Home Habari Lissu sasa abebeshwa upinzani 2020

Lissu sasa abebeshwa upinzani 2020

1167
0
SHARE

MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye sasa anazunguka katika nchi za Ulaya na Marekani kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya Kimataifa, anatajwa kuwa mwanasiasa anayetosha kupeperusha bendera ya upinzani kwenye mbio za urais mwakani. RAI linachambua.

Kwa sasa Lissu (Chadema) aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 20,  Septemba 7, 2017 anatazamwa kama ndiye mwanasiasa wa upinzani mwenye umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Pamoja na kufanya ziara zake hizo, Lissu anaeleza kuwa bado hajapona na anatarajiwa kufanyiwa oparesheni ya 23, Februari 20 mwaka huu.

Kutokana na mwenendo, kauli na matendo ya  Lissu katika siku hizi za karibuni hasa katika mahojiano yake na vyombo vya habari vya mataifa makubwa, wafuatiliaji wa siasa wanaamini kuwa mwanasiasa huyo kwa sasa amebeba ushawishi na mvuto wa kisiasa kwa jamii, hali inayompa uwezo wa kupeperusha bendera ya upinzani kwenye mbio za urais.

Wanaompa nafasi kubwa Lissu kwenye mbio za urais wanaamini kuwa uwezo wake wa kujenga hoja na namna alivyokikwepa kifo vinatosha kuwa mtaji wa kisiasa kwake na kwa upinzani kwa ujumla.

Akiwa kwenye mahojiano hayo Lissu hujikita katika kujenga hoja juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu akitumia matukio kadhaa kama shambulio dhidi yake na mengine yenye kufanana na hilo.

Lissu amekuwa akizungumzia kuminywa kwa demokrasia kama uhuru wa kujieleza akihusisha kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara, pamoja na madai ya kutoweka kwa baadhi ya watu.

Ziara na mahojiano yake hayo yameibua mjadala na majibizano makali kwa takriban wiki mbili sasa huku baadhi ya wanaompinga wakiweka wazi kuwa anachokifanya si sawa kwani anaichafua taswira ya nchi, serikali na viongozi wake.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa Lissu ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni ametembelea nchi za Ujerumani, Marekani na Uingereza pamoja na kufanya mahojiano na vituo vya habari vya Deutsche Welle (DW), Shirika la Habari la Uingereza (BBC) na Sauti ya Amerika (Voa).

Aidha amefanya mihadhara na wasomi wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Kimataifa cha Elliot nchini Marekani.

Kauli zake hizo katika mahojiano aliyoyafanya yamewaibua wabunge, mabalozi, viongozi wa Serikali, wakuu wa wilaya na mikoa, viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa juu wa chama hicho kumjibu na wakati mwingine kukanusha madai anayoyaelekeza kwa serikali ama viongozi wake.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa hatua hiyo ya hoja za Lissu kuwaibua watu mbalimbali wa upande wa Serikali na CCM inatosha kuwa mtaji wa kisiasa kwa mwanasiasa huyo kusimama kwenye majukwa ya kuwania urais mwakani.

Tayari Lissu mwenyewe ameshaweka wazi kuwa endapo chama chacke kitampa nafasi hiyo ya kuwania urais yuko tayari kufanya hivyo kwani anaamini anaweza kufanya vizuri.

Aidha baadhi ya wafuatiliaji wa siasa nchini wanaamini kuwa huruma ya wananchi wengi dhidi ya Lissu pamoja na kauli mbalimbali nzito zinazotolewa na CCM na Bunge zinatosha kumbeba mbunge huyo wa Singida Mahsriki kwenye uchaguzi Mkuu ujao kwa nafasi yoyote ile atakayoiwania.

“Lissu ameshapata huruma kubwa ya wananchi. Matusi mengi anayotukanwa yanamjenga. Tumesikia Spika akisema watakatisha mshahara wake, huko nako ni kumjenga maana watu wanajadili mshahara huo. Yaani hatapata tabu kupigiwa kura kwa kuwa ameshajijenga wakati huu,”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dk Paul Luisulie alipata kuhojiwa na gazeti na la Mwananchi na kueleza kuwa mpaka sasa athari za ziara ya Lissu zimeshaanza kuonekana, kwa kuwa mjadala ni mkubwa. Ndani ya CCM kwenyewe wanajadiliana na wa wapinzani pia kuna mjadala. Hiyo ni impact.

“Kwa upande wa CCM tunajua Rais Magufuli yupo, lakini kwa upinzani Lissu alishasema atagombea, Hata kama hawakuwa na mpango wa kumpitisha, lazima atakuwa na ushawishi mkubwa.”

Ujasiri wa Lissu unapaswa kuwa chachu kwa vijana ambao wanaamini harakati zake ni faida kubwa kwao kama atachaguliwa.

Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzni kwa nyakati tofauti, wameliambia RAI kuwa kwa sasa  Lissu ndio nembo halisi ya upinzani nchini hivyo anapaswa kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya urais kwenye uchaguzi Mkuu ujao.