Home KIMATAIFA LIBERIA KUINUKA AU KUANGUKA TENA OKTOBA

LIBERIA KUINUKA AU KUANGUKA TENA OKTOBA

664
0
SHARE

MONROVIA, LIBERIA


Oktoba 10, mwaka huu  Liberia itafanya uchaguzi ambao unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa katika historia ya nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi, huku hakuna anayeweza kutabiri matokeo yake.

Katika uchaguzi huu wananchi wa Liberia watamchagua rais mpya pamoja na wabunge kutoka orodha ya wagombea ambao miongoni mwao ni wapya kabisa katika medani ya kisiasa.

Huu utakuwa ni uchaguzi wa tatu tangu kumalizika kwa vita haribifu ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka 14. Uchaguzi wa kwanza ulikuwa 2005 na ulikuwa wa kihistioria pia kwani ulikuja baada ya takriban karne moja ya utawala wa chama kimoja uliofuatiwa na miongo kadha ya mapambano ya madai ya demokrasia ya vyama vingi.

Katika uchaguzi huo nyenzo za taifa ziligawiwa sawa kwa vyama vyote vilivyogombania huku ghasia na wizi wa kura haukuwapo. Matokeo yake pia yalikuwa ya kihistoria, kwani wakati Liberia ilikuwa inaponesha vidonda vya vita ya wenyewe kwa wenyewe, mshindi alikuwa ni mwanamke, Ellen Johnson Sirleaf ambaye alishinda katika uchaguzi wa marudio na hivyo kuwa rais wa kwanza mwanamke Barani Afrika.

Na katika mabunge yote mawili – Senate na Baraza la Wawakilishi hakuna chama kilichoweza kupata uwingi wa kufanya maamuzi kipekee. Hata hivyo kuliibuka maswali kwamba fedha za kufanyia kampeni zilitoka wapi. Lakini kwa ujumla ulikuwa ni uchaguzi uliofanyika kwa uhuru na utulivu kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika nchi nyingi Barani Afrika.

Katika uchaguzi wa 2011 Sirleaf aligombea tena na kuwepo kwake madarakani (incumbency) kulimsaidia sana. Alishinda tena katika uchaguzi wa marudio ambao upinzani ulisusia kwa madai ya kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika kura ya awali. Chama cha Sirleaf kiliongeza uwakilishi wake katika Baraza la wawakilishi kwa asilimia 300 na katika Senate kwa asilimia 200.

Sasa hivi, miaka sita baadaye ni wakati kwa wananchi wa Liberia kupiga kura tena. Baada ya vipindi vyake viwili vya miaka sita-sita, Sirleaf anatakiwa kuachia madaraka kufuatana na katiba na hivyo kuacha ombwe kubwa la kisiasa.

Hii ina maana Liberia itakuwa na rais mpya na kuna takriban wagombea 20 wanaowania nafasi hiyo. Kuna wachache ambao ni sura zile zile za zamani ambazo zimeibuka baada ya kutoweka kwa muda mrefu. Na kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita, safari hii pia kunatarajiwa kuwa na kura ya marudio katika kinyang’anyiro cha urais.

Uchaguzi wa mwaka huu unakuja wakati nchi inakabiliana na changamoto nyingi. Kiuchumi, usimamizi mbovu umesababisha mapungufu katika bajeti za serikali na mfumuko mkubwa wa bei.

Balaa la ugonjwa wa Ebola la 2014/15 na kuanguka kwa bei za madini ya chuma (iron ore) na la zao la mpira katika soko la dunia limesababisha kudorora kwa uchumi.

Kipindi cha kwanza cha Sirleaf kilionyesha kuongezeka kwa uchumi wa silimia 5-8 kutokana na ongezeko la mapato ya bidhaa zilizosafirishwa kwenda nje. Lakini pamoja na maendeleo haya, wananchi wengi wa Liberia walibakia katika dimbwi la umasikini na asilimia 64 wakiishi chini ya mstari wa umasikini (below poverty line).

Mgombea urais wa chama cha Sirleaf ni makamu wa rais wake mtiifu, Joseph Boakai ambaye amepata uteuzi huo baada ya kinyang’anyiro kikali. Mgombea mwenza wake ni Spika wa baraza la wawakilishi, Emmanuel Nuquay.

Kwa upande wa upinzani, mcheza mpira nyota wa zamani George weah wa chama cha cha Coalition for Democratic Change (CDC) ndiye anayeonekana kuwa na nguvu. Alikuwa ni mgombea urais katika uchaguzi wa marudio mwaka 2005 ma mgombea mwenza wa chama chake katika uchaguzi wa marudio wa 2011.

Sifa zake za uchezaji mpira zinamfanya kuwa kipenzi hasa kwa vijana, na huko nyuma aliwahi kupata uungwaji mkono mkubwa katika jiji la Monrovia – mji mkuu wa nchi hiyo na pia katia eneo lake la asili la kusini mashariki.

Mgombea mwenza wa Weah ni Jewel Howard-Taylor, mke wa zamani wa aliyewahi kuwa mbabe wa kivita na baadaye kuwa rais – Charles Taylor na anatarajia kutoa upinzani mkubwa kwa chama tawala na hasa kutokana na ufuasi wake mkubwa anaoudhibiti katika jimbo lenye watu wengi la Bong.

Mwingine katika upinzani ni sura ya zamani, Prince Kohnson wa chama cha Movement for Democracy and Reconstruction’s (MDR). Johnson ni maarufu katika siasa za Liberia, ingawa umaarufu wake umejikita zaidi katika jimbo lake la Nimba, ambako amekuwa Seneta kwa vipindi viwili.

Kudidimia kwa umaarufu wake kunatokana na harakati zake wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kwingineko wengi wanamuona kama ni mhalifu wa kivita tu.