Home kitaifa Kwa haya ni hatua kubwa ya maendeleo kwa taifa

Kwa haya ni hatua kubwa ya maendeleo kwa taifa

1336
0
SHARE

Esther Mbusi -Dar es Salaam

NI rahisi sana kuikosoa Serikali ukisikiliza watu waliowasikia watu ambao hawajui kinachoendelea au kuhisihisi.

Ni rahisi sana kuikosoa Serikali kwa kuungaunga maneno ya huyu na yule kisha kuongezea yako.

Ni rahisi zaidi kuyafanya hayo yote ukiwa umeketi kitini pako, iwe nyumbani au mahala pako pa kazi ukiwa na simu yako kiganjani. Naam, huwezi kujua yatokanayo bila kutoka.

Nikiwa shuhuda wa baadhi ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, nachelea kusema changamoto za miundombinu katika sekta karibu zote zinaelekea kuwa historia.

Ukiachilia mbali sekta ya usafiri wa anga ambayo imeanza kurejesha matumaini licha ya changamoto zilizokuwapo, barabara karibu nyingi za vijijini zinapitika kirahisi, lakini sekta ya usafiri wa majini ambayo ilianza kupoteza matumaini nayo imeamka.

Nilibahatika kuwa mmoja wa waandishi wa habari waliozuru katika bandari za maziwa makuu, yaani Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Yako makubwa yanatendeka ambayo naamini ndani ya mwaka mmoja usafiri wa majini utarejea katika hadhi yake.

Bandari hizo zinasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa mujibu wa Sheria Na. 17 ya mwaka 2004.

Katika safari hizo, tunakutana na mameneja wa bandari ambao wengi wao ni vijana wanaotambua vyema majukumu yao ambapo wanatupa darasa na kutuonyesha miradi mbalimbali inayotekelezwa katika bandari zao ikiwamo ujenzi na ukarabati wa meli za abiria na mizigo, miundombinu ya bandari ikiwamo ujenzi wa magati.  

Bandari Ziwa Victoria

Bandari ya kwanza kutembelea ni Bandari ya Mwanza katika Ziwa Victoria. Tunapofika hapo tunapokewa na Kaimu Meneja wa bandari hiyo, Geofrey Lwesya. Siku hiyo ya kwanza tunaitumia kwa kutambuana majina na majukumu yetu.

Lwesya anaitumia siku hiyo kututembeza sehemu mbalimbali za Bandari ya Mwanza ambayo ni bandari kuu katika ukanda huo na kisha kesho yake tunazungumza na kuendelea kututembeza katika bandari nyingine ikiwamo Musoma (Mara), Lushamba (Sengerema), Nyamirembe (Chato), Bukoba (Kagera) na nyinginezo.

Kaimu Mkuu wa Bandari za Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya, akionyesha Meli ya Chelezo (floating boat), yenye uwezo wa kupakia meli zinazofanyiwa ukarabati katika Bandari ya Mwanza Kusini.

 Lwesya anasema katika mwambao wa Ziwa Victoria, TPA inamiliki na kusimamia Bandari kubwa za Mwanza Kaskazini, Mwanza Kusini, Nansio, Kemondo Bay, Bukoba na Musoma.

“Kati ya hizo kuna baadhi ya bandari ambazo mamlaka imeshaanza kuziendeleza kwa kuzijengea miundombinu kama bandari ndogo za Ntama, Lushamba na Kyamkwikwi ambazo kuna miradi inayoendelea.

“Bandari za Mwanza zina uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo ambapo ndani ya mwaka mmoja yaani Julai mwaka jana hadi Mei mwaka huu bandari hiyo imehudumia meli 1,013,” anasema.

MAPATO

Akizungumzia mapato yatokanayo na shughuli mbalimbali bandarini hapo ikiwamo kupakia na kupakua shehena, Lwesya anasema yameongezeka kwa wastani wa asilimia 54.6 sawa na Sh milioni 1,138.28 katika kipindi cha mwaka 2018/19 kutoka Sh milioni 619.71 mwaka 2017/18.

Lwesya anataja sababu za kuongezeka kwa mapato hayo ni kufunguka kwa njia ya Mwanza hadi Bandari ya Uganda ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 10.

“Pia kurejea kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Musoma ambayo inahudumia meli zaidi ya tatu kwa siku, matumizi ya mfumo mmoja unaolingana tangu mwaka jana.

“Lakini pia matumizi kielektroniki katika makusanyo ya mapato yanayotumika katika bandari kubwa za Kemondo na Mwaloni, Kyamkwikwi, Mwanza Kaskazini na Kusini, Isaka, Mwigobero Bukoba na Mwalo wake na Nansio nazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato hayo.

“Pia kurejea kwa wateja ambao walikuwa wameacha kutumia Bandari ya Mwanza Kusini na Musoma na maboresho ya shughuli za usafirishaji katika mashirika ya Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL),” anasema.

