Home Habari LISSU: NATAKA KURUDI NYUMBANI

LISSU: NATAKA KURUDI NYUMBANI

1951
0
SHARE
NA MWANDISHI WETU  | 

RAIS WA Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ameweka wazi kuwa anataka kurudi nyumbani. RAI linaripoti.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alifanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia jana kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg  ikiwa ni upasuaji wa 19 kwenye mwili wake ndani ya kipindi cha miezi saba tangu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka jana.

Afya ya Lissu imekuwa ikitengamaa kwa kasi siku hadi siku hali inayompa matumaini ya kurejea nchini na kuendelea na shughuli zake kama awali.

Tangu mwanasiasa huyo machachari apelekwe Ubelgiji  Januari 6, mwaka huu akitokea nchini Kenya, alipofikishwa muda mfupi baada ya kushambuliwa, afya yake imekuwa ikiimarika kwa kasi.

Katika mazungumzo yake ya wiki iliyopita Lissu alisema kuwa wapo watu wanaomtembelea na kumshauri akirejea nchini asijihusishe na mazingira yatakayohatarisha maisha yake.

Hata hivyo, amebainisha kuwa hafikirii kuacha na anazikumbuka harakati zinazoendelea nchini na kwamba anatamani kurudi.

“Nimekumbuka harakati zinazoendelea nyumbani, nataka kurudi, nikipona nitarudi ili nikashiriki kupigania utawala bora.”

MAENDELEO YAKE

Mwanzoni mwa wiki hii Lissu alinukuliwa na baadhi ya magazeti, akisema kuwa afya yake inaendelea kuimarika na sasa anaweza kusimama bila msaada wa magongo.

Hata hivyo, alisema madaktari wake wamemwambia kuwa kasi ya mfupa wake wa mguu wa kulia kuunga ni ndogo hali iliyowasukuma kumfanyia upasuaji mwingine ili kuharakisha uponyaji huo.

“Wameniambia wasipoingilia kati kuurekebisha mfupa huo itachukua muda mrefu kuunga na hata ukiunga hautaniondolea hatari ya kuvunjika tena baadae.”

Siku chache kabla ya kupelekwa Ubelgiji, Lissu alipata kuviambia vyombo vya habari vya kimataifa kuwa majeraha yote ya risasi yamepona na kwa kadiri ya maelezo ya madaktari risasi 16 ziliingia kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Hapa nilipo majeraha yote ya risasi yamepona na kwa kadiri ya maelezo ya madaktari kuna risasi 16 ziliingia sehemu mbalimbali za mwili wangu, nililetwa katika hospitali hii (Kenya) nikiwa vipande vipande.

“Miguu ikiwa imevunjka, mikono imevunjika na matumbo yamechanwa chanwa, nililetwa nikiwa katika hali mbaya sana, sikuwa mtu wa kupona.

“Lakini miezi mitatu baadae nimeweza kuwaeleza watu popote walipo duniani kwamba majeraha yote yaliyosababishwa na shambulio la kigaidi yamepona.

“Sehemu iliyobaki ni sehemu ya kufanya niweze kutembea, niweze kufanya shughuli za kawaida za kibinadamu ambazo kila mmoja wetu aliye mzima anazifanya na hiyo madaktari wanasema ni safari ndefu kidogo.

Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kubainisha kuwa madaktari wamemuhakikishia kusimama na kutembea tena kama ilivyokuwa awali.

ANACHOKUMBUKA

Alisema anaikumbuka siku ya mchana wa Septemba 7, mwaka huu alipofika nyumbani kwake, dereva wake alimwambia kuna watu wanawafuatilia nyuma yao na inaonekana si watu wazuri usifungue mlango.

“Nilipoangalia kwenye kile kioo cha pembeni cha gari yangu nikaona gari nyeupe, sikumbuki namba ikiwa inarudi nyuma kuangalia mahali tulipotokea, nikaona baada ya kurudi nyuma akatoka mtu mmoja kwenye siti ya nyuma akaenda kwenye siti ya mbele, nafikiri aliongea na mtu wa siti ya mbele kisha akarudi akaingia tena.

“Muda mfupi baada ya hapo, wakatoka watu wawili wembamba, nakumbuka ni wembamba si wanene, mmoja alikuwa amevaa kofia, walitoka wakiwa na bunduki si bastola, baada ya hapo nilisikia ni mshtuko na baada ya wiki mbili nikajikuta nipo Nairobi.

PALIPOJERUHIWA SANA

Lissu alisema sehemu kubwa aliyoumia zaidi ni juu ya mguu wake wa kulia ambao  ulishambuliwa sana.

“Walipoanza kunishambulia dereva wangu alinisukuma nikaenda upande wake, kwa hiyo nikaficha tumbo, kifua na kichwa na ndio maana sikuwa na jeraha kabisa tumboni, kifuani na hata kichwani.

“Risasi nilizopigwa zilipigwa miguuni na baadhi mikononi ndio maana maumivu makubwa yapo  kwenye mguu hasa wa kulia.

“Hizi risasi zilipigwa kila mahali katika gari, ile gari ina alama za risasi 38, lakini risasi nyingi zilipigwa sehemu nilipokuwa nimekaa.”

Lissu alisema tukio lake halielezeki na anaamini shambulio lake ni la kisiasa kutokana na misimamo yake mbalimbali ya kitaifa.

“Mimi nakaa kwenye majengo ya serikali, nyumba wanazokaa viongozi wa Serikali, yanalindwa kwa saa 24, mimi nimeshambuliwa kwenye eneo la parking ya magari ya jengo letu, haiwezekani picha za shambulio lile zisionyeshe shambulio, ukiniambia ni shambulio la majambazi tu, mimi majambazi watakuja kuniibia kitu gani, mimi sina chochote cha kuibiwa.”

HARAKATI ZAKE

Alipoulizwa kama atajiweka kando na harakati zake hasa zile za ukosoaji, Lissu alisema maisha yake yote ya utu uzima na hata ya utotoni na ya shuleni, yamekuwa ni maisha ya kupigania haki, kudai haki na anaamini mtu anaedai haki ni mpenzi wa Mungu mahali popote dunia.

“ Nasubiri nipone, kama ambavyo madaktari wangu wamesema, nitasimama,nitatembea na nitaendelea kudai haki kwa sababu nimekumbuka maandiko yanayosema haki huinua Taifa, ninataka kuinua Taifa langu Tanzania.”