Home Makala Kwa CCM halali, Chadema haramu

Kwa CCM halali, Chadema haramu

1091
0
SHARE

 

Mrisho GamboNA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

SIASA ni sayansi, japokuwa yenyewe ni kama sayansi ‘pori’ ama waweza kuita uchawi na ushirikina. Muhimu ni kukubalika kwenye jamii bila kujali njia unazotumia ni haramu au ni halali alimradi upate idadi kubwa ya wafuasi wanaokusikiliza na kukuamini bila kuhoji kama vile misukule.
Kwa wiki kadhaa sasa suala la posho za madiwani wa Jiji la Arusha  limekuwa gumzo kote nchini, limegeuka siasa za maji taka . Wapo wanaohoji jambo hilo kwa kuzingatia mantiki, lakini wengine ni vipofu wanaosukumwa na ushabiki wa kisiasa.

Posho hizi nchi nzima hutolewa kwa kuzingatia mapato ya ndani ya halmashauri husika , lakini pia kuna waraka unaotumika kama mwongozo.

Hizi posho wanazolipana  zimepewa majina mbalimbali kama vile posho ya usafiri (nauli) , mawasiliano (simu), mchango wa mazishi, takrima wakati wa sherehe na posho ya kikao pale madiwani wanapokuwa kwenye vikao vya kazi.

Nikirudi kwenye posho za madiwani wa Arusha , suala hili lilipitishwa muda mrefu, wakati huo waliopitisha ni lile tabaka katika nchi hii lenye haki kamili (absolute right) ya kula keki ya taifa watakavyo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani lililoketi tarehe 7 /2/ 2008 wakati likijadili bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2008 /2009.

Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi nadhani Mkuu wa Mkoa wa sasa wa  Arusha Mrisho  Gambo ama alikuwa mwanafunzi chuo cha uhasibu Arusha au alikuwa mfanyakazi wa kada ya chini hapo hapo halmashauri ya Jiji akihudumu kama mtaalamu mchanga wa masuala ya Tehama (IT).

Nimetaja jina na cheo cha RC Gambo kwa sababu ndio inaonekana ameshupalia sana jambo hili bila hata kueleza na kutujulisha sisi wananchi ni kwanini hasa au kuna sababu zipi za wazi au za kificho  zilizo nyuma ya uchungu huu alionao kuhusu posho anazoita  kubwa wanazolipwa madiwani.
Katika kikao hicho ambacho idadi kubwa ya madiwani ni kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) iliamuliwa posho za kikao kwa madiwani  ziongezwe, takrima kwa meya iongezeke na unapotokea msiba basi mchango kwa mfiwa usipungue laki tatu uamuzi ambao mkurugenzi wa wakati huo aliubariki.

Leo miaka nane baadaye, halmashauri ya Jiji la Arusha inaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) posho hizo kwa kiwango hicho hicho imekuwa nongwa, haramu, kubwa na nyingi, na sasa RC Gambo anachukulia suala hilo kutafuta huruma za wananchi wa Arusha.

Alianza kuibua chokochoko za posho kubwa wanazolipana madiwani akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) wa Arusha, kiasi cha kubishana hadharani tena mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) Selemani Jaffo, na mshirika wake wa zamani kisiasa Godbless Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini.

Wiki iliyopita Gambo aliwakusanya katika ukumbi wa mikutano wa AICC waalimu wote wa shule za serikali za msingi na sekondari kisha pamoja na mambo mengine akarudia suala lile lile la posho za madiwani wa Arusha na katika kuwapa furaha ya muda akasema madeni yote ya waalimu hao yatalipwa baada ya fedha kukatwa kutoka posho za madiwani.

Wenye kuelewa hawakushangilia, lakini kama nilivyosema hapo juu siasa ni sayansi isiyotabirika kama ilivyo kwa uchawi au ushirikina ndio maana katika kikao hicho walikuwepo walioshangilia bila kuhoji ilimradi shida yao ya siku hiyo imepata mtu wa kuisemea.

