Home Latest News LUCA PACIOLI MWANZILISHI WA UHASIBU DUNIANI

LUCA PACIOLI MWANZILISHI WA UHASIBU DUNIANI

4732
0
SHARE
NA KIZITO MPANGALA

UTUNZAJI wa fedha umepitia hatua nyingi tangu zamani. Hapakuwa na njia maalumu inayojulikana na wengi ambayo ingesaidia kutunza fedha na kuwa na kumbukumbu nzuri. Kila kampuni ilikuwa na utaratibu wake, pengine hata kuzichimbia chini fedha hizo.

Katika harakati mbalimbali za kitaaluma wataalamu mbalimbali walijaribu kuboresha mazingira ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha hasa katika mapato n matumizi ili kuepuka hasara au udanganyifu wa aina yoyote katika fedha. Kila zama zina mambo mbalimbali ya kusisimua na kwa kiwango chake.

Katika harakati za utunzaji wa kumbukumbu za fedha, leo tunamtazama mwanahisabati wa Italia, Luca Pacioli ambaye ndiye mwasisi wa mbinu ya kisasa ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha, na kutoa semina kwa kiasi kikubwa kuhusu tawi jipya la hesabu za biashara ambalo kwa sasa linajumuisha uhasibu.

Luca Pacioli alizaliwa mwaka 1447 katika Mji wa Sansepolcro nchini Italia. Katika mji huo alifanikiwa kupata elimu ya hisabati ambayo ilitolewa kwa lugha ya Kilatini. Elimu hiyo ya hisabati ilitolewa kwa mahitaji ya mapebari. Luca Pacioli alikulia katika famila ya rafiki ya baba yake, Mzee Bartolomea Pacioli.

Mwaka 1464, Luca alikwenda mjini Venice ambako alijiendeleza kwa kujisomea vitabu mbali mbali alipokuwa akiishi na familia ya bepari mmoja ambaye alimteua kuwa mwalimu wa watoto wake. Luca Pacioli, akiwa anawafundisha watoto hao, alitenga muda wa kujisomea binafsi.

Hapo aliamua kuandika kitabu chake cha kwanza kwa ajili ya watoto wa mwajiri wake. Kitabu hicho kiliitwa Summa de Arithmetica. Kilikuwa maalumu kwa ajili ya hatua za mwanzo za motto kujifunza hisabati.

Baadaye alisonga mbele zaidi na mwaka 1472 alijiunga na shirika la watawa wa kiume la Wafrancisca. Huko shirikani alijulikana kama Mtawa Luca. Aliaminika katika uwezo wake kitaaluma ambapo mwaka 1475 alianza kufundisha katika mji wa Perugia akiwa mwalimu binafsi.

Alikuwa akifundisha hisabati na aliandika vitabu zaidi ambavyo vilipendwa na wanafunzi wengi. Kitabu chake alichoandika ni Summa de Arithmetica, Geometria, Proportioni et Proportionalita ambacho kilichapishwa mjini Venice.

Mwaka 1497, aliitwa na Mkuu wa Mkoa wa Milan, Ludovico Maria Sforza, ili akafanye kazi huko. Akiwa Milan, Luca alikutana na Leonardo da Vinci na waliishi pamoja. Mwaka 1499, Luca Pacioli na Leonardo da Vinci, walitimuliwa mjini Milan wakati Mfalme Louis XII wa Ufaransa alipouteka mji huo.

Luca Pacioli aliandika vitabu vingi vya hisabati. Baadhi ya vitabu hivyo ni Tractatus Mathematicus ad Discipulos Perusinos, kitabu hiki kilikuwa na kurasa 600 ambacho alikwaandikia wanafunzi wake katika chuo kikuu cha Perugia ambako alifundisha kwa muda wa miaka mitatu.

Kitabu hiki kilieleza mengi kuhusu masuala ya hesabu za biashara ambapo kilitumika na mabepari wengi, pia kinapatikana katika jumba la makumbusho la Vatican. Kingine ni De Divina Proportione ambacho alikiandika alipokuwa mjini Milan.

