Home Latest News KWA BASHE CCM NI BORA ZAIDI

KWA BASHE CCM NI BORA ZAIDI

5182
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA, MOROGORO


Ukosoaji ni dhana inayochukiwa na wengi. Wengi hudhani anayekukosoa ni adui. Ukweli ulivyo anayekukosoa anakupenda. Binadamu tumeumbwa na mapungufu. Vivyo hivyo taasisi tunazoziongoza, madhali zinaongozwa na sisi biniadamu, nazo huwa na mapungufu katika utendaji na mwenendo wa shughuli zake za kila siku.

Taasisi hizo zisipokuwa na wakosoaji, wanaoweza kusema ukweli, na kushauri nini mbadala kifanyike, taasisi hizo husinyaa au hata kufa. Wakosoaji ni kioo cha kujitazama na kujiweka sawa.

Binadamu tuna hulka ya kupenda kusifiwa kwa kila jambo. Mbaya zaidi hupenda kusifiwa hata tunapofanya vibaya. Upo wakati ambao sifa hulevya. Hakuna aliye mkamilifu. Tunaishi kwa kutegemeana, ukamilifu wa mtu ni mtu mwingine. Vivyo hivyo ukamilifu wa taasisi ni taasisi nyingine. Kwa muktadha huo ni wazi kuwa tunawahitaji wasema ukweli, wasiopepesa macho wala kuona soni kuusema ukweli. Wasio na woga wala wala chembe ya unafiki mioyoni mwao. Hawa ni watu muhimu mno katika ujenzi wa taasisi zetu na katika kufanya ukamilifu wetu kwa lengo la kutukumbusha na kutuimarisha katika kutenda na kuenenda vyema.

Dhana ya vyama vingi vya siasa ilibuniwa ili kuleta ukamilifu na kuondoa uzubavu wa chama kilichopo madarakani. Sote tu mashahidi kuwa CCM ya sasa inayoishi katika upinzani ni imara mara 10 kuliko CCM iliyoishi peke yake pasipo kuwa na upinzani.

CCM ya sasa inapambana kwa nguvu zote kuleta tija kwa wananchi na kuwaondolea kero ikilenga kuendelea kupata uungwaji mkono wa kudumu na waTanzania.

Ukweli Ulivyo kama CCM isingekuwa inaishi katika ulimwengu wa upinzani mambo yasingekuwa kama yalivyo sasa. Sote tunakumbuka namna kodi ya kichwa ilivyokuwa kero kwa wananchi. Ipo mifano mingi ya namna chama kilivyoamua na kuenenda pasipo fikra mbadala  huku kikiwa kimejisahau baadhi ya maeneo.

Uwepo wa vyama vingi vya siasa umeichangamsha CCM na sasa inachapa kazi japo yapo mapungufu ambayo kimsingi yanahitaji ukosoaji. Hili la ukosoaji lilionwa tangu enzi za TANU. Moja ya kanuni/ahadi kumi za mwanaTANU ilitamka wazi kuwa nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko. Ipi tofauti ya kusema kweli na kukosoa? Je nani mkosoaji mzuri. Mkosoaji wa ndani ya chama au wa nje?

Jibu ni kwamba wakosoaji wote ni muhimu. Lakini Ukweli Ulivyo wakosoaji wa ndani ni muhimu zaidi kuliko wakosoaji wa nje. Hii ni kwa sababu wakosoaji wa nje kuna wakati hukosoa pasipo staa. Wengine hutumia lugha za kejeri na matusi pindi wakosoapo upande wa pili. Pia wakosoaji wa nje kuna wakati huwa hawana taarifa sahihi za uhakika juu ya kile wanachokikosoa.

Wakosoaji wa ndani mara nyingi huwa na taarifa sahihi na hulitazama jambo wanalolikosoa kwa mitazamo mitatu. Mtazamo wa kwanza huwa ni kwa manufaa ya chama. Mtazamo wa pili ni kukihami chama dhidi ya wapotoshaji na wapindishaji wa taarifa. Na mtazamo wa tatu ni kukifanya chama kijitathimini na kubaini mapungufu yake kwa kuwa mkosoaji ni miongoni mwa wanachama.

Mwanasiasa kijana, mbunge wa Nzega mjini mwanachama kindakindaki wa CCM ni miongoni mwa wakosoaji wa ndani wa chama hicho. Bashe ni miongoni mwa wadadisi na watukutu wa chama  hiki kikongwe.

Safari ya Bashe kisiasa inaanza mwanzoni mwa miaka ya 2000 akiwa ameshika nyazifa mbali mbali chamani. Hussen Bashe aliwahi pia kugombea nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM).

Namtazama Bashe kama kijana mvumilivu mwenye imani na aliyeshibishwa itikadi ya chama. Kabla ya kuliongoza jimbo la Nzega Mjini sasa, Bashe alishawahi kuwania ubunge wa jimbo hilo bila mafanikio, lakini hakukata tamaa wala kukuhama chama ijapokuwa kuna wakati maamuzi ya chama yamewahi kumuumiza.

Ninaukumbuka uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Katika kura za wagombea ubunge jimbo la Nzega, Bashe alishinda na kushika nafasi ya kwanza, akifuatiwa na Lucas Seleli,  huku nafasi ya tatu ikienda kwa Dk. Hamis Kingwangwala. Katika hali ambayo haikutarajiwa na yoyote, jina la Bashe na la Selelii yalikatwa na Dk. Kigwangwala akapita kama mteuliwa kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Nzega kwa tiketi ya CCM.

