Home Michezo LIGI KUU TIMU ZAANZA HESABU ASUBUHI

LIGI KUU TIMU ZAANZA HESABU ASUBUHI

1036
0
SHARE

NA AYOUB HINJO

HATIMAYE Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza. Ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Raundi ya kwanza ya michuano hiyo imedhihirisha kila timu imejidhatiti kufanya vizuri hasa katika michezo yake ya kwanza, licha ya timu nyingine kuanza kwa kufungwa lakini bado mabadaliko makubwa ya kila timu yalionekana.

Lipuli, Singida United na Njombe Mji zimepanda kwa mara ya kwanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara. Je watafanya nini  kwenye ligi ifikapo mwisho wa msimu?. Tusubiri.

Wikiendi hii ligi itasimama kupisha timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ kucheza mechi ya kirafiki kwa mujibu wa kalenda ya FIFA. Bila shaka kipindi hiki kitatumika vizuri kwa timu zilizopoteza mechi zao za kwanza kujiuliza na ikibidi kurekebisha mapungufu waliyoyabaini.

Hivi ndivyo timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zilivyoanza katika michezo yao ya kwanza, lakini kwa ufupi tuangalie taswira iliyoonekana baada ya mechi za kwanza.

Ni mapema mno kuanza kutabiri nani atatwaa ubingwa au atashuka lakini bado matokeo ya mechi za kwanza pamoja na ubora wa vikosi vyao inaweza kuwa sehemu ya utabiri huo.

Simba

Wamefanikiwa kuanza ligi kwa ushindi mnono, wamewafunga wazoefu wa michuano hiyo Ruvu Shooting kwa mabao 7-0. Emmanuel Okwi alianza kw akuweka historia msimu huu kwa kufunga bao la kwanza la michuano lakini pia akaweka historia nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga ‘Hatrick’ msimu huu.

Ukiachilia hilo pia amefanikiwa kufunga idadi kubwa ya mabao kwani katika mchezo huo dhidi ya Ruvu Shooting amefunga mabao manne peke yake kati ya saba iliyotupia.

Msimu uliopita timu hiyo haikuwahi kushinda zaidi ya mabao manne hivyo tayari inaonesha wazi ushindi huo ni dhahiri unafungua msimu huu kwa ujumbe mzito kwa timu zingine zinazoshiriki Ligi hiyo.

Mashabiki wa timu hiyo wana matarajio makubwa na timu yao msimu huu hasa wakijivunia usajili mzuri unaotajwa kufikia shilingi Bilioni 1.3 huku wakichagiwa na uwepo wa mastaa kadhaa kama vile Aishi Manula, John Bocco, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi. Kile kilichotokea wiki iliyopita kinaonyesha wamejipanga vizuri katika safu ya ushambuliaji kwa kutumia vema nafasi wanazopata.

Simba ni moja ya timu inayoangaliwa zaidi na wapinzani wao kutokana na usajili walioufanya kwani wengi ni wazoefu wa ligi hiyo. Wanaonekana wana uchu na kombe hilo ambalo kwa miaka mitano sasa hawajafanikiwa kulirudisha msimbazi.

Yanga

Mabingwa watetezi wameanza ligi kwa kasi ndogo ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli ambayo imepanda daraja msimu huu.

Bado wanaonekana hawajatulia vizuri, kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu kwenye kikosi cha kwanza kumeacha pengo ambalo halijazibwa kwa asilimia 100.

Simon Msuva, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Haruna Niyonzima  walikuwa wachezaji muhimu sana. Msuva alikuwa mtengenezaji mzuri wa mabao na hata kufunga pia. Msimu uliopita alikuwa kinara wa kiatu cha dhahabu baada ya kufungana na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting kwa mabao 14.

Pengo la Msuva ni dhahiri halijapata wa kuliziba kwani katika mechi chache ilizocheza timu hiyo kuanzia maandalizi na hata ile ya kwanza dhidi ya Lipuli imedhihirika wazi Raphael Daud si mbadala wake kwani ni mzito na ameshindwa kuanzisha mashambulizi hasa yale ya pembeni .

Niyonzima alikuwa mchezaji muhimu ndani ya Yanga kutokana na uwezo wake kusambaza vema mipira iliyozaa matunda kwa kufunga mabao. Alikuwa kiungo safi katika kujenga mashambulizi ya timu.

Pamoja na kuwa kuna ingizo jipya la Tshishimbi Kabamba ambaye katika mechi ya Ngao ya Jamii alionesha kiwango kizuri lakini katika mechi ya kwanza ya Ligi akashindwa kuonesha makeke yake ni dhahiri ugeni ndani ya ligi hiyo ulichangia kutoonekana.

Bila shaka kadri ziku zinavyokwenda na kuanza kuzoea mazingira ya Tanzania na ligi yenyewe ataweza kuwaponesha mashabiki wa Yanga jeraha la kuondoka kwa Niyonzima.

Kwa wakongwe hao sare inaweza kuwa sio ishu sana kwani uzoefu unaonesha mara nyingi huanza michuano hiyo kwa kusua sua lakini baadaye kuongeza mwendo na kuishia kutwaa taji hilo ambalo ni kubwa kuliko yote nchini.