MIRADI

Pamoja na mambo mengine, ipo miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Bandari ya Mwanza kwa lengo la kuboresha bandari ikiwamo ujenzi wa gati la Ntama katika Bandari ya Sengerema, ujenzi wa gati la Mwigobero katika Bandari ya Musoma ambao tayari umekamilika na umegarimu Sh milioni 605.036.

BANDARI YA MUSOMA

Katika Bandari ya Musoma kuna miradi mbalimbali inaendelea ikiwamo kukamilika kwa ujenzi wa gati la abiria huku mkuu wa bandari hiyo, Almachius Rwehumbiza akijinasibu namna walivyojipanga kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara na wadau wa bandari hiyo.

Anasema bandari hiyo inao uwezo wa kupokea meli tatu zenye tani 1,500 hadi 5,000 kwa wakati mmoja.

Moja ya kampuni zinazotumia bandari hiyo kusafirisha mizigo ni kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula yanayotengenezwa kwa mbegu za pamba cha Mount Meru Millers kilichoko Bunda mkoani Mara.

Justine Rukaka ni Ofisa Uhusiano katika kiwanda hicho, anasema Mamlaka ya Bandari Ziwa Victoria imefanya jambo jema kurejesha huduma za usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Musoma kwani huduma hiyo imewaondolea adha ya kusafirisha malighafi na kupunguza gharama za usafiri.

“Tulikuwa tukisafirisha mbegu za pamba kutoka nchini Uganda na kuzipokelea Bandari ya Mwanza Kusini kabla ya Bandari ya Musoma kurejesha huduma za usafirishaji wa mizigo kwa gharama kubwa.

“Kwa sababu hiyo, tulilazimika mara baada ya kupokea mzigo Mwanza tuusafirishe tena kwa malori kutoka Mwanza kwenda Bunda.

“Tumekuwa tukipokea tani 250 hadi tani 500 za mbegu za pamba kwa mara moja kulingana na ukubwa wa meli inayoleta mzigo siku hiyo, hivyo kwetu sisi imekuwa rahisi kwa uendeshaji na uzalishaji wa kiwanda kutokana na gharama za usafiri kupungua,” anasema Rukaka.

Pamoja na mambo mengine, Rukaka anawaasa wafanyabiashara mbalimbali kutumia bandari ya Musoma kusafirisha mizigo yao ya biashara kwa sababu gharama zake ni za kawaida na unaweza kupakia mzigo kwa wingi tofauti na kusafirisha kwenye malori.

BANDARI YA BUKOBA

Katika Bandari ya Bukoba wao wamejizatiti katika meli za mizigo huku wateja wao wakubwa wakiwa Kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Hatua hiyo imefanya kuwapo kwa ongezeko la mapato katika bandari hiyo ambao pia unachagizwa na mfumo wake wa ukusanyaji kwa njia ya kieletroniki.

Mfumo huo umesababisha ongezeko la makusanyo kutoka Sh milioni 21 hadi 29 hadi kufikia Sh milioni 60 hadi 69 kwa mwezi.

Pamoja na mambo mengine, Lwesya anasema mapato hayo huenda yakaongezeka baada ya ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo unaotarajiwa kukamilika Septemba mwaka 2020.

Pamoja na ujenzi wa meli hiyo pia ujenzi wa gati la kisasa unaoweza kuhimili meli zote na boti.

“Baadhi ya majengo muhimu yakiwamo majengo ya abiria, sehemu za kuhifadhia mizigo, vyoo vya kisasa, vibanda vya walinzi na zote vyenye ubora wa kisasa yao katika hatua za mwisho ambapo tumeboresha maneo bandari yetu iendane na huduma zinazotolewa na bandari hiyo.

“Jengo la abiria la kisasa limekarabatiwa pamoja na ofisi, ujenzi uliogharimu Sh milioni 143.8, kwa sababu tunatarajia Meli ya MV Victoria ambayo inafanyiwa marekebisho ya kubeba abiria na mizigo kuanzia tani 1,200 hadi 4,000.

“Pia kuna meli ndogo maalumu zinazohifadhi ubaridi kwa ajili ya kubebea samaki kutoka visiwani na kupelekwa viwandani,” anasema.

Kwa upande wake mkuu wa bandari hiyo, Bulenga Ndalo anasema meli ndiyo usafiri muhimu unaotegemewa Bukoba hivyo kusimama kwa huduma hiyo kumesababisha adha kwa watu wengi kwani kwa sasa bandari hiyo ambayo inahudumia visiwa viwili vya Kerebe na Gozba, haina meli ya abiria bali wanategemea boti kwa ajili ya usafiri.

“Zamani kulikuwa na meli mbili za mizigo, lakini sasa kuna meli tano kubwa zinazoingiza kwa mwezi mizigo mbalimbali ikiwamo vifaa vya dukani tani 200, mkubwa ukiingizwa na Kiwanda cha Kagera Sugar ambao ni tani 3,500,” anasema.

