Home Makala Kimataifa LIBERIA KIMBILIO LA WAKIMBIZI WEUSI KUTOKA UTUMWANI

LIBERIA KIMBILIO LA WAKIMBIZI WEUSI KUTOKA UTUMWANI

3475
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Nchi ya Liberia iliyoko magharibi mwa pwani ya Afrika ilianzishwa katikati ya karne ya 19 kama maskani ya watumwa waliokuwa wakirudi Barani, wakikimbia adha za utumwa kule Marekani.

Labda, kwa wakati ule, haikuwa inashangaza sana pale Katiba ilipoundwa na kipengele kuwekwa kilichodhibiti suala zima la uraia – kwamba raia watakuwa ni wale tu wa asili ya Afrika na hapo hapo kuanzisha ‘taifa la wakimbizi weusi walioachiwa kutoka utumwani.’

Miaka mia kadha baadaye, Rais mpya wa Liberia George Weah, ameielezea kanuni hiyo kuwa siyo ya lazima, ni ya kibaguzi na haifai kwa hali ya sasa.

Zaidi ya hayo, Weah amesema ubaguzi kwa misingi ya rangi ya mtu “inakiuka tafsiri halisi ya ‘Liberia’ yenyewe” neno ambalo lilitokana na neno la Kilatini ‘liber’ – likimaananisha “uhuru.” Tangazio hili limekuja kwa mshtuko mkubwa katika baadhi ya maeneo ya Liberia.

Mfanyabiashara mmoja Rufus Oulagbo aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC katika mahojiano kwamba sasa “watu weupe watawafanya watu weusi kuwa watumwa.”

Oulagbo ana hofu kwamba kupanua wigo wa uraia kutoka kwa ule wa ‘watu weusi’ pekee kutawaharibia Waliberia fursa ya kuiendeleza nchi yao na hasa hasa anataja kwamba hatua hiyo itatoa ruhusa kwa watu wa nje kumiliki mali nchini humo, kitu ambacho alisema ni hatari.

Oulagbo hayuko peke yake katika hofu hiyo. Kikundi kipya cha utetezi kiitawacho ‘Citizen’s Action Against Non-Negro Citizenship and Land Ownership,’ tayari kimeanzishwa kupambana na mpango huo wa Rais Weah.

“Kila nchi ina misingi yake iliyojengewa – na kama utaidhoofisha misingi hiyo, taifa litaangamia kwa hakika,” kiongozi wa kikundi hicho Fubbi Henries aliiambia BBC.

Amesema Weah anatakiwa azingatie sera sahihi kwa Walaiberia. Ameongeza: “Sasa hivi lengo kuu ni namna ya kuirudisha hali ya kibiashara, kilimo na elimu katika njia zake, na siyo suala la umiliki wa ardhi kwa watu wasio weusi.”

Pamoja na utajiri wake wa maliasili, Liberia ni nchi ya 225 miongoni mwa nchi 228 linapokuja suala la pato la kila mwananchi (GDP per Capita) – chini ya Dola za Kimarekani 900 tu mwaka 2017.

Kwa kulinganisha, takwimu kwa nchi ya Marekani ilikuwa Dola 59,500 na Uingereza Dola 43,600. Ukweli ni kwamba theluthi moja ya pato (GDP) ya Liberia inatokana na watu waishio nje ya nchi hiyo, huku famila kadha zikitegemea matumizi yao yote kutoka kwa jamaa zao waishio Marekani.

Hata hivyo Rais Weah amekuwa mkweli katika suala zima la uchumi wa nchi, kwani ametamka bayana kwamba “nchi imefilisika, na amepania kuirekebisha hali hiyo.”

Baada ya miaka mingi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, bila kuacha kutaja athari iliyoletwa na janga la ugonjwa wa Ebola mwaka 2014, ahadi hizi zinawapa matumaini makubwa wananchi.

Lakini wadadisi wa mambo wanasema kubadili sheria sasa hivi itakuwa kama vile kumuweka mtoto wa miaka miwili (Walaiberia) na mtu wa miaka 45 (watu wa nje) katika ulingo wa masumbwi na kuangalia iwapo watapigana kwa usawa.

“Hakika atafaidika dhidi ya mtoto Yule kwani wafanyabiashara wa Liberia hawako sawa na wale wa nje,” wadadisi wanasema.