Azam

Walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mjini Mtwara.

Unaweza kusema kikosi cha Azam ni kipya kwa asilimia 50 kutokana na kuondokewa kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza waliojiunga Simba (wanne), Yanga (mmoja), Singida United (mmoja). Kwa mtazamo huo wa kuondokewa na wachezaji wa kikosi cha kwanza wapatao sita unaweza kuona ni kama inasukwa upya sasa.

Huenda faida ya kuanza maandalizi mapema pengine kuliko timu nyingine yoyote imezaa matunda kwa kufanikiwa kuwa na ‘chemistry’ nzuri kwa timu.  Ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Ndanda ni ishara nzuri ya safari yao kuelekea kulisaka taji la Ligi Kuu.

LIPULI

Wamepanda kwa mara ya kwanza msimu huu. Mchezo dhidi ya Yanga walionekana kucheza kwa kujihami zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kutokana na ukweli kuwa wapinzani wao walikuwa na kikosi bora ukilinganisha na wao.

Pengine uzoefu wa Ligi aliuonao kocha wao Selemani Matola ambaye alishawahi kuwa kocha Msaidizi wa Simba, ndio uliomfanya kukuna kichwa na kuja na mfumo bora ulioweza kuwabana wapinzani hao na kuwapa kazi ya ziada kuweza  kusawazisha bao walilotangulia kuwafunga.

Awali kabla ya Ligi kuanza ilionekana kama vile hawatakuwa na cheche zozote katika ligi hiyo hasa kufuatia mgogoro wa muda mrefu ulioiandama timu hiyo sambamba na ukata.

Mechi za majaribio zilidhihirisha hilo lakini hata hivyo usajili wa dakika za mwisho kwa wachezaji wachache na wazoefu umeonekana kuibeba timu hiyo.

Omega Seme (kiungo), Asante Kwessi, Paulo Ngalema, Novert Lufunga (mabeki) na Malimi Busungu (mshambuliaji) ni kama sasa umezaa tumaini jipya kwa wana Lipuli.

Kiwango walichoonesha katika mechi yao ya kwanza ugenini imejenga taswira nyingine kabisa kwamba itatoa upinzani msimu huu hivyo kwa sasa ni moja kati timu zinazoangaliwa watamaliza nafasi ya ngapi mwisho wa msimu ukifika.

Mji Njombe

Kama ilivyo kwa Lipuli, hata Mji Njombe nao wamepanda daraja msimu huu. Wameanza michuano vibaya kwa kichapo kutoka kwa wakongwe wa Ligi hiyo Prison kwa kufungwa mabao 2-0.

Bado hawajaonyesha kiwango kizuri, inawezekana ugeni wa ligi au maandalizi hayakuwa mazuri. Ubora wa kikosi chao bado haujawapa matumaini makubwa mashabiki wa soka kutokana na aina ya wachezaji waliosajiliwa na kiwango walichoonesha katika mechi ya wkanza.

Wengi ni chipukizi na hata wale wachache wakongwe sio wenye majina ya kutisha katika soka la Tanzania. Hata wao wanaangaliwa kama wataweza kusalia kwenye ligi ikifika tamati.

Singida United

Ni timu iliyopanda daraja msimu huu. Licha ya ugeni wake lakini usajili wake ulitingisha sana hasa baada ya kuchukua majina makubwa katika soka ndani na nje ya nchi.

Tofauti na mjatarajio ya wengi kwamba itatoa upinzani mkubw lakini matokeo ya mechi ya kwanza tu tayari imewavunja nguvu mashabiki wa soka wakianza kuingiwa na shaka kama wataweza kuhimili mikikimikiki ya ligi hiyo.

Wachezaji saba wa kigeni wanne kati ya hao kutoka Zimbabwe,mmoja Uganda na wawili Rwanda wakichagizwa na wazoefu kama Deus Kaseke, Nizar khalfan, Ally Mustapha ‘Bartez’, Peter Manyika, Miraji Adam, Atupele Green na Kigi Makassy wameonekana bado hawajaweza kutengeneza ‘Chemistry’.

Mchezo wao wa kwanza walifungwa mabao 2-1 na kikosi kisichotisha sana cha Mwadui. Ilishangaza kidogo kuona timu yenye kikosi ghali, wakipoteza mchezo dhidi ya timu ambayo haijatumia hata robo ya bajeti kuwafikia.

Wanahitaji kucheza michezo mingi ili timu yao ijijenge kitimu zaidi. Kwa muda huu wanaye kocha mzoefu, Hans van Pluijm anayejua soka la Tanzania linahitaji nini.

Pamoja na kutumia fedha nyingi, mashabiki wengi wanaitaza kwa jicho lingine, je watafanya maajabu gani licha ya kusumbua katika maandalizi na hata usajili?.

Mwaka 2012 timu ya Queen Park Rangers ya nchini England walitumia bajeti kubwa katika uwekezaji lakini walishuka daraja, je hadithi inaweza kuwa kama hiyo kwa Singida United? Muda utaamua.

Bila shaka mechi katika mechi za raundi ya pili na kuendelea itatoa picha halisi ya nini kitatokea katika michuano hiyo msimu huu.