Nilikuwa Nzega wakati huo. Ninakumbuka CCM jimboni Nzega ilipata wakati mgumu sana. Bashe alikuwa na uungwaji mkono wa maelfu ya wapiga kura.Wengi kati ya hao walikasirishwa sana na hatua ya jina lake kuondolewa kuwania ubunge. Vyama vya upinzani vilijaribu sana kumshawishi akihame Chama Cha Mapinduzi ili agombee nafasi hiyo kwa chama kingine. Bashe alikataa kata kata na akabaki kuwa mvumilivu, mstahimili na mwenye subira chamani,japo ni kweli kuwa angeenda chama kingine kuwania nafasi hiyo angeshinda.

Mwaka 2015 baada ya jimbo la Nzega kugawanywa, Bashe alipita kiulaini katika nafasi ya ubunge jimbo hilo. Sio lengo la makala hii kuelezea historia ya Bashe, kisiasa Lah hasha!.

Lengo la makala hii ni kutoa hamasa, funzo na mwelekeo sahihi kwa waTanzania hususani wana CCM kujua, kuthamini na kuwa wavumilivu na kutohamaki pindi wanapokosolewa na wakosoaji wa ndani. Bashe licha ya kuwa mkosoaji wa chama na serikali, ndani na nje ya Bunge, kwa taswira na historia yake ni mwanasiasa anayekipenda chama CCM kwa dhati.

Hayo yanathibitishwa na jinsi ambavyo amekuwa mstahimilivu hata pale maamuzi ya chama yalipokwenda kinyume na matarajio yake. Tumeona na kushuhudia wanachama wasio shibishwa itikadi za vyama vyao, wasio wavumilivu, huhama chama pindi wanapoona maamuzi ya chama yamekwenda kinyume na matarajio yao.

JE UKOSOAJI NI UTOVU WA NIDHAMU?

Dk.  Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, aliwahi kunukuliwa akitolea ufafanuzi juu ya dhana ya  kunyamaza pasipo kukosoa.  Anasema,  “ Tunapozungumzia nidhamu hatuzungumzii kunyamazisha watu, tutapata wapi fikra mpya bila kuhojiana, bila kujadiliana, bila kudadisi, bila uchambuzi?. Tukifanya hivyo chama hichi (CCM), kitakuwa mfu.

Hivi karibuni katibu huyu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akiwa safarini kuelekea Kigoma alipita mjini Nzega, Mkoani Tabora na kuzungumza na wana CCM. Katika mazungumzo yake Dk. Ally alimwagia sifa kem kem Bashe kuwa sio mwanachama mkorofi katika chama, ni miongoni mwa wabunge wadadisi, maana kuna tofauti kati ya ukorofi na udadisi na kwa udadisi wake anasababisha tetesi zisizokuwa na ukweli.

Dk. Bashiru aliongeza kusema na kuwahakikishia wana Nzega na waTanzania kwa ujumla kuwa anamfahamu Bashe kabla hajawa mbunge na kuongeza kusema kuwa Bashe ni mtu mdadisi katika maisha yake aliyomjua pia ni mwanachama mdadisi kwa hulka yake.

Alisema kuwa kutokana na udadisi wa Bashe, watu wengine wanaona kama ni utukutu, kufikia wakati baadhi ya wanachama na watu ndani ya CCM walianza kutaka aondolewe, suala ambalo yeye katibu mkuu hakubaliani nalo.

Dk. Bashiru akiongelea michango ya Bashe Bungeni ambayo imekuwa mwiba kwa baadhi ya wahafidhina wa CCM alisema kuwa Bashe ni mfano mzuri wa wabunge wanaochochea usimamizi na kuibua mijadala mizito yenye manufaa kwa Bunge, chama na serikali.

Msingi wa hoja yangu ni mapenzi ya Bashe kwa CCM, tabia, hulka na mtazamo wa wana CCM kwa Bashe. Wana CCM baadhi wanamchukia Bashe. Wanachukia staili ya ukosoaji wa Bashe kwa serikali ya chama chake. Kama ambavyo katibu mkuu amesema kuwa kuna baadhi ya wana CCM walipendekeza afukuzwe chamani. Hawa si wengine bali ni wale ambao kwao kukosolewa ni kashfa.

 

Ukweli ulivyo, CCM inahitaji sana  wakosoaji wa ndani kuliko wa nje. Ikiwa nafasi ya kukosoa ikaachwa kwa walio nje ya chama/wapinzani, kwanza itawajengea umaarufu watu hao. Lakini kubwa zaidi ukosoaji wa aina ya Bashe unaisaidia CCM kwa kuwaziba midomo wapinzani kwani yale ambayo wapinzani wangeyasema, Bashe anayasema.

Hii ina tija sana kwa afya ya chama CCM. Matendo ya Bashe kwa ujumla yanadhihirisha ni kwa namna gani anakipenda chama chake,  lakini baadhi ya wanachama wa chama chake, hawampendi Bashe.Chama kina kila sababu ya kuwaenzi wanachama wenye mtazamo na uthubutu wa aina ya Bashe.