Home Makala KWA PAMOJA TUUTOKOMEZE UDHALILISHAJI Z’BAR

KWA PAMOJA TUUTOKOMEZE UDHALILISHAJI Z’BAR

1080
0
SHARE

NA RASHID ABDALLAH

Jambo moja zuri sana kuhusu wanafunzi katika kisiwa cha Pemba ni kutolipa nauli, la muhimu uwe tu ya unifomu za skuli ,  kondakta hatokudai hata shilingi kumi. Ile nauli ya mia mbili  kwa wanafunzi haiko kabisa katika kisiwa cha Pemba.

Pia watu wenye gari  binafsi huwasaidia wanafunzi wakati wa kwenda au kurudi shule, ingawa suala hilo la kuwachukua wanafunzi sio la lazima na hufanywa na dereva kwa hiari tu na wengine huwa hawafanyi kabisa.

Kuna kisa cha binti kutoka Pemba ambaye alikuwa anatoka skuli kuelekea nyumbani, alipata msaada wa kuchukuliwa na mtu katika gari yake binafsi, bahati mbaya hakumshusha binti yule eneo la nyumbani kwao, na kuamua kumchukua mpaka anakotaka yeye.

Kumbe lengo kubwa ni kwenda kumshawishi kufanya naye ngono, wakati mtu yule anaendelea kumshawishi, binti akasimama na kusema kwamba; sio tatizo kufanya nae mapenzi lakini yeye ni miongoni mwa wanafunzi sita katika shule yake ambao ni waathirika wa Ukimwi.

Nani anapenda kusikia hadithi za ukimwi mbele ya uso wake? Hayupo, kilichofata mtu yule alimtimua binti na hapo ndipo ilipokuwa salama yake. Ukweli ni kwamba hakuwa muathirika,  kumbe alipitia mafunzo ya  kukabiliana na udhalilisha pindi unapotaka kumtokea.

Siku moja skuli yetu ilipata wageni, ambao kwa sababu ya udogo wangu sikumbuki walitoka taasisi gani, lakini walikuja kwa lengo la kutoa elimu kuhusu udhalilisha,  wakati nikiwa shule ya msingi, na ndipo walipotusimulia kisa hicho.

Huo ulikuwa ni utangulizi na sasa tuanze makala yetu. Suala la udhalilishaji kwa Zanzibar limeanza kupigiwa kelele siku nyingi, linazima na kupumua, kuna wakati kesi zinakuwa nyingi zaidi.

Kuna changamoto kadhaa katika kupambana na jambo hili, kuanzia katika vyombo vinavyohusika na ushughulikiaji wa matatizo haya, hadi katika jamii ambayo matatizo ya udhalilishaji yanatokea.

Katika jamii yenye kusifiwa kwa ustaarabu, lugha moja, imani moja na utamaduni wa aina moja, matukio haya yanachafua sura ya jamii hii, haina maana kwamba jamii yote ni mbaya kwa sababu ya watu wachache.

Maana yangu ni kwamba watu wa jamii hii tunapaswa pia kuwa kitu kimoja katika kupambana na hawa wanaochafua sura ya  hii jamii. Tusiwe wepesi tu kuungana kwa sababu ya CUF au CCM, yatupasa pia tusisahau kuungana katika changamoto zinazotukabili katika majumba yetu.

Miongoni mwa changamoto iliyop,  jamii zetu zinaficha haya mambo. Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Micheweni katika kisiwa cha Pemba , Salama Mbarouk Khatib alilalamika kwamba jamii zinayaficha haya mambo, wakati akizungumza na Zaima TV.

Wala sio uongo, wakati mwengine familia ambayo mtoto wao kaharibiwa hukaa kitako na kukubaliwa palipwe pesa. Vishilingi kadhaa  ndio vitafidia uharibifu aliofanyiwa mtoto?

Kwa sababu hizi pesa kikawaida wazazi au walezi wa mtoto aliyedhalilishwa ndio huzichukua na kuzitumia, jambo kubwa ambalo mtoto yule anaweza kufanyiwa ni kununuliwa kanzu na viatu au suruali na fulana kwa ajili ya siku ya Eid. Khalass!!

Inabidi jamii yetu ibadilike, hawa ni watu wa kufungwa magerezani hawafai hata kukaa katika hizi jamii kwa sababu wataendeleza michezo yao.Waswahili wanasema; ‘paka haachi ungawa’. Yaani paka haachi tabia ya wizi, akishaianza anaweza tu kupumzika lakini kuna siku lazima arudie kazi yake.

Ndio hawa watu, unaanzaje kumficha au kuyasuluhisha kimya kimya. Eti unaogopa uhasama wa kiundugu, kama ni uhasama tayari yeye ameshauanzisha, la msingi vyombo vya sheria vimchukulie tu hatua zinazofaa, kama hataki uhasama asinge najisi na kulawiti watoto wachanga.

