya Kenya kutokana na taratibu za masuala ya ulinzi zilivyo katika uwanja huo.

Hata hivyo Januari 21mwaka huu inadaiwa kuwa Zandi alikutana na mtu anayedaiwa kuwa waziri katika Serikali ya Kenya ambapo alihakikishiwa kuwa dhahabu yake ingeachiliwa lakini hakuipata na wapelelezi wanasema hakukuwa na dhahabu katika makasha hayo.

Baada ya kutokea hayo Sheikh Maktoum alimwandikia barua Waziri wa Usalama wa Kenya, Dk Fred Matiang’i akitaka serikali iachilie dhahabu yake. Inadaiwa kuwa katika barua hiyo, Sheikh Mohamed anasema anafahamu shehena hiyo ilichelewesha kufuatia shambulizi la kigaidi katika hoteli ya Dusit D2 Februari mwaka huu.

Inadaiwa akiwa Nairobi alishauriwa akodishe ndege ya kampuni ya ndani kutoka uwanja wa Wilson ili kusafirisha dhahabu hiyo bila kutambuliwa, ambapo alifungwa macho na kupelekwa eneo fulani ambako alikutana na  maofisa wa polisi na kutambulishwa kwa mwanasiasa mmoja maarufu.

Inadaiwa licha ya kukodisha ndege hiyo hakuruhusiwa kuingia eneo la kupakia mizigo katika uwanja wa JKIA. Zandi, alidahi kuwa alipompigia simu mtu aliyedai kuwa ni Dk. Matiang’i alimweleza kuwa ndege hiyo ilikuwa chini ya ulinzi wa maofisa maalumu kwa sababu kuna mtu aliyetaka kuiba dhahabu hiyo.

Machi 7, Zandi alilazimika kulipa Sh45 milioni za gharama ya ndege ambayo ilidaiwa kupakiwa JKIA taarifa ambazo zinaelezwa kuwa zilipochapishwa na gazeti moja la nchini humo. Hata hivyo alidai kuwa Wetangula alimshauri aondoke nchini humo kwa usalama wake na akalazimika kukodisha helikopta hadi Kisumu ambapo alikodisha ndege ya binafsi kurudi Dubai.