Home Makala Kwanini klabu zinahitaji mkurugenzi wa ufundi?

Kwanini klabu zinahitaji mkurugenzi wa ufundi?

1370
0
SHARE

HASSAN DAUDI

HIVI karibuni, mwekezaji wa klabu ya Simba SC, Mohamed ‘Mo’ Dewji alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo mbali ya mambo mengine, alizungumzia mpango wao wa kuajiri mkurugenzi wa ufundi.

Mo aliwaita waandishi zikiwa ni siku chache kabla ya kurudiana na wababe wa soka la Misri, Al Ahly, katika matanange wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mfumo wa kuwa na mkurugenzi wa ufundi ni maarufu zaidi Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ kwani Bayern Munich, Bayer Leverkusen, Borussia Dortmund, RB Leipzig na Schalke zimekuwa na watu wa aina hiyo.

Je, ni nani huyo mkurugenzi wa ufundi na majukumu yake ni yapi klabuni? Makala haya yanachambua.

Mkurugenzi wa ufundi ni kiungo kati ya kocha mkuu na uongozi wa klabu. Mara nyingi klabu huwatumia wachezaji wao wa zamani. Ni kama walivyofanya Bayern Munich (Hasan Salihamidzic), Leverkusen (Rudi Voller), Dortmund (Michael Zorc), Leipzig (Ralf Rangnick) na Schalke (Christian Heidel).

Huko England nako mfumo huo umeanza kujizolea umaarufu katika miaka ya hivi karibuni, ambapo kuna majina kama Txiki Begiristain (Manchester City), Sven Mislintat (Arsenal) na Michael Edwards (Liverpool), huku Chelsea na Man United zikitarajiwa kuijaza nafasi hiyo siku chache zijazo.

Ikumbukwe kuwa Chelsea haijapata mrithi wa kukalia kiti hicho tangu nyota wao wa zamani raia wa Nigeria, Michael Emenalo, alipoondoka, ingawa kazi zake zimekuwa zikifanywa na mwanamama Marina Granovskaia.

Anayeshika nafasi hiyo hufanya kazi kwa karibu na timu, ikiwamo hata kumshauri kocha baadhi ya mambo ya kiufundi, mfano kuelekea mchezo husika, ukiacha kufikisha matatizo yake kwa uongozi.

“…Huwa nakuwa na timu kwenye mechi, sikosi hata kipindi kimoja cha mazoezi na mara nyingi huwa nakula na wachezaji ili wajue tu kwamba kuna mtu anawafuatilia kwa kila hatua,” anasema mkurugenzi wa ufundi wa Dortmund, Michael Zorc.

Ni jukumu lake kuendesha mikakati ya kusaka vipaji na kushawishi wachezaji wapya wakati wa soko la usajili, ukiweka kando ukweli kwamba hulazimika kukaa mezani na kuwashawishi nyota wanaotakiwa kuongeza mikataba mipya.

 “Ni ngumu kwa makocha wakati wa dirisha la usajili kuweza kuzungumza na kila wakala wa mchezaji anayemtaka.

“Hapo ndipo mkurugenzi wa ufundi anapoingilia kati na kumuepushia mzigo, ili abaki na kazi moja tu ya kufundisha na si kuhangaika kukutana na mawakala,” anasema Zorc.

Anasisitiza kuwa lazima mkurugenzi wa ufundi awe na uelewa mpana wa masuala kusaka vipaji (scouting) ili wachezaji atakaowasajili waweze kuwa na msaada kwa kocha.

“Mkurugenzi wa soka ni yule anayeweza kuwa skauti mzuri, anayejua ubora wa mchezaji…” anaongeza Zorc, kiungo wa kati wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani.

“Huku akiwa na sifa zote za skauti mzuri, si lazima awe anafika moja kwa moja kutazama wachezaji, lakini anapaswa kuwa na jopo lake la maskauti, ambao watakuwa wakimfikishia taarifa za mchezaji anayepatikana,” anasema.

Katika hilo, itakumbukwa kuwa Zorc amejijengea heshima kubwa katika klabu ya Dortmund kwa kuwa ndiye aliyeibua vipaji vya mastaa Robert Lewandowski, Shinji Kagawa na Ousmane Dembele.

Zorc anaongeza kuwa ni kazi ya mkurugenzi wa ufundi wa klabu yoyote kushughulikia suala la wachezaji wasiotakiwa kwenye mipango ya benchi la ufundi.

“Hiyo hufanywa kwa njia tatu; kuwapiga bei, kuwatoa kwa mkopo au kuwatema tu. Hapo, mkurugenzi wa ufundi atasikiliza ofa kutoka klabu zingine na kutafuta ile inayofaa,” anasema.

Kwa maana hiyo basi, wakati kocha akiwa na jukumu la kuongoza, kukinoa na kuchagua kikosi, mkurugenzi wa ufundi hushughulika na masuala yote ya kandanda ndani ya klabu.

“Huwa tunahusika moja kwa moja katika kuendeleza falsafa ya klabu kutoka kwa vijana kwenda kwa timu kubwa,” anasema Zorc na kuongeza:

“Huwa najadiliana na kocha juu ya aina ya uchezaji wa timu ya wakubwa ili hata vijana wa ‘academy’ nao waifuate.”

Aidha, jicho la mkurugenzi wa ufundi kwa wachezaji chipukizi haliishii hapo, bali pia kuwatafutia timu zitakazowapa nafasi za kuonesha viwango vyao. Kwa ushauri wa kocha, inaweza kuwa kwa kuwauza au kuwapeleka kwa mkopo.

Licha ya umuhimu mkubwa wa mkurugenzi wa ufundi, haijasahaulika kuwa nafasi hiyo iliwahi kupondwa na kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, aliposema haoni mantiki yake.

“Mkurugenzi wa ufundi? Sijui inachomaanisha,” alisema Mfaransa huyo, akimaanisha kocha ndiye anayepaswa kuhusika moja kwa moja katika masuala ya kiufundi.