Home Makala Kimataifa Kwa mambo haya Fabregas hawezi kusahaulika England

Kwa mambo haya Fabregas hawezi kusahaulika England

1964
0
SHARE

LONDON, England

HIVI karibuni aliyekuwa kiungo wa zamani wa Chelsea, Cesc Fabregas, alitoa siri ya kilichomfanya aondoke ndani ya kikosi hicho katika dirisha la usajili la Januari mwaka huu.

Kiungo huyo raia wa Hispania kwa sasa yupo nchini Ufaransa ndani ya kikosi cha Monaco, akipambana kila wiki kuisaidia timu hiyo isishuke daraja.

Fabregas alicheza mchezo wa mwisho akiwa na jezi ya Chelsea dhidi ya Nottingham Forest kwenye Kombe la FA katika mzunguko wa tatu.

Fabregas atabaki kuwa mmoja wa viungo bora kuwahi kutokea katika Ligi Kuu ya England hasa alipokuwa chini ya Arsene Wenger ndani ya Arsenal na hata Chelsea.

Aliondoka Arsenal kujiunga na klabu yake ya utotoni Barcelona ambako alishinda kila taji nchini Hispania akiwa na kikosi hicho chenye maskani yake Catalunya.

Alirejea nchini England lakini safari hii alijiunga na Chelsea ambao ni wapinzani wa Arsenal na kufanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England, FA na Carabao.

Anashika nafasi ya pili kwenye rekodi ya wachezaji wanaoongoza kupiga pasi za mabao ‘assist’ nyuma ya Ryan Giggs lakini Fabregas anatajwa kuwa kiungo bora wa kigeni kuwahi kutokea ndani ya Ligi Kuu ya England.

Haya ni mambo ambayo yatamfanya kiungo huyo asisahaulike kwa urahisi ndani ya England kwa kipindi chote alichokuwa Arsenal na Chelsea.

MCHEZAJI MDOGO ZAIDI

Oktoba 28, 2003 Fabregas alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa na jezi ya Arsenal dhidi ya Rotterdam kwenye Kombe la Ligi, wakati huo akiwa na miaka 16 na siku 177.

Siku hiyo ilimfanya kiungo huyo kuandika historia ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuvaa jezi ya Arsenal.

Desemba ndani ya mwaka huo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika historia ya Arsenal.

Hapo ndipo alipoanza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi cha Arsenal, zile zilikuwa mechi ambazo zilimpa kujiamini na kumshawishi Wenger kuwa ni mchezaji anayestahili nafasi ya kucheza.

Fabregas alikuwa kando ya Patrick Vieira mpaka pale alipojiunga na Juventus, kiungo huyo raia wa Hispania alikuwa tofauti na wengine nchini England hasa kwa aina ya uchezaji wake wa kupiga pasi nyingi.

NAHODHA WA ARSENAL

Novemba 2008, Fabregas alikabidhiwa kitambaa cha unahodha kwa mara ya kwanza ambacho kilikuwa kikivaliwa na William Gallas.

Wakati huo alikuwa na miaka 21 tu, lilikuwa jambo la kushangaza kwa baadhi ya mashabiki na wadau wa soka duniani ikiwa ndani ya Arsenal kulikuwa na nyota wenye umri mkubwa zaidi ya Fabregas.

Lakini hilo halikumfanya Wenger kushindwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo kubwa ndani ya klabu, kwa kipindi chake alifanya kazi kubwa kama nahodha wa Arsenal.

Mwaka 2011 ulikuwa msimu wake wa mwisho kabla ya kurejea Barcelona ambako muda mwingi alitumika katika eneo la straika.

Aliporejea England kujiunga na Chelsea alitumika eneo la chini zaidi kwenye kiungo akiwa na kazi ya kuvusha mipira lakini inadaiwa kuwa Fabregas bora zaidi alicheza namba 10 chini ya Wenger.

MEDALI ZA EPL

Kwa zaidi ya miaka sita aliyokuwa Arsenal hakufanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya England lakini alipoenda Barcelona alishinda makombe mawili ya La Liga.

Mwaka 2013, Jose Mourinho alimsajili Fabregas ndani ya kikosi cha Chelsea na kumfanya kutimiza ndoto ya kuvaa medali ya Ligi Kuu ya England.

Msimu wa 2014/15, Chelsea walifanikiwa kutwaa taji hilo na Fabregas kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi hicho.

Chini ya Antonio Conte msimu wa 2016/17 alifanikiwa kuvaa medali ya pili ya ligi hiyo na kukata kiu ambayo alikuwa nayo wakati yupo Arsenal.