Peter Hiza, ni nahodha wa meli ya MV Luxury II, ambayo ni ya mizigo inayofanya safari zake Mwanza-Bukoba, anasema anapata huduma nzuri ikiwamo kupakia na kushusha mzigo kwa wakati ambapo kwa wakati mwafaka.

Anasema meli yake imeingia ubia na TBL kupeleka bia Bukoba kutoka Mwanza.

“Tunatumia bandari za serikali kutokana na gharama za kawaida ambapo huwa nakuja kuleta mara mbili kwa mwezi kuleta mzigo,” anasema.

Kwa upande wake, Shamsa Mohammed, mwakilishi wa Kagera Sugar, anasema wanaisubiri meli mpya kwa hamu kwani kuna unafuu mkubwa katika usafiri wa mjini kuliko barabara katika kusafirisha sukari.

“Tani tunazosafirisha kutoka Bukoba kwenda mikoa mingine tunatumia meli kwani ina gharama nafuu na inafika salama,” anasema.

BANDARI YA LUSHAMBA

Katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, nako kuna mradi mkubwa katika Bandari ya Lushamba ambapo unaotarajia kunufaisha wakazi wilayani humo katika  usafiri wa majini baada ya adha ya usafiri huo kwa miaka 61.

Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa gati la bandari hiyo iliyopo katika Kijiji cha Kanyala, uliogharimu Sh bilioni 1.265 ambazo ni fedha za ndani, itakayoanza kutumika Julai baada ya usafiri huo kuwa wa kusuasua tangu mwaka 1958.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Lazaro Mgonzo anasema kuanzia mwaka 1958 hakukuwa na usafiri wa kwenda kisiwani hivyo kuanza kwa usafiri huo utatatua changamoto hiyo.

“Tunashukuru serikali kwa kutukumbuka kwa ujenzi wa bandari ambayo itarahisisha usafiri wa kwenza kisiwani ambao kwa miaka mingi umekuwa na changamoto nyingi,” anasema.

Naye Mtendaji wa kijiji hicho, Benjamin Ndungwizi, anasema licha ya kurahisisha usafiri, pia bandari hiyo ambayo inategemewa na wakazi 8,798 wa vitongoji vinne vya Mwibale, Msikitini, Kisarazi na Gembale, itatoa ajira kwa vijana wa maeneo hayo kuzunguka kijiji.

“Tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kufikiria kutujengea bandari kwa sababu pia ni njia moja ya kututangaza  na sababu nyingine nyingi katika kurahisisha huduma mbalimbali.

“Nitoe wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya bandari hii kwa sababu wote ni wanufaika,” anasema.

Lwesya anazungumzia mradi huo kuwa umefikia asilimia 90 ya kazi ya utekelezaji ambapo sehemu iliyobaki ni kumalizia ujenzi wa jengo la abiria, jengo la mizigo, uzio, vyoo mnara wa tanki la maji na chumba cha mashine ya umeme.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina, anasema gati hilo lina urefu wa mita 60 ambapo wakati wa ujenzi wake nyumba nne za wananchi zililipwa fidia ili kupisha mradi huo.

“Mradi huu ni wa mwaka mmoja ambapo tunategemea mkandarasi kuukabidhi Julai 9, mwaka huu na hatutegemei kuongeza muda,” anasema.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi katika Kijiji cha Kanyala, Charles Shuka, anasema wanaishukuru Serikali kwa bandari hiyo, ambapo sasa watatumia meli kulinganisha na boti ambazo zimekuwa ni usafiri hatarishi, lakini pia anaiomba  ifikirie kuwapelekea vivuko.

BANDARI YA CHATO

Kwa upande wa Bandari ya Nyamirembe, iliyopo Wilaya ya Chato mkoani Geita, yenyewe iko katika hatua za umaliziaji na inatarajiwa kukamilika Agosti 23.

Mradi wa ujenzi huo uliogharimu Sh bilioni 4.1 ambazo ni fedha za Serikali, unajengwa na Mkandarasi wa ndani ambaye ni Kampuni ya VJ Mistry kutoka Bukoba mkoani Kagera.

Injinia Msina anasema mradi huo kazi iliyobakia ni kumalizia ujenzi wa gati, jengo la abiria, jengo la mizigo, chumba cha mashine ya umeme, vyoo na chumba cha walinzi.

“Katika gati hili, meli ziliacha kuja miaka minane iliyopita kwa sababu kampuni iliyokuwa inaleta meli hizo kusitisha kwa sababu zao wenyewe, lakini TPA wameurudisha mradi huu.

“Bandari hii itakapoanza kazi itachochea biashara kati ya nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na nchi jirani,” anasema.

Naye mwakilishi wa mkandarasi wa mradi huo, Injinia Anderson Mbogowe, anaeleza kuwa hadi Juni 8, mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 47 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo Julai na kisha kuukabidhi kwa Serikali Agosti.