Home Makala LINI MAREKANI ILIKUWA ‘TAIFA KUBWA’ DUNIANI?

LINI MAREKANI ILIKUWA ‘TAIFA KUBWA’ DUNIANI?

1659
0
SHARE

Donald Trump

NA HILAL K SUED

KATIKA hotuba yake baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, Januari mwaka huu, Rais Donald Trump, aliahidi kuirudishia nchi hadhi yake kama ‘taifa kubwa’ duniani. Lakini swali linalokuja mara moja hapa ni je, ni lini Marekani iliwahi kuwa taifa kubwa duniani?

Kwa wanazuoni wengi, achilia mbali wahanga wa historia ya dunia hii, swali ni hilo hilo – lini Marekani ilipata kuwa taifa kubwa.

Jibu la swali hili haliwezi kupatikana katika tukio la udondoshaji wa mabomu ya atomic (nyuklia) nchini Japan mwaka 1945, au kemikali za sumu walizomwagiwa wananchi wa Vietnam, au hata katika mabomu yaliyotegwa ardhini nchini Laos na ambayo hadi sasa hivi yanalipuka na kuwaua na kuwapa ulemavu wananchi miongo mitano baada ya ile ‘vita ya siri’ iliyoendeshwa na Marekani katika nchi hiyo.

 

Katika miaka ya 1970, Marekani iliendesha vita ya siri dhidi ya Laos kutokana na nchi hiyo kukubali kupitisha misaada ya kijeshi kutoka China na Vietnam ya Kaskazini kwenda kwa wapiganaji wa Kikomunisti wa Vietnam ya Kusini, waliokuwa wanapambana na majeshi ya Marekani.

 

Hata mauaji yaliyokuwa yakifanywa na tawala za kidikteta za Amerika ya Kusini zilizokuwa zinaungwa mkono na Marekani, haziwezi kutoa sababu ya Marekani kuwahi kuwa taifa kubwa kihistoria.

Vivyo hivyo kwa mauaji ya maelfu ya raia yaliyotokea au yanayoendelea kutokea Afghanistan, Iraq, Yemen na maeneo mengine kutokana na mashambulizi ya anga ya ndege za Marekani na washiriki wake, na ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiainishwa kama ni “athari isiyokusudiwa,” (collateral damage).

Na nchini Marekani kwenyewe, dhana nzima ya “ukubwa wa taifa” hilo imekuwa haieleweki vyema – labda iwapo tuchukulie, ina maanisha utamaduni wa karne nyingi wa kuwaangamiza wananchi wazalendo (Red Indians), watu weusi (wa asili ya Afrika) na wengine wowote ambao hadhi zao ziko tayari kufutiliwa mbali kwa manufaa ya ukandamizaji wa tabaka la watu weupe.

Aidha, kipaumbele cha Marekani katika ‘afya’ ya sekta ya utengenezaji wa silaha ambayo ndiyo nguzo ya mfumo uliopo wa ubepari, kinawekwa kwa gharama za maisha ya watu wa nje na wa ndani ya nchi hiyo.

Katika kitabu chake ‘A People’s History of the United States’ – yaani ‘Historia ya Watu wa Marekani’, mwanahistoria mmoja wa nchi hiyo, Howard Zinn, ametaja kipindi kimoja cha matumizi ya kijeshi katika miaka ile ya Vita Baridi (Cold War) kwamba nyambizi moja ya aina ya Trident ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa na wa kutisha, ilikuwa haina kazi yoyote isipokuwa wakati wa vita ya nyuklia tu. Gharama ya utengenezaji wake ni Dola za Kimarekani 1.5 bilioni.

Zinn alisema kiasi hiki cha fedha kilitosha kugharamia chanjo za watoto dhidi ya magonjwa hatari kwa miaka mitano duniani kote na kuepusha vifo milioni tano.

