Home Habari Lipumba, Maalim Seif  ‘waungana’

Lipumba, Maalim Seif  ‘waungana’

1852
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA

Kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Liwale zinaweza kurejesha muungano, ushirikiano na mshikamano mpya wa kisiasa ndani ya Chama cha Wananchi –CUF, RAI linachambua.

Ukweli wa hilo unadhihirishwa na namna viongozi hasimu wa chama hicho, Profesa Lipumba (Mwenyekiti) kwa upande mmoja na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu) kwa upande mwingine kila mmoja na kundi lake kumuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo Mohammed Mtesa.

Mtesa mbali ya kuhusishwa na upande wa Maalim Seif, kwa sasa anatajwa kuwa katikati ya makundi hayo mawili hali inayomfanya kukubalika na pande zote mbili huku kila moja ikiwa na utayari wa kumnadi kwa gharama na kiwango cha juu.

Upande wa CUF ya Prof. Lipumba ambaye anatambuliwa na Msajili wa  vyama vya siasa nchini, unajinadi kumteua mgombea huyo kama ilivyo kwa upande wa Maalim Seif ambaye anaungwa mkono na baadhi ya vyama vya upinzani kikiwemo Chadema.

Muungano wa matendo wa Maalim Seif na Prof. Lipumba umeanza kuonekana kwenye kampeni za Mtesa, tayari upande wa Lipumba umeshafungua kampeni za mgombea huyo  huku upande wa Maalim ukiwa tayari kwenda kufunga kampeni hizo, hatua inayoonekana huenda ikawakutanisha mahasimu hao kwenye jukwaa moja.

Kama hiyo haitoshi upande wa Prof. Lipumba umeweka wazi kuwa uko tayari kufanya kazi na Maalim Seif kama atafuata taratibu za chama na hawatasita kumpatia walinzi ili aende kukinadi chama kwa nguvu na weledi Liwale.

Pamoja na mwelekeo huo wenye sura ya kusaka suluhu na kumaliza msuguano wa muda mrefu, ikumbukwe kuwa mgogoro wao tayari uko mahakamani.

Katika kile kinachooneka mwanzo mpya wa CUF, upande wa Profesa Lipumba ndiyo ulikuwa wa kwanza kutangaza kumuunga mkono Mtesa ikiwa ni pamoja na mwenyekiti huyo kushiriki katika kampeni za ufunguzi pamoja na kutoa baraka kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kulipitisha jina la mgombea huyo.

Siku chache baadae Maalim Seif, ambaye mbali ya kutotambulika NEC, lakini pia kwa muda mrefu amekuwa kinyume kabisa na upande wa Prof. Lipumba aliibuka na kuweka wazi kuwa wanamuunga mkono Mtesa.

Katika kudhibitisha kuwa CUF ya Maalim Seif itafunga kampeni za Mtesa, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Mbarala Maharagande aliliambia RAI kuwa ni kweli chama chao kipo katika maandalizi ya kumpokea Katibu Mkuu huyo ili afunge kampeni hizo Oktoba 12 mwaka huu.

Akizungumzia namna Mtesa alivyopitishwa, Maharagande alisema, kutokana na mgogoro uliopo ndani ya chama hicho, fomu za mgombea huyo zilipitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kupelekewa na upande wa Lipumba ambaye anatambuliwa na NEC.

Alisema kwa upande wao hawana ugomvi na mtu yeyote kwani lengo lao kuu ni kuhakikisha mgombea wa CUF anashinda ubunge katika jimbo hilo.

Aidha, alisema licha ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kususia chaguzi zote za marudio kwa upande wa CUF hawana mpango wa kususia.

“Huo ni msimamo wao kama chama nasi tunayo maoni yetu ya kudai demokrasia na haki ya kisiasa nchini, tumekuwa tukisusia chaguzi nyingi, mtakumbuka hata katika uchaguzi wa Kinondoni hatukushiriki kwa sababu hatukuwa tukimuunga mkono mgombea aliyepitishwa na Profesa Lipumba.

“Hapa ni tofauti kwa sababu tuna madiwani 13 kati ya 20, hivyo isingekuwa busara kwa ngome yetu hiyo kuiacha iteketee,” alisema Maharagande.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma CUF, Abdul Kambaya, aliliambia RAI kuwa hajui msingi wa mvutano kuhusu mgombea huyo unatoka wapi kwa sababu amepitishwa na upande wa Profesa Lipumba.

“Kwanza tunavutana na nani, mtu ambaye hayupo ofisini, hana nyenzo yoyote ya chama unavutana naye vipi, ni nani amewahi kumwona Maalim Seif, Liwale tangu awe Katibu Mkuu, hata kabla ya mgogoro uliomfanya kuwa Mkamamu wa Rais.

“Liwale imejengwa na wananchi wenyewe na Profesa amekaa pale siku 15, mimi nimekwenda nimekaa pale siku 15 kwa ziara tofauti, Maalim hajawahi kufika pale hawajawahi kumwona mtu anaitwa Maalim, mvutano unatoka wapi” alisema Kambaya.

KUSHINDA UCHAGUZI

Aidha, Kambaya alisema hawatarajii kuwapo kwa haki kutokana na wasimamizi wengi wa NEC katika ngazi za chini kuwa makada wa CCM.

“Utaona hata mgombea wetu wa udiwani katika kata ya Kibutuka amerudishwa na tume ngazi ya Taifa na aliondolewa kwa pinganizi la kipuuzi kabisa. Taabu ya chaguzi za Tanzania, tume haina watendaji hadi chini, huku chini inategemea makada walioteuliwa na Rais kusimamia masuala ya maendeleo ya nchi, hao ndiyo wanakuwa wasimamizi wa uchaguzi,” alisema.

Mapema wiki hii Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara (maarufu Bwege), alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema mgogoro baina ya pande hizo hasimu haujamalizika kwa sababu kesi bado iko mahakamani, lakini wote kwa pamoja wanaunganishwa na mgombea huyo.

Bwege alibainisha kuwa mgombea huyo yuko upande wa Maalim Seif, lakini kwa sababu anakubalika katika eneo hilo, upande wa Lipumba pia ukaona kuwa hauna budi kumuunga mkono.

Bungara aliongeza kuwa upande wa Profesa Lipumba uliweka masharti kwamba mwanachama yeyote anayetaka kusaidia kampeni za mgombea huyo lazima awe na barua kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu CUF (Bara), Magdalena Sakaya sharti ambalo alidai kuwa baadae liliondolewa baada ya kupingwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho.

KIINI CHA MGOGORO

Mgogoro ndani ya Chama hicho ulianza baada ya Mwenyekiti wake Profesa Lipumba kujiuzulu nafasi zake ndani ya chama hicho mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu, akipinga uamuzi wa kupitishwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) licha ya awali kushiriki kumkaribishwa katika umoja huo.

Baada ya kukaa nje ya ulingo wa siasa kwa miezi kadhaa mwaka 2016 Lipumba alirejea na kudai kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa chama hicho kutokana na chama hicho kutojibu barua aliyoiwasilishwa akiomba kujiuzulu wadhifa huo.

Mgorogo huo uliibua mjadala baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kumtambua Lipumba kama mwenyekiti jambo ambalo lilisababisha pande hizo mbili kukimbilia mahakamani.