Home Afrika Mashariki KWA NINI KESI ZA UHAINI NI KAWAIDA BARANI AFRIKA?

KWA NINI KESI ZA UHAINI NI KAWAIDA BARANI AFRIKA?

6654
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Hakuna ubishi kwamba Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu ’Bobi Wine’ – mwanasiasa, mwanamuziki na mcheza sinema sasa hivi ni mwiba mkubwa kwa utawala wa rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye yuko madarakani kwa miaka 32 sasa.

Wiki mbili zilizopita Bobi Wine alikamatwa kupitia nguvu kubwa ya dola na baadaye kushitakiwa kwa makosa ya uhaini pamoja na watu wengine 32. Waendesha mashitaka walisema watuhumiwa hao walirusha mawe kwenye msafara wa Rais Museveni akiwa kaskazini mwa Uganda.

Kesi hii ilitikisa nchi nzima, lakini pia si mara ya kwanza kwa wanasiasa wa upinzani kufunguliwa kesi za uhaini nchini humo. Mwaka 2016, Kizza Besigye kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Forum Democrtatic Change (FDC) alishitakiwa kwa uhaini baada ya kujiapisha kuwa ‘rais wa watu’. Alidai uchaguzi mkuu wa mwaka huo ulijaa udanganyifu na kwamba yeye ndiyo alikuwa mshindi halali.

Lakini hata katika nchi nyingine Barani Afrika, kesi za uhaini dhidi ya viongozi wa upinzani zimetokea kuwa kitu cha kawaida. Kesi hizi mara nyingi hujengwa kwa ushahidi dhaifu na ni mara chache sana watuhumiwa hukutwa na hatia, hali ambayo huibua maswali kwa nini baadhi ya tawala hukibizana nazo.

Sababu iliyo wazi ni kudhibiti upinzani. Kuwatia nguvuni wanasiasa wakuu wa upinzani huwaondoa kutoka barabarani, majukwaani na mitandaoni. Katika baadhi ya nchi kesi ya uhaini humfanya mtuhumiwa akose dhamana.

Na katika nchi nyingine watuhumiwa wanaweza kupata dhamana, kama vile ilivyo kwa Bobi Wine, lakini kwa masharti magumu yanayoathiri harakati zao za kisiasa.

Na usikilizaji wa kesi hizo huchukua miaka kadha. Huko Zimbabwe chini ya Robert Mugabe ilikuwa kawaida kesi za uhaini kutumika dhidi ya viongozi wa upinzani wakati uchaguzi ukikaribia. Kwingineko kesi za uhaini zimefunguliwa dhidi ya wapinzani wanaopinga ushindi wa mgombea wa chama tawala kama vile Dk Kizza Besigye huko Uganda.

Huko Kenya, mapema mwaka huu mwanasheria Miguna Miguna mwenye pasi ya kusafiria ya Canada alitiwa nguvuni na kushitakiwa kwa uhaini baada ya kushiriki katika tukio la kujiapisha kwa kiongozi mkuu wa upinzani kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta. Hata hivyo baadaye mwanasiasa huyo alipelekwa Canada kwa nguvu.

Aidha uhaini ni msamiati mkuu katika suala zima la siasa katika nchi nyingi Barani Afrika, ambako baadhi ya viongozi wao huwaona wapinzani kama maadui wa taifa.

Kuna baadhi ya nchi ambako maandamano yanayopangwa na wapinzani hupigwa marufuku na utawala kwa onyo kwamba atakayeshiriki atakuwa amefanya kosa la uhaini.

Aidha baadhi ya watawala walio madarakani hawapendi kuonekana kuzidiwa hadhi na wapinzani. Mwaka jana (2017) kiongozi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema, alitiwa nguvuni na kushitakiwa kwa uhaini baada ya msafara wake wa magari kushindwa kuupisha ule msafara wa Rais Edgar Lungu.

Inadaiwa hali hii ya kutovumiliana ina mizizi tangu enzi za ukoloni. Waingereza walikuwa wanawakamata na kuwatia korokoroni viongozi wa kizalendo kama vile Jomo Kenyatta (Kenya) na Kwame Nkrumah (Ghana), kuhusiana na tuhuma mbali mbali. Hawa hawa walipopata uhuru walitunga sheria ambazo sasa zinatumika dhidi ya watu kama akina Bobi Wine.

Maeneo ya siasa za upinzani yamebanwa sana katika nchi kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Congo DRC na hata Tanzania. Baadhi ya nchi hizi siasa hupiganwa kupitia maeneo mawili. Mosi ni eneo lile la kawaida la kushindana kwa hoja katika mijadala ya wazi ya kutafuta ushawishi wa kuomba kura, na pili ni mapambano kupitia vikosi vya usalama kudhibiti hali ya kisiasa.

Mwaka 2016 Katibu Mkuu wa chama tawala cha National resistance Movement (NRM) nchini Uganda, akitoa onyo wa watu kutoandamana alisema: “Watoto wenu wanaweza kuuawa.” Nchini Uganda na kwingineko, maandamano ni kama uasi mkubwa kwa sababu utawala hauwezi kufikiri vinginevyo.