Home Makala Kwenye hili la korosho, kongole Tizeba

Kwenye hili la korosho, kongole Tizeba

3048
0
SHARE

MUDHIHIR M. MUDHIHIR

Hongera nyingi kwako Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Dk. Charles Tizeba. Hatimaye umetambua kwamba njaa haimalizwi kwa funda la maji wala kiu haikongwi kwa tonge la ugali.

Hatua uliyoichukua kukutana na wabanguaji wa korosho wadogo, wakati na wakubwa ili kutambua matatizo na changamoto inahitaji kuungwa mkono.

Ulikuwa sahihi kuhoji ni kwanini Msumbiji wanabangua asilimia 40 ya korosho zao wakati sisi hatukaribii hata asilimia 10!Hao uliokutana nao wanalo jawabu, kwani Msumbiji wana nini na sisi tunakosa nini tushindwe.

Zipo sababu zinazodumaza ubanguaji wa korosho nchini na zipo sababu zinazohamasisha uuzaji wa korosho ghafi nje ya nchi.

Nakupa hongera Tizeba kwa sababu ubanguaji wa korosho hapa nchini utatuletea tija teletele.

Tutakuza ajira kwa Wataznania, tutaliongezea thamani zao la korosho, tutaimarisha utulivu wa soko na kudhibiti kuyumba kwa bei. Hapana ubishi kuwa kuuza malighafi nje ya nchi kunatokana na kasumba ya uchumi wa kikoloni kuliko visingizio vya uwezo wetu mdogo wa kuchakata malighafi hizo.

Waziri tunao wabanguaji wadogo mmoja mmoja na wengine katika vikundi ambao ingawa hawana misaada ya kibenki au serikali kupitia Bodi ya Korosho, wanabangua kwa viwango vya kuridhisha. Tunavyo vikundi vya wabanguaji wadogo kama vile WAKORU (Ruangwa), DEMROS (Tanga), UVUKI (Kibaha), Kitama (Tandahimba) na vingine vingi. Dk. Tizeba ubanguaji Tanzania unawezekana.

Viwanda vya wabuanguaji wadogo vikishikwa mkono na serikali vina uwezo wa kubangua hadi tani tano za korosho ghafi kwa siku. Kikundi kinahitaji sh. milioni 10 kununua ‘boiler  na cooker’ yake kwa ajili ya kuchemshia korosho na kinahitaji wastani wa shilingi 440,550 kununua seti moja ya kukatia korosho (advanced cutting machine), milioni 15 zinakidhi pamoja na vifaa vingine vidogo vidogo.

Viwanda vidogo vya aina hii nchini India vipo zaidi ya 2000 na viwanda vikubwa humalizia kazi ya ufungashaji na nembo (packaging and branding).

Fedha za ushuru wa kusafirisha korosho ghafi (export levy) zinaweza kutumika kama ‘revolving fund kukopesha vikundi vitakavyojiunga kama vyama vidogo vya ushirika.

Serikali ikijipanga vizuri zinaweza kununuliwa boiler na cooker kubwa zitakazochemsha korosho za vikundi kadhaa na hivyo kupunguza gharama za utitiri wa vi-boiler vidogovidogo kwa kila kikundi.

Wataalamu kutoka wizara ya Fedha, Kilimo, Bodi ya Korosho na Tume ya Ushirika wakiketi pamoja wataipata namna bora ya kuliendea suala hili.

Zipo changamoto zinzohitaji kufanyiwa kazi. Kwa vikundi vya wabanguaji vinavyotokana na wakulima tatizo la upatikanaji wa korosho si kubwa, lakini wabanguaji wadogo wasio na mashamba ya korosho wanalo tatizo la mtaji wa kununua korosho pamoja na tatizo la kushindana na wafanyabiashara wakubwa mnadani. Changamoto hii inahitaji kufanyiwa kazi.

Zipo changamoto zinazotokana na matakwa ya kiutawala kama vile kanuni za TFDA, OSHA, Zimamoto na Baraza la Mazingira. Fimbo za wakubwa huwa hazitambui uwezo wa watoto wanaosimama dede wala wanaotembea tete. Kwa mwenendo huu wabanguaji wadogo hasa wale wakulima vijijini hawawezi kusonga mbele. Mimi siamini hata kidogo kuwa ati hamna namna za kuwashika mkono wabanguaji wadogo na wa kati.

Ikiwa vibanda vya mama lishe, vihoteli vya mitaani, wakaanga chips, samaki na mihogo nao wanahusika na vyakula vya wanadamu, kwa nini masharti ya viwango vya vyakula na mazingira yang’ate zaidi kwenye korosho tu? Au tatizo ni hili jina la kiwanda? Mashamsham haya hatuyaoni kwenye vibanda vya kukoboa na kusaga nafaka.

