Home Uchambuzi Afrika Kwenye siasa EAC inakosa umuhimu

Kwenye siasa EAC inakosa umuhimu

2446
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Wakati Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) inaanzishwa (1975) kulikuwapo jumuiya nyingine kubwa ya kikanda upande wa mashariki – Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) iliyoanzishwa miaka minane kabla’

Kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa ECOWAS kulisukumwa na uwepo wa EAC kwani nchi za magharibi mwa Bara la Afrika waliona umuhimu wa kuwa na chombo cha ushirikiano baina yao – hasa kiuchumi na masuala mengine.

Lakini matumaini ya ECOWAS kuifanya EAC kama dira yao yalipata pigo kubwa pale EAC ilianza kuugua na hatimaye ikafa miaka miwili baadaye. Jumuiya hiyo ilikuwa ya kipekee kabisa duniani, kimuundo na kiutendaji kwani ushirikiano baina ya nchi hizo ulikuwa mkubwa na wa karibu mno kuliko hata uliopo ndani ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) sasa hivi.

Mbali na kuendesha kipamoja mashirika ya kutoa huduma kama vile usafiri wa reli, ndege, shughuli za posta na simu na uendeshaji wa bandari, pia kulikuwapo mahakama moja ya rufaa kwa nchi zote tatu – Court of Appeal for East Africa – na uendeshaji wa kipamoja taasisi kadha nyingine kama vile za utafiti wa malaria, uvuvi na uthibiti wa wadudu waharibifu wa mimea.

Ilikuwa ni kazi ngumu kuvunja jumuiya yenye mshikamano kama ule, lakini siku zote wanasiasa si watu wa kuchezea hata kidogo. Matarajio ya wengi yalikuwa ni kwa Jumuiya hiyo kukua, siyo kufa. Hata hivyo ilifufuka tena miaka 23 baadaye (2000) ingawa tofauti kimfumo na kimkakati kuliko ile ya awali ingawa umbo na ukubwa ulikuwa ule ule.

Na baadaye zikaongezeka nchi za Burundi na Rwanda (2007) katika Jumuiya hiyo na mwaka 2016 Sudan ya Kusini nazo zilijiunga, pamoja na matatizo yao yote hususan yale ya kisissa.

Mapema mwa miaka ya mwanzo ya Milenia  aliyekuwa Katibu Mkuu wa EAC Amanya Mushegga wa kutoka Uganda aliwahi kusema kwamba iwapo Burundi na Rwanda wangeruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ile ya zamani na kwamba Jumuiya hiyo isingeachiwa kuvunjika mwaka 1977, matatizo ya kikabila yasingejitokeza katika nchi hizi mbili na kwamba hata mauaji ya kimbari ya Rwanda yasingetokea mwaka 1994.

Lakini kauli hiyo ilikuwa ni ya kufikirika tu kwani mwaka 2007 Rwanda na Burundi zilijiunga na Jumuiya (ya sasa) lakini bado hii haijasaidia kutuliza migongano ya kikabila na ya kisiasa ndani ya nchi hizo, hususan Burundi.

Hii ni pamoja na miaka kadha iliyopita kuanzishwa kwa mkataba wa pamoja (Protocol) wa kusimamia masuala ya utawala bora na utoaji wa maamuzi ya haraka kuhusu masuala ya migogoro ya siasa, masuala ambayo yalitajwa kuwa muhimu katika ajenda ya ushirikiano wa kisiasa (political integration agenda) wa nchi hizi.

Haya yalitarajiwa kutoa suluhisho la kudumu katika uendeshaji wa chaguzi – suala nyeti kwa nchi zote wanachama. Kwa mfano Ibara ya 2 na 3 ya Mkataba huo yalizitaka nchi wanachama kudumisha misingi ya demokrasia, kusimamia utawala wa katiba na kufanya chaguzi zilizo huru na haki na katika kubadilisha serikali kwa njia ya amani.

Je haya yanatokea? La hasha, migogoro ya kisiasa kuhusiana masuala ya uchaguzi yamekuwa ya kawaida katika kila nchi na hakuna nchi nyingine inyoweza kumnyooshea kidole mwenzake – eti kufanya hivyo ni kuingilia masuala ya ndani. Sasa ile Protocol iliyosainiwa ina maana gani iwapo inavunjwa na takriban kila nchi?

Migogoro na ghasia wakati na baada ya chaguzi kutokana na chaguzi zisizo huru yamekuwa ni masuala ya kawaida. Tanzania pia ina sehemu yake ya siasa haribifu pamoja na majigambo ya majukwaani kwamba ni kisiwa cha amani katika bahari ya machafuko.

Mfano mmoja ni suala lilitokana na kufutwa ghafla kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar mwaka 2015 yaliyoonyesha kuupa ushindi upinzani ni mfano mmoja. Pengine mgogoro huo haukufikia kiwango cha kutaka kuingiliwa na viongozi wengine wa Jumuiya, lakini mbegu mbaya imeshapandwa na huko tuendako Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye.

Nimeleta habari ya hali ilivyo ndani ya jumuiya yetu ya EAC kwa lengo la kulinganisha na ile ya wenzetu ECOWAS. Pamoja na jumuiya hiyo kuwa na nchi wanachama wengi zaidi (15) kuliko sisi, lakini wamepata mafanikio makubwa katika masuala ya kukuza na kulinda demokrasia miongoni mwao. Wamekuwa na uthubutu mkubwa wa kuonyeshana kidole kwa kiongozi yoyote anayekwenda kinyume.

Mwaka 2016 kwa mfano, ECOWAS iliingilia kati mgogoro wa kisiasa nchini Gambia uliotokana na uchaguzi uliofanyika ambapo Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Adama Barrow, mgombea wa upinzani kuwa mashindi.

Aliyekuwa mtawala wa kidikteta wa nchi hiyo kwa miaka 22 Yahya Jamme baada ya awali kukubali kushindwa, baadaye alibadili uamuzi huo na kutaka kubakia madarakani.

ECOWAS ilifanya juhudi kubwa, pamoja na kuandaa majeshi ya kuivamia nchi hiyo ndipo Jamme alikubali kuyabwaga madaraka na kuondoka nchini humo. Aidha ECOWAS imewahi kuingilia kati migogoro ya kisiasa katika nchi nyingine kadha hata ile iliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi kama vile Sierra Leone, Liberia, Ivory Coast na Mali.

Katika migogoro ya nchi hizo ECOWAS ilitoa msukumo wa kipamoja kutoka nchi wanachama na kuweza kuwang’oa viongozi ambao walikuwa wamepora demokrasia baada ya uchaguzi. Ivory Coast kwa mfano, nguvu za wanachma wa ECOWAS zilifanikiwa kumpeleka mporaji wa demokrasia Laurent Gbagbo katika Mahakama ya ICC kule The Haig, Uholanzi.

Matunda ya jitihada za namna hii zinaanza kupatikana – mfano katika chaguzi katika Nigeria na Ghana ambapo marais waliokuwa madarakani (incumbents) walioshindwa walikubali kushindwa. Au tuseme kutokana na hofu ya kile kinachoweza kutokea dhidi yao viongozi wa nchi za Jumuiya hiyo wameanza kujenga utamaduni wa kutowaza kuendesha chaguzi za hadaa ili kujipatia ushindi. Wameanza kuogopa.

Maeneo mengine ya Bara la Afrika pamoja na mashariki mwa Bara hilo bado viongozi wanaendeleza utamaduni wa chaguzi za hadaa na usanii mtupu ili kuendelea kubaki madarakani – kama si wao wenyewe, basi vyama vyao. Masuala ya jumuiya kama EAC kuwaingilia kati – tupa kule.