Home Makala Kuwe na mpango mzuri wa kukabiliana na Covid-19

Kuwe na mpango mzuri wa kukabiliana na Covid-19

528
0
SHARE
Close up of lab assistant in uniform, with mask and rubber gloves holding test tube with blood sample while sitting on chair and typing on laptop. Selective focus on test tubes.

NA TENGO KILUMANGA-STOCKHOLM, SWEDEN

UKWELI ni kwamba ugonjwa wa Covid-19 ni janga la dunia na umeibua mambo mengi sana, kuanzia kwenye taarifa kuhusu maambukizi na jinsi ya kujikinga hadi jinsi ya kuweza kujikinga kuambukiza wengine. 

Hili ni janga ambalo limezileta nchi nyingi kwenye usawa wa magoti na hata kuzishughulisha jumuiya nyingi za ugaibuni, Watanzania wa ughaibuni “diaspora” wameonyesha upendo wao kwa nchi mama.

Hata hivyo bado tuna changamoto nyingi sana hasa kwenye suala la utendaji. Kwa bahati mbaya utendaji wa baadhi ya jumuiya umechukua sura ya siasa za kibinafsi na uwajibishaji ambao kweli unadhihirisha sura ya ukomavu na nadharia umechukua siti ya nyuma. 

Tumeshindwa kuona kwamba mafanikio yetu yapo kwenye kujenga mfumo ambao unatuunganisha kutufikisha kwenye malengo yetu. Ukishaweka tu masilahi ya binafsi kuliko ya umma basi lengo linapotea. 

Kiongozi wa aina yeyote yule ambaye anasimamia muono ni wajibu wake kuangalia mbele na kuona tunaenda wapi, kutafuta njia na kuwahamasisha wenzake anaowaongoza kufuata muono uliopendekezwa. 

Wengine ni kwenye utendaji kuona kwamba dhamira hiyo inafuata na kutekelezwa kutokana na makubaliano na mikataba iliyokuwepo kuona kwamba malengo yanafuatwa kiutendaji wa kila  siku na hii ni dhahiri kufahamu kwamba watendaji wakuu wana majukumu makubwa kuliko mtu yeyote, hata kuliko mwenyekiti au mkurugenzi mkuu hasa kwa kuongoza kamati kuu na kutokuingiza tafsiri za ubinafsi. 

Hapa ni kuhakikisha utaratibu unafuatwa. Utendaji ukianza tu kuleta siasa kwenye jukumu la utendaji basi mfumo hauna mwelekeo na kupoteza mwenendo. Hapa ni dhahiri kwamba utaratibu umevunjwa, kwa sababu gani? Ni kwa sababu wao ndio wanatoa mapendekezo kutokana  na mazingira na shughuli ambazo zinaweza kuathiri jumuiya. Wengine wanafuata mapendekezo ambayo yanaletwa baada ya mijadala ya kuangalia pande zote. 

Si rahisi kupambana na adui usiyemwona au adui ambaye haonekani, mavazi yake ni kama yale ambayo unavaa na harufu ni kama yako au ile ambayo unaitambua kwa hiyo hauioni wala haikushtushi, hasikiki na uhai wake upo mikononi mwako kwa yeye kuishi. 

Ananyoya nguvu zako na kuishi ndani yako mpaka hapo unapopoteza maisha halafu na yeye anaendelea kwa mwingine. Asipopata mwenyeji basi anafariki. Anaishi pale ambapo wengi wapo na wapo karibu. Ni mdudu mwenye njia za hila. 

Ubinafsi ni janga kama Covid-19. Gonjwa la Corona lipo lakini halina nguvu kama halina kiumbe ambacho kinaweza kukibeba. Wakati Covid-19 inaingia kwenye mwili inakumbana na selli ambayo anaifungua na kufanya nyumba yake. Covid-19 inaingia mwilini na kutaka kutawala, inakuja na ufunguo lengo ni kutafuta uhai kwenye mwilli wa binadamu.

Baada ya muda inaipa hiyo seli maagizo kutengeneza virusi vingine kama yeye na baada ya muda inaitekeleza hiyo nyumba na kusambaza virusi vingine mwilini. Ni hali ya hatari kama huna kinga. 

Ukiwa na kinga inazuia kwanza hivyo virusi kungia kwenye seli kwa hiyo virusi havina njia ya kuteka seli yako. Kama huna kinga vikiingia kwenye seli, labda mwili wako utapeleka majeshi ya kinga kupambana na hivyo virusi. 