Sisemi kwamba vyombo hivi vilivyoundwa kisheria na vinavyofanya kazi muhimu ya kulinda afya ya walaji na bidhaa za nchi yetu, na vinavyolinda wafanyakazi na mazingira yake, visitimize wajibu wao. Hata kidogo! Ninachosema ni kuviomba vyombo hivi vijishughulishe kidogo ili vione sababu na namna ya kutunisha misuli yao.

Japo wapo wanaosema kwamba soko la korosho zilizobanguliwa nalo ni changamoto, binafsi nasema hapana. Soko bado ni kubwa hapa ndani, Afrika Mashariki, nchi za SADC na huko duniani. Masuala ya soko yasitutie hofu kiasi cha kututoa nje ya shabaha yetu ya kuliongezea thamani zao la korosho. Tukaze buti hakuna kurudi nyuma.

Changamoto kubwa tuitarajie kutoka kwa wabanguaji wakubwa duniani. Kwao wao ubanguaji wa korosho ni chanzo cha uhakika cha ajira kwa raia wao. Ni chanzo kikubwa cha mapato ya ndani na chanzo muhimu cha fedha za kigeni. Korosho zetu ndiyo bora zaidi duniani, na wao miaka nenda miaka rudi ndiyo wanunuzi wa korosho zetu ghafi. Hawatokaa kimya, tujiandae.

Siishi kujiuliza kwa nini waliouziwa viwanda vyetu vya kubangua korosho hawabangui. Halafu ni kwa nini miongoni mwao ni wanunuzi na wasafirishaji wakubwa nje ya nchi korosho ghafi. Najiuliza pia kwa nini tozo ya kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi (export levy) haileti matarajio yetu ya kuimarika ubanguaji hapa nchini. Maswali haya yanayo majibu.

Hapana! Hatuna sababu ya kuendelea kuuza nje ya nchi korosho zetu ghafi. Waziri Tizeba umefanya jambo jema kukaa meza moja na wabanguaji wa korosho ili kujua kulikoni. Picha inayonijia kichwani ni ile ya wewe  Waziri Tizeba kuambiwa kuwa ubanguaji korosho hapa nchini hauwezekani. Kutamani kubangua korosho hapa nchini ni kutangaza vita ngumu ya kiuchumi.

Kukutana na wabanguaji korosho ni kama kupeleka sampuli za mgonjwa wako maabara. Utayatambua matatizo yanayomsibu mgonjwa wako. Je, utaishia hapo? Hapana! Yafikishe matokeo ya maabara kwa jopo la madaktari. Mheshimiwa Waziri madaktari wako ni wataalamu wako. Ni suala la uamuzi tu ndilo litakalofanikisha ubanguaji wa korosho zetu.

Kikao chako Waziri Tizeba na wabanguaji wa korosho hapa nchini si jaribio la kwanza. Yamekuwapo majaribio kadhaa ambayo hayakuzaa matunda. Tunahitaji kufanya uamuzi kama tulivyofanya wakati wa kuanzisha viwanda hivi wakati wa awamu ya kwanza. Tuwasikilize wabanguaji, tuwashike mkono na tuweke dhamira, ubanguaji unawezekana Tanzania.

Katika hoja zangu humu utaona Mheshimiwa Waziri kuwa sikujielekeza sana kwa wabanguaji wakubwa. Nimefanya hivyo kwa kutambua kuwa hawa wakitaka na wakiamua kubangua korosho wanaweza kufanya hivyo. Serikali inahitaji tu kuwa karibu nao kwa ajili ya mashauriano katika kuzikabili changamoto zitakazokuwa zinaibuka hapa na pale. Mitaji si suala gumu sana kwao.

Nimejielekeza sana kwa wabanguaji wadogo kwa sababu kwanza wanayo nafasi kubwa na muhimu katika kufanikisha dhamira ya ubanguaji korosho na kuwaongezea kipato. Pili, kuanzisha vikundi hivi, kuviwezesha visimame na viwe endelevu vinahitaji utashi wa serikali. Waziri Tizeba umeonyesha nia na wataalamu hawana budi wakuunge mkono.

Bodi ya Korosho na Tume ya Ushirika ni wasaidizi wako wakuu katika suala hili. Kwa sisi tuliokaribu na vyombo hivi tunaziona ishara za mvutano usio na tija. Watanzania hatuhitaji kufahamu ni nani mkubwa kati ya hawa wawili. Tunachohitaji ni mahusiano yenye afya yatakayowezesha utendaji wa pamoja katika kuleta ustawi wa Tasnia ya Korosho nchini.