Home kitaifa Lowasa ni nembo ya uongozi

Lowasa ni nembo ya uongozi

989
0
SHARE

Na JAVIUS KAIJAGE

KATIKA mazingira ya kawaida, ukizungumzia wanasiasa wanaofaa  kuwa viongozi wa ngazi za juu hata kuongoza dola, kamwe huwezi kumuacha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa.

Lowasa ambaye alipata kuwa Mbunge wa muda mrefu wa Monduli, anafaa kuwa kiongozi kutokana na historia yake ya muda mrefu au kwa maana nyingine mapito aliyoyapitia hadi hivi sasa.

Akiwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya nne iliyokuwa inaongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Lowasa alikumbana na kashfa kubwa ya Richmond iliyosababisha kupoteza kibarua chake mwaka 2008.      

Uwezo wa kufikiri kwa haraka na ukomavu katika siasa, Lowasa alipokomaliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili ajiuzulu, alifanya hivyo bila kusita kwa ajili ya mustakabali wa taifa.   

Nasema alifanya hivyo kwa ajili ya mustakabali wa taifa kwa maana ya kwamba, hadi sasa tuhuma za ufisadi anazotuhumiwa nazo hakuna ushahidi wa kujitosheleza kumtia hatiani na ndiyo maana hadi sasa hakuwahi kupelekwa mahakamani kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.     

Ni Dhahiri kashfa ya Richmond ya mwaka 2008 ilikuwa ni mtaji mkubwa kwa wanasiasa hususan wa  upinzani hadi kupelekea kupanda kwa idadi kubwa ya wapiga kura kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.     

Kila kona ya nchi ajenda kuu ya upinzani ilikuwa ni kuwaambia wananchi kuwa serikali iliyoko madarakani, imeelemewa na ufisadi ambao umefanywa na watendaji wakuu akiwemo Lowassa.      

Nani hakumbuki aliyekuwa Mbunge Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyojitahidi kuzunguka nchi nzima akimponda Lowassa kuwa ni fisadi mkubwa?      

Hata hivyo pamoja na wanasiasa wa upinzani kumponda Lowassa, bado ilipokaribia uchaguzi mkuu na mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kumpata mpeperusha bendera wake, upinzani uliweza kuzisoma alama za nyakati ili kuhakikisha wanapata ushindi.     

Inasemekana kuwa pamoja na Lowassa kutuhumiwa kwa ufisadi, bado wapinzani walielewa fika nguvu ya mwanasiasa huyu kuwa anao wafuasi wengi nyuma yake na hivyo kuwatega  CCM katika uteuzi wa mpeperusha bendera.     

Mtego wa vyama vya upinzani hususan Chadema kwa chama tawala ulikuwa hivi, endapo CCM itamtema Lowassa basi watamshawishi na kumsafisha uchafu wa ufisadi ili atumike kupeperusha vyama vyao kwani anao wafuasi wengi.    

Mtego wa pili ulikuwa ni endapo CCM itajisahau na hatimaye kumteua Lowassa kuwa mpeperusha bendera wake, basi vyama vya upinzani vitatumia kashfa ya ufisadi hususan ile ya Richmond kuwarubuni wapiga kura wamtose kwa kishindo.    

Ni ukweli usiopingika kwamba mazingira magumu ya mpasuko uliosababisha makundi ndani ya CCM, bila kusahau harufu za ufisadi yalisababisha kitendawili katika kumpata mpeperusha anayefaa.     

Ni kashfa ya Richmond isiyo na ushahidi  iliyosababisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kubaki njiapanda kwa kuwaza Lowassa ateuliwe kuipeperusha bendera ya chama kutokana na kuwa na wafuasi wengi, au atoswe kutokana na tuhuma alizonazo ili mwisho wa siku upinzani usije ukapata mtaji wa kunadi ufisadi.       

Yote katika yote CCM iliamua kumpa kisogo Lowassa kama njia ya kunusuru chama huku upinzani uliokuwa ukimbeza kuwa ni fisadi ukiamua kumtongoza na kumbatiza upya ili apeperushe bendera za vyama vyao (Ukawa) kama njia ya kunasa idadi ya kura nyingi za wafuasi wake ambao kimsingi walikuwa tayari kumfuata popote aendako.      

