Home Michezo Kimataifa LICHA YA USAJILI MAN CITY TATIZO LILE LILE

LICHA YA USAJILI MAN CITY TATIZO LILE LILE

821
0
SHARE
MANCHESTER, ENGLAND - SEPTEMBER 17: Raheem Sterling of Manchester City burst through the AFC Bournemouth defence during the Premier League match between Manchester City and AFC Bournemouth at Etihad Stadium on September 17, 2016 in Manchester, England. (Photo by Stu Forster/Getty Images)

KELVIN LYAMUYA NA MITANDAO

LICHA ya kupata pointi nne ndani ya mechi mbili za Ligi Kuu England walizocheza hivi karibuni, timu ya  Manchester City, inaonekana kusumbuliwa na changamoto zile zile ambazo kocha wao, Pep Guardiola alidhaniwa amezipatia ufumbuzi.

City ilicheza mchezo wa kwanza wiki iliyopita dhidi ya Everton na kulazimisha sare ya bao 1-1, bao la Raheem Sterling likiokoa angalau pointi moja katika mchezo huo.

Baada ya mchezo huo, City ilicheza tena juzi dhidi ya Bournemouth na kushinda mabao 2-1, huku mwokozi akiwa ni yule yule, Sterling, ambaye alifunga bao la ushindi ndani ya dakika saba za nyongeza, kwani ilionekana kama mchezo ungeisha kwa sare nyingine ya bao 1-1.

Kabla ya mchezo dhidi ya Everton, Guardiola alinukuliwa akisema kwamba kikosi chake hakina budi kupata matokeo mazuri nyumbani kwa hali yoyote ile ili kufuta udhaifu wa msimu uliopita.

Kwa namna moja au nyingine, ukiachana na ile kadi nyekundu ya Kyle Walker dhidi ya klabu hiyo ya Merseyside, kufuatia rafu mbaya aliyomchezea Calvert Lewin, City walikuwa na kikosi bora cha kuibuka na ushindi siku ile.

Lakini ilionekana City pamoja na Guardiola mwenyewe, walishakubali sare ingewatosha. Walishakubali kuzipoteza pointi mbili nyumbani.

Sio mwanzo mzuri kwa kikosi kama hicho ambacho kina wachezaji waliosajiliwa kwa fedha nono. Matatizo ya msimu uliopita bado yapo.

Moja ya tatizo lililowatesa sana Man City ni kuruhusu bao katika kila shuti la kwanza tu walilopigiwa, hii ilikuwa ikimpa hofu sana Guardiola. Tatizo hilo lilionekana si pungufu ya mara saba katikati mwa mwezi Januari msimu uliopita. Mhanga mkubwa alikuwa ni kipa Claudio Bravo, ambaye aliruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye mashuti saba aliyopigiwa kwa mara ya kwanza tu.

Kiuhalisia hatuwezi kumlaumu sana kipa mpya, Ederson, ambaye alifungwa bao na Wayne Rooney katika shuti la kwanza ‘on target’ la Everton dakika ya 35, muda mrefu baada ya City kuumiliki sana mpira na kukosa mabao ya wazi.

Kumlaumu Ederson ni mapema sana, lakini kamwe usitegemee kwamba lawama hazitofuata huko mbeleni.

Inawezekana kabisa, kutokuwa na safu imara ya ulinzi kwa City hupelekea hata kipa naye asijiamini langoni. Maana kuwa na uwezo ni jambo la kwanza, lakini kujiamini ambako kutakufanya ucheze

City kwa sasa inatumia mfumo wa mabeki watatu, Vincent Kompany, Nicolas Otamendi na John Stones. Ambao hadi sasa hawajaonesha mwanga kwamba watakuwa mabeki wagumu kupitika.

“Makosa siku zote husababisha woga na kila mtu hatomuamini mwenzake ndani ya timu kama mwanzo,” alisikika akisema mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa Man United, Garry Neville.

“Baada ya dakika 25 ilibidi awabadilishe nafasi mabeki wake wawili wa kati, ilionekana Otamendi alishindwa kumdhibiti Calvert-Lewin,” alisema Neville.

“Otamendi alishindwa kabisa. Kompany naye akawa mzembe kuzuia pasi ya bao isifike kwa Rooney ambaye aliachiwa nafasi kubwa na John Stones. Hivyo mabeki wote watatu walikuwa hovyo,” alimalizia Neville.

Aidha, City haikufungwa tena bao licha ya kupunguzwa uwanjani baada ya Walker kutolewa kwa kadi nyekundu. Na suala hilo nalo lilimvuruga sana Guardiola hasa msimu uliopita kiasi cha kuamua akutane na mkuu wa waamuzi England, Mike Riley kufuatia timu yake kunyimwa penalti baada ya Raheem Sterling kusukumwa na mchezaji wa Tottenham Januari mwaka huu, timu hizo zikitoshana nguvu ya kufungana mabao 2-2.

Katika mchezo huo, ukiachana na tatizo la mabeki, pia City ina udhaifu mkubwa wa kutotumia vyema nafasi nyingi wanazozitengeneza. Ukitazama takwimu ya mashuti waliyopiga siku ile ni 19, ila bao ni moja tena la kusawazisha.

“Tumejaribu kufanya kila kitu, hata sijui tumetengeneza nafasi ngapi?” alisema Guardiola baada ya mchezo huo kumalizika. Lakini, mtandao wa Opta ulionesha kwamba nafasi walizotengeneza City ni nzuri mara mbili zaidi ya zile za Everton.

Hata hivyo, kwa mara nyingine tena hakuna jipya . City ya Guardiola inaonesha dalili za kupenda kuishi na matatizo sugu.

Guardioa huwa ana jibu lake moja kila anapoulizwa na waandishi wa habari kwamba nini tatizo hadi kushindwa kupata matokeo mazuri, naye hujibu kwa kusema siku hiyo ni yenye faraja zaidi katika maisha yake. Yaani ameridhika na yote.

Ni zimwi ambalo halimjui Guardiola. Litayatafuna maisha yake Etihad. Litaivuruga klabu kama akiendelea kuwa mwoga wa kutafuta suluhisho.

Mchana wa Jumamos iliyopita , waliivaa Bournemouth ugenini, unaweza kusema walionesha mabadiliko lakini ikumbukwe, timu waliyocheza nayo haina nguvu zaidi ya City.

Lakini, kama haina nguvu mbona walitegemea bao la usiku namna ile? Tunarudi pale pale, udhaifu wa kutotumia nafasi vizuri na itachukua muda mrefu sana kama Guardiola akiwa mzito kutafuta suluhisho. Tuendelee kuwaangalia mwanzo wao huu utakuwaje. Ndipo tutajua mwisho wao utakavyokuwa.