Ubinafsi ukiingia kwenye mtu mwenye tamaa ya madaraka, unatelekeza yote yale ambayo yanaweza kuwa ni mazuri kwa ushirikiano na maendeleo ya jumuiya. Lakini kama kinga ipo kwa mfano wa katiba ambao ni kinga ya mwanzo kabisa ni rahisi kupambana na ubinafsi. 

Wakati mwingine kinga hiyo haitoshi ubinafsi ukishaingia kwenye utendaji, kinga ya pili ni mwongozo au mfumo wa utendaji ambao upo kawaida na utaratibu ambao upo ingawa haujaandikwa kwa maandishi, ambayo ni busara, akili na maarifa ya kawaida. Ubinafsi ni ugonjwa unaoletwa na tamaa za madaraka au kutokuleta ushirikiano kwa sababu hauleti manufaa ya kibinafsi. 

Nchi nyingi wakati hili janga linapamba moto hazikujua zifanye nini au jinsi la kupigana nalo kwani lilikuwa limevaa mavazi ya kibinadamu na sio rahisi kulitambua. 

Utaratibu ambao upo kwenye janga kama hili haukuzingatiwa au kufuatwa kwani ilionekana hakuna sababu. Nchi zingine ubinafsi umewafanya watu wengi kupoteza maisha na maagizo yamekuja vibaya au kuchelewa. Walioathirika wengi ni masikini, watu ambao wana hali duni na wengi ambao kimsingi kinga yao ipo chini na wana magonjwa mengine. 

Makosa yapo wapi? Katika utendaji kwenye mazingira yoyote yale hauwezi kufahamu kila kitu, hata ukiwa mbunifu na mchapakazi namna gani, ni lazima uombe ushauri wa aidha wenzako katika kazi na kama kuna maamuzi magumu lazima upate baraka waliokuzunguka. Utendaji pia una taratibu zake, unaitwa utendaji ni kwa sababu unafuata ukiritimba uliowekwa kutokana na mazingira ya shughuli zinapofanyika.

Utawala lazima uweke utaratibu katika kutekeleza na kufuata maagizo ambayo yapo wakati kuna matatizo au changamoto kwenye shirikisho, kampuni au nchi. Wakati utaratibu kama huo upo ni kwa sababu pia unaweza kurudi nyuma siku zingine na kuona utendaji ulifanyika vipi kwenye masuala magumu. Ni kama tungetengeneza barabara halafu kuweka utaratibu wa kufuatwa njiani na matumizi ya hiyo barabara. 

Kwenye ujenzi wa barabara lazima ufuate masharti ya ujenzi kama barabara itadumu. Kwenye ujenzi huo zinajumuisha hatua kadhaa. Hatua za msingi za ujenzi katika ujenzi wa barabara zinafanana kwa barabara yoyote. 

Ni kusafisha kila kitu na inaweza kuhusisha  uchimbuaji, kulipua. Sehemu ambayo barabara itajengwa lazima mimea yote iondolewe na kadhalika na ni mchakato mrefu. 

Hata baadaye mkaguzi akija anaweza kuona ubora wa barabara na kiwango kilichokuwa nacho. Haya yote ni masuala na utaratibu unaojulikana, hauwezi mtu ukaja kubadilisha huo utaratibu na ukalaumu kwamba haukuruhusu kuufuata kama wewe ni mhandisi mtendaji, ni wajibu wako kuangalia kazi inafanyika na kama kuna utaratibu umekiukwa ni wajibu wako kuuleta ukashugulikiwa. Hauwezi kupeleka lawama sehemu nyingine kama wewe umehusika.

Nchi inahitaji mpango na utaratibu mzuri wa kukabiliana na matatizo ya Covid-19 na hilo ni suala la utendaji na jinsi nchi imejipanga kutoa taarifa ya kujihadhari, kuwahudumia walioambukizwa na wapo kwenye hospitali maalumu mpaka wanatoka. 

Pia ni muhimu jinsi ya upokeaji wa misaada kwa mfano kutoka kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni. Na ughaibuni ni masuala ya kujipanga na kuona ni njia gani tutaweza kusaidia nchi mama. Yote haya ni masuala ya utendaji, ukikiuka na kusema kwamba haukuwepo au haukufahamu hauwezi kumtupia hizo changamoto mtu mwingine. Wakati wote una vyombo ambavyo vipo tayari kusaidia kama tumekwama.

Intagram: @tengognet

Twitter: @tengok k

Email:  HYPERLINK “mailto:tengo@gmail.com” tengo@gmail.com

Tel: +46705263303