Lakini ni wachambuzi wachache tu wa kufananishwa na Zinn ambaye bila kuchoka alifichua kazi na misingi ya kiuchumi, uhamishwaji watu kwa nguvu au kwa hila, uporaji na unyonyaji – vitu ambavyo vimetendeka nchini humo tangu ujio wa baharia Christopher Columbus katika safari yake iliyoitwa ya “uvumbuzi” wa eneo hilo la dunia mwaka 1492.

Sasa hivi mtu mmoja tajiri anatishia kuifanya Marekani kuwa taifa kubwa tena. Lakini kwa vile “ukubwa wa Marekani” siku zote umekuwa ukihusishwa na ukandamizaji kila mahali, itakuwa si makosa iwapo tutaitilia sana mashaka azma yake hiyo.

Aidha, tungekubaliana naye moja kwa moja iwapo, kwa mfano, polisi wa nchi hiyo wangesitisha tabia yao ya kuwaua kwa risasi watu weusi wasiokuwa na hatia.

Na kwa bahati mbaya, mfumo wa elimu wa Marekani uliundwa ili kufuata sera rasmi za utawala. Wanafunzi wanaleweshwa na dhana ya “utofauti” wa nchi yao katika medani ya dunia ili kufunika uozo katika jamii, huku sera za nchi hiyo kwa nchi za nje zinaelezwa kuwa ni kuendeleza uhuru na demokrasia kwamba zinatokana na utamaduni wa kiasili wa “taifa hilo kubwa.”

Agosti mwaka jana kipindi kimoja cha chaneli ya CNN – ‘CNN Money’ kilitangaza kwamba, katika ripoti ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Congressional Budget Office) matajiri wa nchi hiyo wanazidi kutajirika, ambapo asilimia 10 ya raia wa nchi hiyo wanamiliki asilimia 75 ya utajiri wote katika jamii. Ripoti iliongeza kwamba nusu ya chini ya watu wa Marekani walibakiwa na asilimia moja tu ya keki yote ya taifa.

Wachambuzi wengine wa mambo wanasema umaarufu wa Marekani umeanza kupotea kwa miaka kadhaa sasa na umejikita katika kitu kingine kabisa, hali ya mabadiliko inayoendelea duniani kote. Karibu katika kila fani na katika hali yoyote ya maisha, picha inayopatikana ni kwamba mpangilio wa mambo ulivyokuwa huko nyuma unavurugwa.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika kumbukumbu za binadamu walio hai, Marekani haionekani kuwa inaongoza duniani katika masuala kadhaa. Wamarekani wanaona dhahiri kuwa dunia mpya inajitokeza, lakini wasiwasi wao ni kwamba, muundo wake unapangiliwa na nchi za nje na watu wa nje kabisa na si Marekani au Wamarekani.

 

Hebu tupa macho yako tu huku na kule. Jengo refu kuliko yote duniani liko Dubai. Lile la Marekani la Sears Towers la Chicago lililokuwa refu zaidi lilipitwa tangu 1998 na lile la Kuala Lumpur, Malaysia. Kampuni kubwa ya kujitangaza (publicity firm) iko Ubelgiji, China. Kiwanda kikubwa cha kusafishia mafuta kinajengwa India. Ndege za abiria kubwa kuliko zote zinatengenezwa Ulaya (Airbus).

 

Tuendelee: Mfuko wa uwekezaji (Investment Fund) mkubwa kuliko yote duniani uko Abu Dhabi. Sasa hivi sehemu kubwa inayotengeneza filamu kwa wingi ni Bollywood, Mumbai, India, na si Hollywood kule Marekani. Kwa maana hii wacheza sinema maarufu wa Marekani wanaanza kupoteza umaarufu wao kwa watu wa taifa la nje.

 

Tuendelee tena: Kamari (gambling) kubwa duniani sasa hivi inachezwa Macao, Pwani ya China, mji ambao miaka minne tu iliyopita uliupita mji wa Marekani wa Las Vegas kwa mapato kutokana na kamari.