Huenda Gambo yuko sahihi kwa sababu serikali hii ya awamu ya tano inajinasibu kwa aina yake ya uongozi wa kubana matumizi kiasi cha Rais John Magufuli kuacha kusafiri kwenda kuhudhuria mikutano inayofanyika nje ya nchi kwa sababu ile ile ya kubana matumizi lakini kubana matumizi ni katika maeneo yale tu yanayoongozwa na wapinzani wa CCM?

Kubana matumizi ili fedha zilizotokana na kodi ya wanachi kuelekezwa  kwenye matumizi ya lazima na ya muhimu kwa wananchi wote wa Tanzania ni jambo jema sana, isipokuwa yanaibuka mambo kwa mfano  Sh 169 zilizotumika kulipa madai ya waalimu ni kweli zilitokana na kufyeka posho za madiwani, kama sio zilitoka kwenye kasma ipi nani aliidhinisha na kwa kikao gani ni miongoni mwa maswali yatakayoibua ubishani baadaye.

Baraza la madiwani kwa mujibu sheria iliyoanzisha Serikali za mitaa ndicho chombo pekee kinachotambulika kama muidhinishaji wa fedha za matumizi ya halmashauri husika na sio kiongozi au mtu mwingine yoyote nje ya chombo hicho kama ambavyo bunge ndicho chombo pekee kinachopanga na kuamua bajeti ya nchi.

Kwa Arusha ni tofauti, hapa RC , DC au DED aweza wakati wowote kupanga, kupangua, kukataza au kuidhinisha matumizi ya fedha bila kujali kama anayo mamlaka hayo alimradi lengo lake la kufurahisha kundi linalomshabikia linafanikiwa.

Haya yote ni upande moja wa shilingi, sasa kama msumeno tuukate upande wa pili. Waliogombea uongozi katika uchaguzi Mkuu uliopita kupitia Chadema hususan Arusha waliahidi masuala mengi ambayo walisema ndiyo yangewatofautisha wao na CCM.

Kwenye majukwaa wakati wa kampeni  rushwa na ulaji mwingine uliokuwa umekithiri ndiyo mambo ambayo yaliitambulisha CCM na kuitofautisha na Chadema au chama kingine chochote.

Kwa kifupi nembo ya CCM ilikuwa wizi na ubadhirifu wa mali za umma na utakatifu wa vyama vingine ni kuwa kinyume na mambo hayo.

Kama nilivyosema dhana ya kuitwa mwanasiasa haieleweki kama ni sayansi au ni uchawi , wananchi wakaamua kujaribu hawa waliojipachika utakatifu kwa kuwachagua kuwa viongozi wao kwa ngazi ya mbunge na madiwani.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mke wa Kaisari hapaswi kutuhumiwa kwa suala lolote , sasa najiuliza kwa dhana hii kwanini Chadema Arusha  imesubiri kwa karibu mwaka mzima kurekebisha kasoro ilizorithi kutoka CCM mpaka RC au DC aipoke madaraka chombo chake halali ambacho ni baraza la madiwani katika kupanga matumizi ya fedha za halmashauri? Nani alaumiwe kama sio wao.

Kwa kutumia sayansi ya siasa makada wa CCM walioletwa kimkakati , RC, DC, na DED wa Arusha wanailazimisha  Chadema kucheza ngoma yao kwa kufuatisha mirindimo wanayopiga kutoka ndani ya ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji Athumani Kihamia, penda wasipende.

Baada ya posho nani anajua kinachofuata? Chadema imelewa sifa na iko kwenye fungate la ushindi, mimi ni mkazi wa Kata ambayo Mstahiki Meya Kalisti Lazaro Bukhay ndiye diwani, matatizo yaliyoko katika Kata hiyo ukisimulia watu wanashangaa wakilinganisha na jinsi wanavyomwona diwani wao tena mshangao umeongezwa na vigezo vilivyotumika kutangazwa kuwa miongoni mwa ma- Meya bora Tanzania.