Home Habari Lissu arudi ‘kitandani’

Lissu arudi ‘kitandani’

1672
0
SHARE

MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye katika siku za karibuni alikuwa na ziara katika nchi za Ulaya na Marekani kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya Kimataifa, amerejea tena kitandani wiki hii kufanyiwa upasuaji wa 23, tangu aanze kupatiwa matibabu Septemba 7, 2017 mara baada ya kushambuliwa kwa risasi, mkoani Dodoma.

Mara baada ya kushambuliwa Lissu alikimbizwa Nairobi nchini Kenya na huko ndiko upasuaji wake wa kwanza ulianzia.

Katika kipindi cha miezi minne alichokitumia akiwa kitandani hospitalini jijini Nairobi, Lissu alifanyiwa upasuaji wa maeneo mbalimbali ya mwili wake yaliyoathiriwa mara 17 na risasi.

Mara baada ya kupelekwa nchini Ubelgiji katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Campus ya Gasthuisberg, mjini Leuven, Januari mwaka jana Lissu alifanyiwa upasuaji wa 18 na hadi kufikia Desemba 31, 2018 alishapasuliwa mara 22.

Katika salamu zake za mwaka mpya wa 2019 Lissu alipata kusema kuwa tofauti na mwanzoni mwa mwaka jana, mwaka huu anarudi hospitali ili kumalizia safari ndefu ya tiba, iliyoanzia Hospitali ya Mkoa wa Dodoma siku ya kushambuliwa kwangu.

“Katika operesheni hii ya majuzi (Desemba 31, 2018) , timu ya madaktari bingwa ambao wamenitibu tangu nilipofika hapa Ubelgiji mapema mwaka jana, imeondoa kifaa kikubwa cha chuma kilichowekwa ili kuunganisha mfupa wa mguu wangu wa kulia, ambao uliumizwa vibaya katika shambulio la Septemba 7.”

Akizingumzia upasuaji wake wa 23, kwenye mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha Sauti ya Amerika (VOA), Lissu alisema bado hajapona lakini anaendelea vizuri na upasuaji huu wa wiki hii ndio utamwezesha kujua uimara wa afya yake.

“Siwezi nikazungumzia nimepona kwa asilimia ngapi, lakini naweza kusema kwamba naendelea vizuri, sijapona kwa sababu tarehe 20 ya mwezi huu (Februari) naenda kufanyiwa oparesheni ya 23, kwa hiyo sijapona ila naendelea vizuri,” alisema Lissu.

Kuhusu kurudi nyumbani, Lissu alisema siku yoyote daktari wake akimwambia anaweza kurudi, hatosita na badala yake siku inayofuata atakuwa ndani ya ndege kurejea Tanzania.

Lissu ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni ametembelea nchi za Ujerumani, Marekani na Uingereza pamoja na kufanya mahojiano na vituo vya habari vya Deutsche Welle (DW), Shirika la Habari la Uingereza (BBC) na Sauti ya Amerika (Voa).

Aidha, amefanya mihadhara na wasomi wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Kimataifa cha Elliot nchini Marekani.

Kauli alizopata kuzitoa katika mahojiano aliyoyafanya ziliwaibua wabunge, mabalozi, viongozi wa Serikali, wakuu wa wilaya na mikoa, viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa juu wa chama hicho kumjibu na wakati mwingine kukanusha madai anayoyaelekeza kwa serikali ama viongozi wake.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa hatua hiyo ya hoja za Lissu kuwaibua watu mbalimbali wa upande wa Serikali na CCM inatosha kuwa mtaji wa kisiasa kwa mwanasiasa huyo kusimama kwenye majukwa ya kuwania urais mwakani.

Tayari Lissu mwenyewe ameshaweka wazi kuwa endapo chama chacke kitampa nafasi hiyo ya kuwania urais yuko tayari kufanya hivyo kwani anaamini anaweza kufanya vizuri.

Aidha baadhi ya wafuatiliaji wa siasa nchini wanaamini kuwa huruma ya wananchi wengi dhidi ya Lissu pamoja na kauli mbalimbali nzito zinazotolewa na CCM na Bunge zinatosha kumbeba mbunge huyo wa Singida Mahsriki kwenye uchaguzi Mkuu ujao kwa nafasi yoyote ile atakayoiwania.

“Lissu ameshapata huruma kubwa ya wananchi. Matusi mengi anayotukanwa yanamjenga. Tumesikia Spika akisema watakatisha mshahara wake, huko nako ni kumjenga maana watu wanajadili mshahara huo. Yaani hatapata tabu kupigiwa kura kwa kuwa ameshajijenga wakati huu,”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dk Paul Luisulie alipata kueleza kuwa mpaka sasa athari za ziara ya Lissu zimeshaanza kuonekana, kwa kuwa mjadala ni mkubwa. Ndani ya CCM kwenyewe wanajadiliana na wa wapinzani pia kuna mjadala. Hiyo ni impact.

“Kwa upande wa CCM tunajua Rais Magufuli yupo, lakini kwa upinzani Lissu alishasema atagombea, Hata kama hawakuwa na mpango wa kumpitisha, lazima atakuwa na ushawishi mkubwa.”

Ujasiri wa Lissu unapaswa kuwa chachu kwa vijana ambao wanaamini harakati zake ni faida kubwa kwao kama atachaguliwa.

Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzni kwa nyakati tofauti, wameliambia RAI kuwa kwa sasa  Lissu ndio nembo halisi ya upinzani nchini hivyo anapaswa kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya urais kwenye uchaguzi Mkuu ujao.