Hakika mitego ya vyama vya upinzani kwa kiasi kikubwa ilifanikiwa maana mara baada ya kumnasa Lowassa palikuwepo na harufu ya kitisho kuelekea katika uchaguzi mkuu kwani hata kwenye mikutano ya kampeni kati ya CCM na Ukawa ilikuwa ni vigumu kubaini atakayeibuka mshindi.       

Kama waswahili wasemavyo kuwa siasa ni mchezo mchafu, baada ya Lowassa kuhamia upinzani na kuonekana ni tishio kwa mgombea wa CCM, alianza kuchafuliwa vibaya na upande wa pili kwa maana ya wapambe wa CCM ili kuhakikisha anabwagwa chini.       

Wanasiasa ndani ya CCM walioteuliwa kuongoza kampeni katika uchaguzi wa mwaka 2015 akiwemo mwanasiasa machachari na mwenye uwezo wa kumwaga sera Nape Nnauye, walihakikisha kila kona ya nchi wanamwaga matusi ya nguoni dhidi ya Lowassa.      

Kinachoshangaza pamoja na matusi yote yaliyomwagwa kwa kumwita fisadi, mara mgonjwa, Lowassa hakujaribu hata siku moja kurudisha mapigo kwa kutumia ulimi wake au kwenda kushitaki  mahakamani.      

Ni Lowasa mwenye kuvumilia matusi na kebehi za wanasiasa wenzake bila kulipa visasi hata alipokuwa ndani ya CCM, ndani ya upinzani na kisha ndani ya CCM.     

Ni Lowassa mwenye moyo wa kutopenda kukurupuka katika kufanya maamuzi yanayoweza kupelekea  kuumiza wenzake baada ya kuambiwa maneno ya umbea, uongo au uzushi  hata alipokuwa waziri mkuu.        

Si tu ndugu Lowassa ni mvumilivu wa matusi na kebehi bali pia ni kiongozi  mwenye moyo wa kutopenda kuabudiwa/kunyenyekewa au kupewa misifa hata kama anafanya mambo makubwa kiasi gani.

Lowassa alipokuwa waziri mkuu, akitambua thamani ya uongozi kuwa kiongozi ni baba ndani ya familia, mara zote amekuwa akijiepusha kutumia ukali kupindukia au vitisho vinavyoweza kupelekea watoto wanapomuona akitokea matembezini wajifiche chini ya uvungu wa kitanda badala ya kumkimbilia na kuleta matatizo.      

Lowassa amekuwa ni kiongozi mwenye moyo wa kifua kwa kuvumilia kukosolewa na wanasiasa ndani ya chama chake CCM na ndani ya vyama vya  upinzani kwani hata alipokuwa waziri mkuu alikuwa na rungu lakini hakulitumia kuleta majeraha kwa wenzake kwa mahasimu wake.      

Hakika mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio haambiwi sikia kwani kipindi Lowassa akiwa waziri mkuu vyama vya upinzani, vilipewa uhuru wa uhakika kwani wapinzani mbali na kusema ukweli lakini kwa upande mwingine walikuwa wakizungumza mpaka uzushi kama sio umbea.       

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kisiasa, inasemekana uhuru mkubwa uliokuwepo kwa vyama vya upinzani katika kusema lolote huku waandishi wa habari za kiuchunguzi wakifanya kazi bila woga katika kipindi ambacho Lowassa alikuwa waziri mkuu, ilisaidia kwa kiwango kikubwa kuibua ufisadi hata kwa viongozi ambao hawakutegemewa kama wanaweza kufanya hivyo.      

Si tu Lowassa amekuwa akiheshimu mawazo kinzani ndani ya CCM na ndani ya vyama vya upinzani bali pia akitambua umuhimu wa kalamu ya mwandishi wa habari hakutumia nafasi yake ya uongozi kama mtendaji mkuu wa serikali kuwabana wanahabari hususan wale wenye vidomodomo, kwani alitambua kuwa kiongozi unaposifiwa kwa kufanya mazuri basi uwe tayari kutabasamu unapokosolewa pale  ukiteleza na wala siyo kununa.       

Lowassa akichukuliwa kama kinyonga asiyetabirika rangi yake hasa baada ya kutoa talaka kwa CCM, kwa kuhamia upinzani ili apewe madaraka makubwa na kisha kurejea tena ndani ya CCM, lakini kwa upande mwingine  anachukuliwa kama mwanasiasa anayefaa kuitwa kiongozi kuliko wanasiasa mamboleo ambao wengi wao ni watawala/wafalme.