Home Michezo Lampard kufuata nyayo za Guardiola, Solskjaer?

Lampard kufuata nyayo za Guardiola, Solskjaer?

1545
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WAKAII wa usajili wa majira ya kiangazi, mwaka jana, Chelsea walikuwa ‘bize’ kusaka mrithi wa kocha Antonio Conte na ni Muitalia mwenzake, Maurizio Sarri, ndiye waliyekuwa wakimtaka.

Kipindi hicho, Sarri alikuwa mkuu wa benchi la ufundi wakati Napoli ikisifika barani Ulaya kwa soka lake la kuvutia.

Mwishowe, Sarri alitua Stamford Bridge, huku kiti chake kule Napoli kikikaliwa na Carlo Ancelotti, ambaye naye aliwahi kuinoa Chelsea kabla ya kutimuliwa.

Msimu huu ulipoanza, ilionekana Chelsea wamelamba dume kwa kumchukua Sarri kwani timu ilikuwa kwenye kiwango cha juu, ikishinda mechi nne kati ya tano za awali.

Hata hivyo, upepo ulibadilika ghafla baada ya kupoteza mechi yao ya kwanza kwenye ligi dhidi ya Tottenham pale Wembley. Tangu walipotandikwa mabao 3-1 siku hiyo, Blues wakapotea rasmi.

Kocha Sarri amekuwa akikosolewa kwa mbinu zake, hasa uamuzi wake anaoutaja kuwa wa kiufundi, kumng’ang’ania Jorginho kwenye eneo la kiungo wa ulinzi badala ya N’Golo Kante.

Kilichowauma zaidi mashabiki wa Blues na hata kuanza kushinikiza Sarri afungashe virago vyake, ni kichapo cha hivi karibuni cha mabao 4-0 kutoka kwa Bournemouth.

Ikizingatiwa kuwa bilionea wa klabu hiyo, Roman Abramovich, si mmoja kati ya wamiliki wenye subira pale timu inapofanya vibaya, ni wazi haitachukua muda mrefu kabla ya kocha huyo kufukuzwa.

Isisahaulike kwamba ni wakati huu, ambapo kuna orodha ndefu ya makocha wanaotajwa kwenda Stamford Bridge kuchukua mikoba itakayoachwa na Sarri.

Je, Abramovich atamchukua Thomas Tuchel anayeinoa PSG, Diego Simeone wa Atletico Madrid, Laurent Blanc aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa, au Zinedine Zidane?

Wakati majina hayo yakiendelea kugonga vichwa vya habari huko Ulaya, yakihusishwa na ulaji atakaouacha Sarri, wachambuzi wa soka barani humo wanaamini ni zamu ya Frank Lampard.

Kama ambayo Pep Guardiola aliichezea Barcelona na kisha kwa kukabidhiwa benchi la ufundi, nafasi iliyomfanya kuwa mmoja kati ya makocha bora duniani, ni wakati mwafaka kwa Lampard kuaminiwa Stamford Bridge.

Ikiwa Manchester United wameweza kumpa nafasi mkongwe wao, Ole Gunar Solskjaer, na sasa timu hiyo inafanya vizuri chini yake, kwanini Lampard ashindwe kuibeba Chelsea?

Licha ya kutokuwa na jina kubwa kwenye kazi ya ukocha, Lampard ameianza vizuri taaluma hiyo akiwa na Derby County ya Ligi Daraja la Kwanza England (Championship).

Si tu timu hiyo inayocheza soka la kushambulia ina nafasi kubwa ya kutinga Ligi Kuu, ukiachilia mbali kwamba tayari nayo imeingia raundi ya tano ya Kombe la FA.

Kama alivyofanya Guardiola na sasa Solskjaer, ni kweli Lampard hawezi kuwa na uzoefu wa kufundisha soka lakini heshima kutoka kwa wachezaji itatokana na mafanikio yake makubwa akiwa mchezaji wa Chelsea.

Mataji 13, yakiwamo manne ya Ligi Kuu, mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Chelsea, ni sehemu ndogo tu ya mafanikio yatakayowafanya wachezaji wenzake wamheshimu.

Katika hilo, ilikuwa hivyo kwa Zinedine Zidane pale Real Madrid. Wakati anapewa kazi, hakuwa ameinoa timu yoyote ya Ligi Kuu lakini alipeleka mafanikio makubwa Santiago Bernabeu.

Hadi anaondoka mwishoni mwa msimu uliopita, alikuwa ndiye kocha pekee katika historia ya Madrid kuipa klabu hiyo mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kama hiyo haitoshi, bado inakumbukwa namna Roberto Di Matteo alivyoipa Blues taji la Ligi ya Mabingwa katika mazingira ambayo hakuna aliyekuwa akitarajia. Hakuwa mzoefu lakini wachezaji waliokuwa chini yake waliuheshimu ukongwe na mafanikio yake katika soka.