Jambo jengine ni usimamiaji dhaifu wa kesi hizi katika vyombo vya sheria, na hili jambo wala halipingiki. Mkuu wa wilaya ya mjini, Unguja mhe Marina Joel Thomas, alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa utetezi katika kuimarisha malezi bora kwa watoto na kupinga udhalilishaji,  uliofanyika katika ukumbi  wa tasisi ya utalii ya SUZA Maruhubi katika kisiwa cha Unguja, alisema;

“imeonekana wazi kuwa vyombo vya sheria (polisi, ofisi ya DPP, mahakama na madaktari) havitendi haki katika kuzipatia ufumbuzi kesi za udhalilishaji hali ambayo inawavunja nguvu walalamikaji”

Mhe Thomas anasema; “mara nyingi wanapata taarifa kupitia vyanzo vya habari vya kuamikia kuwa ushahidi wa kesi za udhalilishaji haujakamilika, upatikanaji wa ushahidi kuchukua muda mrefu kitendo ambacho kinazivunja moyo  familia za waathirika”.

Ikiwa kesi hizi zitakuwa ni za nenda rudi, kunachangia kumchosha hata yule anayetafuta haki yake, hivyo serekali iwe tayari kusimamia kesi hizi ziendeshwe haraka ili aliyedhalilishwa atendewe haki kabla hata machungu ya udhalilishaji hayajamtoka vizuri.

Pia ningeshauri serekali angalau kubadisha sheria kidogo ili hawa wadhalilishaji wasipatiwe dhamana, ni jambo ambalo limewahi kupelekwa katika baraza la Wawakilishi lakini sijui liliishia vipi!

Vitendo vya udhalilishaji vipo juu kwa sasa, inabidi sheria ibadilishwe kwa sababu ya wakati tulio nao, ikiwa huko mbele mambo yatakaa sawa, tunaweza kufanya tena mabadiliko tukarudi kama awali.

Jambo jengine ni elimu. Ni muhimu elimu kutolewa, elimu ya kuwafunza wanawake na watoto jinsi ya kukabiliana na udhalilishaji, kama kile kisa nilichokitoa mwanzo wa makala hii.  Pia hawa wanaume wa jamii yetu na wao wapewe elimu.

Manake kesi nyingi kama sio zote, zinahusisha mwanaume kumdhalilisha mtoto mdogo au kumdhalilisha mwanamke. Viongozi wa dini, wana nafasi kubwa kutoa elimu katika mimbari za misikiti juu ya jambo hili.

Zamani mtoto alikuwa analelewa na jamii nzima, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuadabishwa kwa sababu ya kosa fulani na mtu yeyote hata asiyekuwa Baba au Mama yake, pia watoto walikuwa na ulinzi wa jamii.

Mambo haya siku hizi yametoweka, yameyeyuka katika mitandao ya Facebook na Google, hakuna mtu anajali kuhusu mtoto wa mwengine, kila mmoja na maisha yake.

Ukweli ni kwamba tunapaswa kubadilika ,kesi za udhalilishaji zinachoma moyo ikiwa utazisikia, jamii ikiungana kwa malezi na ulinzi wa viumbe dhaifu vinavyoizunguka,  tutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hili.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja ,ndugu Khamis Kona , hivi karibuni alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari anaseama; licha ya jitihada zinazofanywa na serikali na taasisi katika kupambana na udhalilishaji, bado hali sio shuari katika mkoa huo, kutokana na watoto kuendelea kudhalilishwa”.

Anasema; “kuanzia Januari hadi Disemba 2016 kulikuwa na kesi 126 lakini Januari hadi Oktoba ya mwaka huu kuna kesi 166 nyingi zao zikiwa za kubaka”. Nadhani unaona jinsi ya ongezeko lilivyo, na kumbuka hizo ni takwimu za wilaya moja tu.

Oktoba 16 mwaka huu, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya  Mwanakwerekwe,Unguja , Fatma Muhsini alimuhukumu Almasi Hamid (30) kifungo cha miezi 18 jela kwa kosa la kumuingizia mdomoni uume wake mtoto wa miaka 2.

Miongoni mwa matukio aliyoyasimulia Ofisa Ustawi wa  Jamii ni lile la Oktoba 6 ya mwaka huu, Donge Mchangani, bwana Mcha Juma Juma (23) aliwabaka watoto wawili akiwemo ndugu yake baba mmoja mama mmoja.

Oktoba 16 ya mwaka huu , mtuhumiwa  Ibrahim Said Ali (24) alikamatwa kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto wa miaka mitano.

Nadhani kwa matukio ya namna hii, ambayo yapo mengi,  jamii na serekali ione haja ya kupambana na hawa magaidi wa watoto na wanawake kwa pamoja na juhudi zote.

0657414889