Home Latest News Kwanini Tazania imeshindwa kupeleka mabondia Olimpiki Kushindwa kupeleka mabondia Olimpiki nani alaumiwe?

Kwanini Tazania imeshindwa kupeleka mabondia Olimpiki Kushindwa kupeleka mabondia Olimpiki nani alaumiwe?

805
0
SHARE

NA GEORGE KAYALA,

Tanzania imekuwa na historia ya kujivunia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola. Ushiriki wa Tanzania katika Michuano ya Jumuiya ya Madola ulianza tangu mwaka 1962 katika Michezo iliyofanyika mji wa Perth, Australia.

Historia inaonesha kuwa katika Michezo hiyo iliyofanyika mwaka 1970 mjini Edinburg, Scotland, bondia Titus Simba aliipatia Tanzania medali ya kwanza (fedha) kwenye mchezo wa ngumi katika uzito wa juu(Heavy weight).

Kana kwamba hiyo haitoshi mwaka 1974 michezo hiyo ilifanyika Christchurch, New Zealand ambapo Filbert Bayi aliyekuwa na miaka 21 wakati huo aliishangaza dunia baada ya kushinda Medali ya dhahabu, lakini pia alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 kwa muda wa 3.32.2.

Gidamis Shahanga ni mmoja wa Watanzania walioionesha Dunia uwezo wa wanariadha wa Tanzania pale aliposhinda Medali za Dhahabu katika mbio za masafa marefu (Marathon) huko Edmonton, Canada mwaka 1978. Shahanga aliweka historia ya kuwa mwanariadha pekee Tanzania kushinda Medali nyingine ya dhahabu katika mbio ya mita 10,000 miaka minne baadaye, katika michezo iliyofanyika huko Brisbane, Australia mwaka 1982.

Tanzania iliendelea kung’ara katika michezo hiyo iliyofanyika mjini Kuala Lumpar, Malaysia mwaka 1998, baada ya mwanariadha wa mbio ndefu (Marathon), Simon Mrashani kushinda Medali ya Fedha na Gewey Suja Medali ya Shaba.

Katika upande wa ngumi, bondia Michael Yombayomba naye aliweka rekodi ya aina yake baada ya kupata medali ya dhahabu katika uzito wa juu. Historia ya mashindano hayo inaonesha kuwa mara ya mwisho Tanzania kufanya vizuri kwenye mashindano hayo ni mwaka 2006 ambapo mwanariadha, Samson Ramadhan aliposhinda medali ya dhahabu katika michezo iliyofanyika Melbourne, Australia na Fabian Joseph kupata medali ya Shaba katika mbio za mita 10,000.

Makala haya leo yanaangalia zaidi mchezo wa ngumi ambao miaka ya nyuma ulifanya vizuri. Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) limeshindwa kupata mabondia waliotakiwa kwenda kushiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika Rio, Brazil kuanzia Agosti 5 hadi 21 mwaka huu.

Hii ni aibu kwa viongozi  wa BFT ambao wamedai kushindwa kuwapata mabondia hao kumetokana na ukata uliowanyima fursa wana mwasumbwi hao kwenda kushiriki mashindano ya kufuzu huku ikiitupia lawama Serikali.

Seleman Kidunda ni moja ya mabondia waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo lakini kukosekana kwa maandalizi na michezo ya kutafuta kufuzu kwenda huko kulizima ndoto zake. Mwana masumbwi huyo ni mchezaji wa timu ya ngumi ya Ngome, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ) anacheza uzani wa 69Kg (welter weight).

Kocha wa timu ya Taifa wa masumbwi, Remmy Ngabo alidai Kidunda alikuwa na vigezo vinavyokubalika kushiriki michuano ya Olimpiki mwaka huu kutokana na uzoefu, vilevile ndiye bondia pekee wa Tanzania kwa sasa anayecheza ngumi za ridhaa ambaye amefuzu viwango.

Mwaka 2010, Kidunda alifanikiwa kutwaa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika jijini New Delhi, India. Bondia huyo alifuzu kucheza michuano ya Olimpiki 2012 jijini London, Uingereza, akiwa ni bondia pekee Mtanzania aliyeshiriki michuano hiyo, lakini ndoto yake ya kufanya vizuri zaidi ilikatishwa na Vasilii Belous wa Moldova, aliyempiga kwa pointi katika hatua ya awali.

Kidunda pia alifanikiwa kufuzu mashindano ya dunia yaliyofanyika mwaka 2013 mjini Kazan, Urusi, kabla ya mwaka 2014 kuchaguliwa tena kuwa miongoni mwa wanamichezo wa Tanzania walioshiriki michuano ya Jumuiya ya Madola jijini Glasgow, Scotland.

Mashindano mengine aliyowahi kushiriki ni michuano ya ‘All Africa Games’, iliyofanyika Msumbiji. Ni muda mrefu sasa BFT imeshindwa kuipeleka timu katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Shirikisho hilo lilishindwa kupeleka mabondia katika mashindano ya ndondi ya Afrika yaliyofanyika Cassablanca, Morocco na baadae yale ya dunia yaliyofanyika Doha, Qatar.

Pia, mabondia wa Tanzania walishindwa kupata viwango vya kufuzu baada ya kudundwa katika Michezo ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika Brazzaville, Congo mwaka jana. Katika hali ya kushangaza mabondia hao walishindwa kwenda Younde, Cameroon kusaka nafasi ya kupata kigezo cha kufuzu michuano ya Olimpiki iliyofanyika Machi 9 hadi 20 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alieleza kuwa kukosekana kwa ufadhili ndiko kulikosababisha washindwe kuwapeleka mabondia hao kwenye mashindano ya kufuzu kwa michuano hiyo jijini Yaounde Cameroon.

Kwa muda mrefu uongozi wa BFT umekuwa ukiahidi kupeleka mabondia katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, lakini muda unapofika wamekuwa wakishindwa kupeleka timu hiyo. Uongozi huo tangu uingie madarakani miaka mitatu iliyopita, haijawahi kupeleka timu ya taifa katika mashindano ya kimataifa kama yale ya Afrika au dunia kutokana na kutokuwa na fedha.

Wachambuzi wa michezo nchini wamewataka viongozi hao wajitathimini iwapo wanafaa kuendelea kuongoza ama la, kwani hata katika Olimpiki iliyofanyika London mwaka 2012, Tanzania ilipeleka bondia mmoja tu, Selemani Kidunda baada ya wengine kushindwa kufuzu.

Katibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusisitiza hali hiyo inatokana na ukata unaoviandama vyama vingi vya michezo ikiwemo BFT, hivyo kuitaka serikali kubeba mzigo huo.

Katika michezo ya Olimpiki Tanzania inatarajiwa kuwakilishwa na wa wanamichezo saba tu ambapo wanariadha ni wanne, waogeleaji wawili na mchezaji wa juzdo akiwa ni mmoja.