Kitabu hiki kilieleza hesabu ambazo sasa zimeboreshwa zaidi na kutumika katika mafunzo ya usanifu majengo (Architecture). Leonardo da Vinci alijifunza hisabati kutokana na kitabu hiki na hivyo Luca Pacioli alimfundisha Leonardo da Vinci hisabati tangu walipokutana mjini Milan.

Kitabu ambacho kilwavutia watu wengi hasa mabepari wa Venice wakati huo ni Summa de Arithmetica, Geometria: Proportioni et Et Proportionalitia ambacho aliandika kwa lugha mama. Kitabu hiki ni cha kwanza duniani kuandikwa maarifa yanayohusu mbinu za kihisabati za utunzaji wa kumbukumbu za fedha ambapo sasa hujulikana kama uhasibu.

Katika kitabu hiki, Luca Pacioli alidadavua kwa kina na kuasisi sehemu kuu mbili za uandikaji wa hesabu za fedha. Sehemu hizo hujulikana kama “Mpe” na “Mtoe” (DEBIT na CREDIT, DR & CR) ambapo pande zote zinatakiwa kuwa na uwiano sawa wakati wa kufunga hesaby za fedha katika lipindi Fulani kadiri ya kampuni husika au taasisi husika. Kwa Kiingereza hujulikana kama Double-entry accounting system, Luca Pacioli ndiye mwasisi.

Alichokiandika katika kitabu hicho ndicho kile kifahamikacho sasa kama mzunguko wa fedha (Accounting cycle). Alidadavua matumizi ya majarida na sehemu za leja leja. Pia aliandika kwamba mtu hapaswi kwenda kulala hadi ahakikishe upende wa “Mpe” na upande wa “Mtoe” vinakuwa na uwiano sawa wakati wa kufnga hesabu za fedha.

Alielezea kuhusu kile kinachojulikana sasa kama Balance sheet na Income statement (waraka wa faida au hasara), vile vile alipendekeza ufungaji wa hesabu za fedha katika mwaka Fulani wa fedha ambapo sasa hujulikana kama Trial Balance kwa Kiingereza. Hutumika kutoa hakikisho la akaunti za leje leja zote zilizofunguliwa katika kipindi husika. Anajulikana kama Baba wa Uhasibu.

Kutokana na kazi yake hii ambayo sasa imekuwa ni msaada mkubwa katika biashara au jambo lolote linalohusisha matumizi ya fedha, kumeibuliwa vipengele vipya mabavyo navyo huhusiana na uhasibu. Vipengele hivyo ni kama vile maadili ya uhasibu, utoaji wa ripoti ya hesabu za fedha katika kipindi fulani kilichokubaliwa, na utaratibu mpya wa uhasibu unaohusu masuala ya gharama za mchakato fulani, huu hujulikana kama Cost Accounting, au Managerial Accounting ambao nao una mchakato mkubwa na mrefu. Nyongeza hizi zimeongezwa na wataalamu mbalimbali waliojifunza taaluma hii ili kuboresha ufanisi wa Uhasibu.

Luca ameiathiri dunia kwa athari chanya katika Uhasibu. Jambo hilo limezalisha vpengele vingine katika Uhasibu ambavyo kila kimoja kina utaratibu wa kipekee lakini ulio wa msingi ni ule ule ulioasisiwa na Luca Pacioli. Kuna utunzaji wa kumbukumbu za fedha unaohusu serikali pekee ambapo huingia katika taasisi isiyohitaji faida, yenyewe husimamia fedha zke zitumike kadiri ilivyopangwa, hivyo kumbukumbu za fedha hizo ni lazima.

Kuna utunzaji wa kumbukumbu za fedha zinazihusika katika shughuli za viwandani na kadhalika. Hii inaonyesha kwamba Uhasibu sasa ni taaluma pana na inahitaji maadili ya kipekee.

Luca Pacioli alifariki mwaka 1517 akiwa na umri wa miaka 70. Haluonana na rafiki yake kipenzi, Leonardo da Vinci, kwa muda wa miaka 10 tangu walipotimuliwa mjini Milan. Ingawa hakuwa na shahada yoyote, hakika kichwa cha Luca Pacioli kilibeba shahada za watu wengi duniani katika taaluma ya Uhasibu.