 

Marekani pia si maarufu tena katika fani wanayoipenda wananchi wake, kama wanunuzi wakuu wa bidhaa yaani ‘shopping.’ Duka lililokuwa kubwa la bidhaa nchini Marekani – Mall of America – lililoko Minnesota sasa hivi haliwezi kuwamo katika orodha ya kumi bora duniani.

 

Na kutokana na orodha ya sasa hivi ya mabilionea wakubwa duniani, ni Wamarekani wawili tu ambao wamo katika orodha ya mabilionea kumi wakubwa duniani.

 

Kwa ujumla orodha ya vitu hivi, huenda ikawa ya kipuuzi tu, au pengine ya ujinga ujinga tu, lakini rudi tu miaka 15 iliyopita ambapo Marekani ilikuwa inaongoza katika karibu vitu vyote hivyo.

 

Vitu hivi vinaashiria kuhama kwa hali ya uwezo na fikra. Hali hii inaonekana dhahiri kwa Mmarekani yeyote anayetembelea nchi za nje. Nchini Marekani, wananchi bado wanajadili hali na sababu za dunia kuipinga Marekani. Kuna baadhi yao wanasema hali hii ni halisi kabisa na ni kitu cha kutia wasiwasi na kwamba, ni muhimu kwa Marekani kujaribu kuiita tena dunia iwe upande wake.

 

Wengine wanasema kwamba hali hii (ya kutengwa na dunia) haiepukiki na ndiyo gharama ya kuwa taifa lenye nguvu, kwani nchi nyingi zinazoipinga Marekani zinaona wivu tu na hivyo hizo zinaweza zikapuuzwa tu bila ya kutokea madhara yoyote.

 

Lakini wakati Wamarekani wanaendelea kujadili suala la kwanini wanachukiwa na dunia, dunia yenyewe inaonekana kusonga mbele na kuanza kuelekeza macho yake sehemu nyingine ambazo inaona itapata masilahi zaidi.

 

Kwa kifupi dunia inaondokana kabisa na ile dhana ya “kuichukia Marekani” (anti-Americanism) na kuanza kuingia katika hali ya kuachana kabisa na Marekani (yaani post-Americanism).

 

Sasa hivi dunia inajaribu kujifunza kutoshabikia hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Marekani na hivyo kuanza kutoitegemea nchi hiyo. Wanaanza kuiona nchi hiyo kama ya kawaida tu na kwamba hata nchi nyinginekama vile China, inaweza kufikia hatua ya maendeleo iliyofikiwa na nchi hiyo na pengine kuipita. Na China sasa hivi inayo mwelekeo huo bila ya wasiwasi wowote.

 

Hebu fikiria: Katika mwaka 2006 na 2007, uchumi wa takriban nchi 124 za dunia ulikua kwa kiwango cha asilimia nne. Nchi hizi ni pamoja na nchi 30 katika Bara la Afrika. Na kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita, uchumi wa nchi zilizoko nje ya zile nchi za viwanda za Magharibi umekuwa ukikua kwa kiwango cha juu kushangaza.

 

Mwanauchumi Antoine van Agtmael, aliyebuni maneno “masoko yanayojitokeza” yaani (emerging markets) ameainisha makampuni makubwa 25 ambayo ana uhakika yatakuwa makampuni makubwa kabisa (multi-corporations) duniani.

 

Katika orodha hiyo kuna Brazil, Mexico, Korea ya Kusini ambayo ina makampuni manne kila moja, makampuni matatu kutoka India, mawili kutoka China na kampuni moja kila moja kutoka Argentina, Chile, Malaysia na Afrika ya Kusini.

 

Hali hii inaonyesha kuibuka kwa wengine duniani – yaani Kiingereza “the rise of the rest.” Ni dhahiri dunia inashuhudia uhamaji mkubwa wa kiuwezo.