Home Latest News Kwa hili la Makonda naamini mmenielewa

Kwa hili la Makonda naamini mmenielewa

1732
0
SHARE

WAKATI naandika makala kwenye gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari Rais Magufuli bwana, eti Makonda naye RC. Watanzania wengi hawakunielewa.

Sababu iliyochangia wengi kutonielewa ilitokana na wengi kutomuelewa kiongozi huyo kijana na kujikuta wakifikiria labda nilikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakimuonea wivu.

Ingawa katika makala ile niliwaonyesha wasomaji kwamba kiongozi huyo si mtendaji zaidi ya kujificha katika kichaka cha kutoa matamko yasiyotekelezeka.

Katika makala ile niliweka wazi kile nilichokibaini katika utendaji wake alipokuwa akihudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Kichaka hicho cha matamko ndicho hasa kilimsaidia Makonda kuteuliwa kwa kile ambacho Rais John Magufuli alifikiri ni mchapakazi mzuri huku akiishia kuwaponda wakosoaji wake kwamba walikuwa wakimuonea wivu.

Katika makala hiyo nilijiuliza kuhusu sababu zilizowaingiza mkenge kumteua ni Je, waliamini atafanikiwa kuwabana wapinzani ambao kwa sasa wanaongoza jiji?.

Niliuliza chaguo hilo lilichangiwa na namna alivyo mjanja wa kutumia vyombo vya Habari katika matamko yake bila kujali kama yanatekelezeka au la?

Katika makala ile nilionyesha baadhi ya matamko ambayo amewahi kuyatoa hadi kesho hakuna lililofanyiwa kazi kwa mfano ujenzi wa machinjio ya kisasa Kinondoni.

Nilihoji kwamba nafasi hiyo ameipata kwa sababu ya kutumia jeshi la polisi kumzuia Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kuhutubia wafanyakazi wa kiwanda cha Took Tanzania kilichopo EPZ waliokuwa wakitafuta ufumbuzi wa madai ya nyongeza yao ya mshahara?.

Ahadi nyingine ambazo nilionyesha kwenye makala ile kwamba si kiongozi wa kuaminiwa ni ile aliyowaahidi walimu wa Dar es salaam kupanda mabasi bure ambayo hadi leo ilishindwa kutekelezeka kisheria na kinadharia.

Katika makala ile nilionyesha kwamba wakati akiwa Mkuu wa wilaya alitoa ahadi ya kumalizia jengo la hospitali ya Palestina ambalo hadi leo halijamalizwa.

Ahadi nyingine aliitoa hospitali ya Mwananyamala akiahidi kufanya mipango ya kuhakikisha kuwepo kwa askari polisi watakaotoa Huduma ya Karatasi namba Tatu (PF3) ya jeshi la polisi jambo ambalo halijatekelezwa.

Jambo ninalokumbuka alilosema na kulisimamia hadi mwisho ni shindano la kusaka vijana wenye vipaji wa Kinondoni ambao walikuwa wakishindanishwa.

Niliandika katika makala ile kwamba Rais Magufuli aliingia mkenge kwamba kutokana na ahadi zake zisizotekelezeka alidhani ni mchapakazi hivyo aliamini ataweza kuwabana wapinzani katika chaguzi zijazo dhidi ya CCM.

Rais wetu mpendwa ameshindwa kutazama alama za nyakati kwamba kijana huyo pamoja na kuwa Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni, Ukawa wamefanikiwa kutwaa majimbo manne na hakuna alichoisaidia CCM.

Udhaifu wa kijana huo umeanza kubainika zaidi kwa watanzania walio wengi baada ya kupata nafasi ya kuongoza Mkoa wa Dar es salaam.

Sababu kubwa inayomuonyesha hivyo ni matamko anayoyatoa katika mkoa huo na kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu ikiwemo kuwatoa ombaomba lakini hadi leo limebaki kuwa kitendawili.

Pamoja na kutoa matamko hayo huku akishindwa kutimiza kile alichoahidi amejikuta akiendelea kutoa matamko mengine yasiyotekelezeka.

Miongoni mwa tamko ambalo limeachwa maswali ni lile alilotoa Julai 15, 2016 saa 2:18pm kwenye akaunti yake ya Mkuu wa mkoa la kutaka kukamata vijana wasiokuwa na kazi.

Andiko lile lilikuwa likisomeka “Nimetangaza msako wa wakazi wa Dar es Salaam wasiokuwa na kazi maalumu za kufanya, Nasema jeshi la polisi litaanza msako huo wakati wowote na nawataka wenyeviti wa mitaa kutoa ushirikiano wa kutosha, na nasisitiza viongozi ambao hawatatoa ushirikiano watakamatwa”

Mkuu huyo wa mkoa alikuwa kimya pamoja na taarifa kuandikwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hadi Julai 18, 2016 ndipo aliibuka kukanusha baada ya kulaaniwa tamko lile kila mahali.

Mkuu huyo wa Mkoa ninayeweza kusema anaandikwa zaidi ya wakuu wenzake wa mikoa ameibuka na kukanusha kauli hiyo na kusema kwamba hakuandika maneno hayo.

Jambo la kuchekesha na kuacha maswali kijana huyu alikanusha kwenye kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Clouds FM, akisema amezushiwa na mashabiki wa ushoga na wauza shisha.

Kauli hiyo ya Makonda, bado anaacha maswali kadhaa ikiwemo je, akaunti hiyo ambayo ilitoa taarifa za awali za kutaka wasiokuwa na ajira wakamatwe, ni yake au siyo yake na kama si yake kwa nini alikaa muda kujibu kauli hiyo?

Makonda alitakiwa kuthibitisha kwa kauli yake kuhusu hao aliosema wanatumia jina lake vibaya mitandaoni ili wananchi waamini si muendelezo ule ule wa kutoa ahadi zisizotekelezeka.

Makonda anatakiwa kuwataja hadharani hao mashabiki wa ushoga na wauza shisha ambao wanamlisha maneno ambayo siyo yako, wala haukuwahi kuyatamka.

Swali jingine la kujiuliza ni kwamba amekana kuijua akaunti hiyo lakini inakuwaje, anasema hatafuti vijana wasio na ajira na badala yake anataka kujua vijana wote walioko kwenye mitaa yetu.

Swali jingine unasema hao watu wauza shisha na waunga mkono ushoga watakuwa wanafanyahivyo kwa faida ya nani?

Swali jingine la msingi kama waraka ule haukuwa wa Makonda imekuwaje amjibu, Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliyesema sheria haimruhusu kukamata na mwenyewe kusema anaweza kufanyahivyo kwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa?