Home Latest News LALA SALAMA YA LIGI KUU UMAKINI UNAHITAJIKA

LALA SALAMA YA LIGI KUU UMAKINI UNAHITAJIKA

1451
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

HATIMAYE Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara unaanza mwishoni mwa wiki hii kwa timu zote 16 kupigana kufa na kupona kuwania taji la michuano hiyo.

Toka kusimama kwa mzunguko wa kwanza Novemba mwaka huu, kila timu imejidhatiti kwa kutumia vema dirisha dogo kufanya usajili kwa ama kuzipa mapungufu au kuboresha idara zao ili kuongeza ushindani katika mzunguko wa lala salama unaotarajiwa kufikia tamati Aprili mwakani.

Kama ilivyo kawaida mzunguko wa pili huwa ni mgumu ukilinganisha na ule wa kwanza kutokana na ukweli kuwa kunakuwepo na ushindani zaidi katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linalohusisha timu zinazowania ubingwa ambapo kuanzia hatua hii ushindani na mvutano huwa ni mkali zaidi na timu yoyote itakayofanya makosa basi inakuwa ndiyo imeondolewa katika ushindani halisi wa mbio hizo.

Katika mpambano wa kundi hilo timu za Simba inayoongoza Ligi kwa pointi 35 ikifuatiwa na Yanga (pointi 32), Azam (pointi 25), Kagera (pointi 24), Mtibwa (pointi 23) na Stand (pointi 22).

Timu hizi zinapewa nafsi kubwa kutokana na mazingira halisi yanayozizunguka sambamba na historia yenyewe ya michuano inayoonesha kwamba miamba hizo mitatu ndiyo inayotoana jasho takribani misimu mitatu sasa ikipambana yenyewe kwa yenyewe katika hatua hii.

Ukiacha mbio za ubingwa, ushindani mwingine upo katika timu zinazopigana kuepuka kushuka daraja. Hapa timu kama Toto (pointi 12), Mwadui na JKT Ruvu (pointi 13), Majimaji na Mbao (pointi 16), African Lyon (poiti 17) ndizo zenye hatari zaidi hivyo zinatakiwa kujidhatiti ili zijihakikishie usalama wa kubaki ligi kuu msimu ujao.

Mazingira ya Ligi hiyo kwa muda mrefu yanaonesha kuwepo kwa wakati mgumu zaidi katika kipindi hiki kuliko kingine chochote kuanzia wka wachezaji, viongozi, makocha mpaka waamuzi ambao vitu kama malalamiko ni vigumu sana kutosikia yakitolewa.

Lakini pia ‘rafu’ miongoni mwa timu husika zimekuwa ni jambo la kawaida sana kuzisikia achilia mbali shutuma nzito za rushwa na upendeleo kwa waamuzi.

Shutuma za rushwa miongoni mwa timu zenyewe, waamuzi na hata viongozi zimulikwe kwa kuchunguzwa na hatimaye hatua zichukuliwe iwapo itabainika kuna namna iliyofanyika.

Zipo baadhi ya timu hupenda kufanya propaganda ili mradi tu kuvuruga utaratibu na mfumo wa uendeshaji wa michuano hao wanapaswa kuwekewa makakati wa kudhibitiwa.

Matukio yenye utata, malalamiko na rufaa vyote vinapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka na ndani ya muda muafaka ili kutoweka mazingira ya upendeleo miongoni mwa timu shiriki.

Katika mzunguko wa kwanza tatizo hilo lilionekana sana kiasi cha kuzua malalamiko na hata kutaka kuvuruga sura ya michuano likiwemo suala la usajili wa mchezaji Ramadhani Kessy aliyetua yanga akitokea Simba. Vilevile sakata la mwamuzi Martin Saanya aliyevurunda pambano la watani wa jadi kati ya Yanga na Simba Oktoba mwaka huu.

Matukio hayo pamoja na mengine kadhaa yalipaswa kuamuliwa na kutolewa maamuzi kwa wakati lakini katika hali ya mshangao yalicheleweshwa hivyo kuzusha malalamiko yasiyokuwa na msingi iwapo maamuzi yangefanyika kwa wakati.

Ili kutoitia doa michuano hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi (TPBL) wanapaswa kuwa makini na hata kukunjua sasa makucha yao waliyoyaficha kwa muda mrefu ili kuhakikisha michuano inamalizika katika ngwe hii ya lala salama bila ya kupindishwa kwa sheria au kanuni.

Hiyo itaiweka salama michuano yenyewe pamoja na kupunguza malalamiko kwa vile haki itakuwa imepatikana kwa kila mdau anayehusika katika mchezo huo khakikisha ametimiza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Uimarishwaji wa usalama ndani ya viwanja vya soka pia utaifanya michuano kufanyika na kumalika katika hali inayotakakiwa kwa mujibu wa sheria.

TPLB pamoja na TFF hatakwepa lawama kwa uzembe wowote unaoweza kujitokeza na uvuruga haki ya kupatikana bingwa sahihi sambamba na timu zitakazoshuka daraja.